http://www.swahilihub.com/image/view/-/4926264/medRes/2218551/-/uq4sor/-/mjana.jpg

 

Meshack Omega: Kamishna kijana

Meshack Omega

Meshack Omega, naibu kamishna katika kaunti ndogo ya Loitoktok, na anayeshughulikia Tarafa ya Lenkisem. Picha/HISANI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  15:27

Kwa Muhtasari

Meshack Omega ni mfano wa kipekee kwamba kweli vijana wanaweza kuaminika wakipewa wajibu.

 

KATIKA umri wa miaka 29 pekee, huenda yeye ni mmoja wa manaibu makamishna vijana zaidi nchini Kenya.

Kutana na Meshack Omega, naibu kamishna katika kaunti ndogo ya Loitoktok, na anayeshughulikia Tarafa ya Lenkisem.

Kama wenzake wanaoshikilia wadhifa kama huu majukumu yake yakiwa uratibu wa shughuli za serikali ya kitaifa, usalama, utatuzi wa migogoro miongoni mwa mengine.

Lakini sio hayo tu yanayomfanya Bw Omega kunasa jicho la wengi unapozungumzia eneo hili. Katika miaka miwili ambayo amehudumu katika nafasi hii, afisa huyu wa serikali pia amekuwa mwanaharakati sugu katika vita vya kuhakikisha haki za mtoto msichana, kwa kupambana na ukeketaji na ndoa za mapema.

Ni shughuli ambayo amekuwa akiitekeleza kwa kuandaa michuano ya mchezo mbali mbali, ikiwa ni pamoja na soka ya wasichana na wakati mwingine kwa upande wa wavulana.

“Hapa washiriki huja asubuhi mapema, kisha wanagawanywa katika makundi kuambatana na umri wao. Kisha wanatarajiwa kushiriki katika majadiliano na wenzao chini ya usaidizi wa viongozi waliopokea mafunzo. Kwa kawaida mazungumzo haya huhusisha ushauri na unasihi. Baada ya hapo wanaenda nje kushiriki michezo ikiwa ni pamoja na soka miongoni mwa zingine,” anaeleza Omega.

Kadhalika jamii inashiriki katika shughuli hii.

“Shughuli hizi pia zinahusisha mazungumzo kuhusiana na ukeketaji na masuala husika. Hapa machifu na manaibu wao wanachangia pakubwa,” anaeleza.

Mbali na hayo, amekuwa akipaza sauti kupitia mikutano ya baraza ya kila wiki ambayo kwa kawaida huhudhuriwa na viongozi na raia katika jamii.  

Kufikia sasa wameandaa mashindano sita huku shughuli zao zikiwa tayari zimewaokoa wasichana wanne kutokana na kisu cha ngariba. “Lakini hasa nimehusika katika kushirikisha jamii katika kuhifadhi haki za watoto hasa wasichana,” aeleza.

Hili limedhihirika kupitia ongezeko la idadi ya wanawake wanaohudhuria mikutano anayoandaa ili kuzungumza nao kuhusiana masuala haya. “Nimekuwa nikitembelea vyama vya wanawake na kuzungumza nao, hasa ikizingatiwa kuwa wanawake katika eneo hili mara nyingi ndio huwa mstari wa mbele kuunga mkono ukeketaji,’ aeleza.

Pia, kazi yake imekuwa na mchango mkuu kiasi cha kubadilisha wanawake 15 ambao awali walikuwa wakitekeleza ukeketaji, ambapo badala yake sasa wameanza kupokea mafunzo ya kuendeleza jamii yao.

Haya yote amekuwa akifanya kwa usaidizi wa machifu na wazee wa vijiji, mbali na mashirika kama vile Amref.

Kadhalika kwa Bw Omega ambaye amesomea shahada ya Ustawi wa Jamii, anasema kwamba jitihada hizi zimefanikishwa na usaidizi wa wakubwa wake serikalini, kama vile Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Loitoktok.

Mfanyakazi wa umma

Bidii yake ilimfanya kutambuliwa kama mfanyakazi wa umma wa mwaka miaka miwili iliyopita katika Africa youth Awards, mbali na kupata fursa kadha za kushiriki kwenye warsha za haiba ya juu, ikiwa ni pamoja na YALI (Young African Leaders Initiative) East Africa regional fellowship. 

Ari ya kujihusisha na juhudi za kutetea msalahi ya mtoto msichana ilianza Aprili 2017 baada ya kuanza kuhudumu katika kituo chake.

“Niligundua kuwepo kwa pengo kubwa la kijinsia shuleni katika eneo langu. Idadi ya wasichana katika shule za upili na madarasa ya juu ya shule za msingi ilikuwa duni ikilinganishwa na wale katika madarasa ya chini. Nilitaka kujua wasichana hawa walikuwa wakitoweka na kwena wapi?”

Baada ya kuzungumza na watu kadha katika jamii, aligundua kuwa ukeketaji ulichangia pakubwa hali hii.

“Hii ni kwa sababu ya dhana iliyokita mizizi kwamba pindi baada ya msichana kufanyiwa ukeketaji anachukuliwa kuwa mwanamke, na hivyo ametosha kuolewa au kuanza kuwindwa na wavulana. Mara nyingi wasichana hawa walikuwa wakitungwa mimba na hivyo kulazimika kuacha shule,” anaeleza huku akiongeza kuwa hapa ndipo alipoamua kuwaadhibu waliokuwa wakitekeleza uhalifu huu.

Kwa sasa ananuia kuendeleza shughuli hizi katika maeneo mengine ambayo bado yanazidi kukumbatia utamaduni huu.