http://www.swahilihub.com/image/view/-/3841784/medRes/1583482/-/9xblm2z/-/deds.jpg

 

Juhudi za kumkomboa mwanamke ziungwe mkono

Siku ya Wanawake Duniani

Mkusanyiko wa picha zilizotengenezwa Novemba 7, 2016 zikionesha (kutoka juu kushoto) Rais wa Nepal Bi Bidhya Devi Bhandari, Rais wa Croatia Kolinda Grabar-Kitarovic, Rais wa Korea Kusini (anayekabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani) Park Geun-Hye, Ameenah Gurib-Fakim wa Mauritius, Waziri Mkuu wa Norwey Bi Erna Solberg, Rais wa Chile Michelle Bachelet, Chansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel, kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi, Rais wa Taiwan Bi Tsai Ing-wen, Rais wa Lithuania Bi Dalia Grybauskaite, Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina Wajed, Waziri Mkuu wa Poland Beata Szydlo, Rais wa Malt Bi Marie-Louise Coleiro Preca, Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May, Rais wa Visiwa vya Marshall Bi Hilda Hein, Waziri Mkuu wa Namibia Bi Saara Kuugongelwa-Amadhila na Rais wa Estonia Bi Kersti Kaljulaid. Machi 8, 2017 ni Siku ya Wanawake Duniani. Picha/AFP 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, March 8  2018 at  10:04

Kwa Muhtasari

Watanzania wanaungana na wenzao wa nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake.

 

LEO Machi 8 Watanzania wanaungana na wenzao wa nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake.

Kwa kawaida siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka hapa nchini kuwezesha wanawake kukutana kwa kuanza na maandamano yanayotawaliwa na ujumbe mbalimbali ya kuhamasisha maendeleo ya wanawake. Mada kadha wa kadha hutolewa zinazomhusu mwanamke na maendeleo yake.

Serikali yetu ni miongoni mwa zile zinazotoa kipaumbele kwa maadhimisho haya.

Siku hiyo kihistoria ilianza kwanza kwa kuitwa siku ya wanawake wafanyakazi ya kimataifa na ilikuwa ikiadhimishwa kila Machi 8.

Lengo la maadhimisho haya ilikuwa ni kumuonyesha upendo na heshima mwanamke kutokana na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Tunaweza kusema ni siku ambayo wanawake hutambuliwa kutokana na mafanikio yao bila kujali mgawanyiko wa taifa, kabila, lugha, itikadi, utamaduni, uchumi na siasa.

Kifupi ni siku ambayo husisitia kujenga mshIkamano wa wanawake wote duniani kuhamasisha jamii kutafakari kauli mbiu ya maadhimisho hayo.

Tunaweza kusema ni siku ambayo husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani kuhamasisha jamii na kutafakari kaulimbiu ya maadhimisho haya.

Wanawake wameanza kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo na zile za ngazi za uamuzi ikilinganishwa na siku za nyuma.

Historia inaonyesha kuwa awali wanawake walikuwa wanahofia hata kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya kijiji kutokana na hofu ya kutopewa nafasi na hasa mikinzano ya mila na desturi.

Hivyo, kama kauli mbiu ya mwaka 2018 inavyosisitiza, umefika wakati Serikali na wadau wengine kuunga mkono juhudi za wanaharakati ambao wanajitolea kuwaelimisha na kuwajengea uwezo wanawake kusonga mbele kielimu, kisiasa na kiuchumi.

Wakati siku hii ikiandhimishwa ni wazi kuwa inaendelea kutoa shime hasa kwa wanaharakati wa kike ambao shauku yao kuu ni kujitolea ili wenzao wananyanyuka na kuwa sehemu kamili ya ujenzi wa Taifa badala ya kuwa watazamaji na wasindikizaji.

Tumeshuhudia wanaharakati hao wakiwamo wale wa mijini na vijijini wakitumia nguvu nying ili kutaka kujua kila mwanamke anajikwamua kutoka utegemezi na kuwa mtafutaji ndani ya family yake na katika ujenzi wa Taifa kwa jumla.

Kwa hapa nchini tunasema kwamba siku hii ina maana kubwa sana hasa kwa mwaka huu wakati wanawake wakiiadhimisha, wanajivunia mafanikio ya kujikwamua kiuchumi kwa kuendelea kuimarisha  shughuli zao za ujasiriamali ambazo wanazifanya kila uchao sambamba na kujiimarisha katika nyanja za kielimu na kisiasa.

Pamoja na jitihada za Serikali za kutaka wanawake wanaboreshewa mazingira ya kufanya kazi hasa za ujasiriamali lakini wao binafsi na kupitia katika asasi na vikundi vya ujasiriamali wameweza kuthubutu kwa imani ya kufikia malengo ya maendeleo waliyojipangia.

Hivi sasa wengi wao wameamua kuungana na kuwa kitu kimoja na sauti moja wakiwa wamelenga kulinda na kutetea haki zao bila kujali itikadi zao za kisiasa, ukabila wala dini.

Hivyo sisi tunasema nguvu hii ya kumkomboa mwanamke iendane na kaulimbiu ya mwaka huu kwa wanaharakati kuongeza juhudi zao sababu mwanga umeshaanza kuonekana.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647