Jenga mtandao wa kiajira

Judith Nduva

Bi Judith Nduva msusi wa vikapu asili Kitengela Kaunti ya Kajiado, kwa kutumia nyuzi za sweta ama fulana. Hii ni kazi ya ziada inayompa donge nono, kando na ajira ya ofisi. Sheria za kupiga marufuku matumizi ya karatasi za plastiki nchini yumkini itaanza kutekelezwa baada ya Agosti 28, 2017 na ususi wa vikapu kwake Nduva ni dhahabu. Picha/ SAMMY WAWERU 

Na JENITHA WALTER

Imepakiwa - Friday, April 13  2018 at  12:47

Kwa Mukhtasari

Aghalabu kazi hutolewa kwa kujuana na hili si jambo la ajabu kwani watu hutoa ajira kwa wale wanaofahamu uwezo wao na kuwaamini.

 

NJIA ya kusubiri matangazo ya kazi ili uombe kazi imeshapitwa na wakati. Matangazo hayatoki kila siku, lakini watu wanaajiriwa kila siku.

Unadhani hawa wanaajiriwa vipi bila kazi kutangazwa? Kwa kifupi ni kuwa, kazi hutolewa kwa kujuana na hili si jambo la ajabu kwani watu hutoa ajira kwa wale wanaofahamu uwezo wao na kuwaamini.

Usikae ndani na vyeti na wasifu wako ukisubiri kazi itangazwe. Toka nje jenga urafiki na watu wenye ushawishi kwenye kutoa ajira, lakini pia wenye taarifa sahihi za masuala ya ajira na kazi.

Ukikutana na watu wa aina hii jitambulishe, chukua mawasiliano yao na hakikisha wanajua sifa zako na uhitaji wa ajira.

Watu wa namna hii wapo sehemu nyingi sana. Kanisani au msikitini kwako, kuna mkurugenzi wa kampuni fulani, kwenye vyombo vya usafiri unakutana na mameneja wa kampuni na wamiliki wa biashara mbalimbali, hizo ni fursa za kuwaunganisha kwenye mtandao wako wa kiajira.

Jenga mazoea nao ya kiuweledi na hakikisha unawatafuta mara kwa mara na hata kuomba kuwatembelea kwenye sehemu zao za kazi au biashara kama inawezekana.

Watu wenye uthubutu ndiyo wenye uwezo wa kutumia fursa mbalimbali, kuwa mthubutu mwenye ujasiri wa kufungua milango ya fursa na siyo kulalamika.