http://www.swahilihub.com/image/view/-/2758636/medRes/1040993/-/hpl66o/-/nyonyesha.jpg

 

Jamii ipewe elimu zaidi ya uzazi wa mpango

Mwanamke amnyonyesha mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, July 13  2017 at  11:33

Kwa Mukhtasari

Juzi ilikuwa Siku ya Kimataifa ya Idadi ya Watu Duniani na taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) inasema endapo matumizi ya uzazi wa mpango hayataongezeka nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 10 ijayo, idadi ya watu itafikia kati ya watu milioni 68 na 71 ikilinganishwa na idadi ya sasa ya watu zaidi ya milioni 47.

 

JUZI ilikuwa Siku ya Kimataifa ya Idadi ya Watu Duniani na taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) inasema endapo matumizi ya uzazi wa mpango hayataongezeka nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 10 ijayo, idadi ya watu itafikia kati ya watu milioni 68 na 71 ikilinganishwa na idadi ya sasa ya watu zaidi ya milioni 47.

Hata hivyo Serikali imeonyesha nia ya kukabiliana na changamoto hiyo na juzi katika mkutano wa kimataifa wa masuala ya uzazi wa mpango uliofanyika jijini London, Uingereza iliahidi kuongeza fedha kwenye eneo la kutoa huduma za uzazi wa mpango kutoka Sh 14 bilioni ifikapo mwaka 2020.

Sambamba na hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk Otilia Gowele aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho yaliyofanyika katika Uwanja wa Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam alisema huduma bora za kijamii zitawezekana endapo Taifa litadhibiti ongezeko La watu.

Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kudhibiti kasi ya ongezeko la watu kupitia uzazi wa mpango kwa sababu athari zake ziko katika viwango mbalimbali, ikiwamo ngazi ya familia.

Kuna ongezeko kubwa la watoto wa mitaani ambao wengi wao anatoka katika familia zenye idadi kubwa ya watoto na zenye kipato duni.

Familia nyingi nchini ambazo zinaishi katika mazingira ya ya umaskini zimekuwa na idadi kubwa ya watoto. Hali hii  inayoongeza mzigo kwa anayeihudumia. Pia familia za aina hiyo zimekumbwa na mikasa ya kukosa matunzo bora baada ya mlezi wake mkuu kuzitekeleza.

Takwimu zilizotajwa katika Bunge la Mwezi Aprili mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kuhusu ongezeko la idadi ya watoto wa mitaani kwa mwaka 2012 zinatisha. Waziri alisema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee kwa mwaka huo uliongoza kwa kuwa na watoto 5,600 kutoka mikoa 10 nchini.

Waziri Mwalimu  alisema watoto hao ni kutoka Dar es Salaam yenye asilimia 28,  Dodoma nane, Mwanza na Morogoro saba, Tanga sita, Iringa, Pwani na Kilimanjaro tano na Arusha nne.Tunaamini kuwa ni miaka mitano imepita tangu kutolewa kwa takwimu hizo, idadi ya watoto wa mitaani kwa maeneo hayo na mengine nchini itakuwa imeongezeka.

Mazingira magumu

Watoto hawa wanaishi katika mazingira magumu na yenye mazingira magumu na yenye changamoto nyingi ikiwamo kufanyiwa ukatili na watu waliowazidi umri. Hivyo jitihada za Serikali za kuongeza fungu kwenye mpango wa uzazi zitafanikiwa tu iwapo wananchi watakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Ni vyema Watanzania wakaweka nia madhubuti ya kuondokana na uzazi holela unaoongeza watoto wa mitaani ambao madhara yake ni mtambuka.

Inafahamika wazi juhudi za Serikali zimelenga kujenga uwezo wa kutoa huduma bora lakini familia nazo zinapokuwa na watoto ambao hawawezi kuwahudumia, madhara yake ni makubwa ikiwamo ongezeko la watoto wa mitaani.

Wito wetu kwa Watanzania ni vyema wakashirikiana na Serikali ili familia ziwe na watoto ambao wanaweza kupata huduma bora.

Hakuna maana ya kuwa na watoto wengi ambao wazazi hawawezi kuwapa huduma bora kama elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.