http://www.swahilihub.com/image/view/-/3349892/medRes/918919/-/ajvk65/-/DNAidsDay0112f%25283%2529.jpg

 

Jamii ijiepushe na mila zinazodhalilisha

Kupimwa hali ya HIV

Mtu katika kituo cha afya akipimwa kujua hali yake ya HIV katika Siku ya Ukimwi Duniani awali. Picha|BILLY MUTAI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, October 3  2018 at  01:00

Kwa Muhtasari

Kuna zaidi ya watu milioni 36.7 wanaoishi na virusi vya Ukimwi duniani mpaka sasa, huku watu milioni 20.9 wakitumia dawa za kufubaza.

 

MIONGONI mwa magonjwa ambayo yameitesa dunia kwa miaka mingi na bado hayajapata kinga wala tiba ni Ukimwi.

Ikiwa ni miaka 37 tangu ugonjwa huo ugunduliwe, umeendelea kupukutisha maisha ya watu wengi kila mwaka na mwaka 2017 tu, zaidi ya watu milioni 1.8 waliambukizwa virusi vya ugonjwa huo duniani kote.

Kuna zaidi ya watu milioni 36.7 wanaoishi na virusi vya Ukimwi duniani mpaka sasa, huku watu milioni 20.9 wakitumia dawa za kufubaza.

Tangu mwaka 1981 mtu wa kwanza alipogunduliwa kuwa na ugonjwa huo, jumla ya watu milioni 76 wameugua na tayari watu milioni 35 wamefariki dunia.

Juhudi mbalimbali zimefanyika kuutokomeza ugonjwa huo, lakini bado hazijafanikiwa kupata tiba wala kinga. Nchini Tanzania, watu milioni 1.5 wanaishi na virusi vya Ukimwi, huku asilimia zaidi ya 60 wakitumia dawa za kufubaza.

Idadi hiyo, inatutisha licha ya kampeni na jitihada zote za Serikali, taasisi za dini, asasi za kiraia na baadhi ya wadau wa afya, bado ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Licha ya tishio hilo, tunasikitishwa na baadhi ya mila na tamaduni ambazo badala ya kuwa suluhisho la kujikinga na gonjwa hilo, zinahamasisha maambukizi ya ugonjwa huo.

Tumeshtushwa na habari iliyochapishwa na gazeti hili toleo la jana, kuhusu mila ambayo bado inaenziwa na baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Ukara kilichopo Ziwa Victoria.

Pamoja na majanga ya kiafya yanayosababishwa na magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, mila hiyo inahamasisha watu waliofiwa na wenzi wao au ndugu katika ajali ya MV Nyerere kufanyiwa ‘utakaso’ kwa kufanya mapenzi na watu wengine.

Kutokana na mila hiyo, wafiwa hutengwa kwa kutoruhusiwa kuchangamana na wengine katika shughuli za kijamii hadi itakapofahamika kuwa wametakaswa.

Katika ajali hiyo, kivuko hicho kilichoanza rasmi kazi mwaka 2004 na chenye uwezo wa kubeba watu 100, kilipinduka kikiwa mita 50 kabla ya kufika kisiwa cha Ukara na takriban watu 230 wameripotiwa kupoteza maisha wakati wengine zaidi ya 40 walinusurika.

Tukio hilo linaweza kuangaliwa kwa mtazamo tofauti na jamii ya baadhi ya Wakara ambao wana mila kongwe ya kuwatenga watu wanaofiwa na wenzi wao katika majanga kama ajali za nchi kavu, angani na majini na pia wanaofariki kwa sababu za kawaida kama magonjwa.

Kwa mujibu wa wakazi wa Ukara, mila zinazotumika kuwatenga wafiwa hao zinajulikana kama Lichumu na Emisilo. Lichumu ni mila ya kuwatenga wanaofiwa katika matukio ya ajali, wakati Emisilo huwatenga wafiwa wa vifo vya kawaida.

Lichumu na Emisilo haiwatengi mume na mke pekee wanapofiwa, bali hata watoto ambao wazazi wao wamefiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella licha ya kwamba hakutaka kuzungumzia kwa urefu kuhusu kuwapo kwa mila hiyo, ameshauri watu kuepukana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, zikiwamo hizo za kuwatenga wafiwa kwa sababu zinawaongezea machungu.

Mongella aliwataka viongozi wa dini kueneza mafundisho kwenye jamii kama njia ya kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Tunaungana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwashauri kuachana na mila na desturi ambazo si tu zimepitwa na wakati, lakini zinaweza kuwaletea magonjwa kama Ukimwi.

Ni muda mwafaka pia kwa Serikali kuingilia kati na kuzuia baadhi ya mila na desturi ambazo zinadhalilisha utu wa binadamu na zenye madhara. Mila ambazo zinadhalilisha utu wa binadamu hazifai.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647