Kampuni ya kuchunguza almasi isiwahurumie waporaji

Philip Mpango

Waziri wa Fedha wa Tanzania Dkt Philip Mpango na kushoto kwake ni Spika wa Bunge Job Ndugai akifuatiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakiwa bungeni. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, July 6  2017 at  09:51

Kwa Mukhtasari

Spika wa Bunge Job Ndugai ametangaza kuunda Kamati Maalumu itakayotathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, udhibiti na umiliki wa madini ya almasi nchini.

 

SPIKA wa Bunge Job Ndugai ametangaza kuunda Kamati Maalumu itakayotathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, udhibiti na umiliki wa madini ya almasi nchini.

Lengo la Ndugai kuunda kamati hii ni ahadi yake aliyoitoa Juni 12 wakati Rais John Magufuli alipokuwa akipokea ripoti ya pili ya wanasheria na wachumi kuhusiana na makontena ya makinikia kwamba Bunge nalo litaangalia eneo la madini ya almasi.

Pia malalamiko ya wananchi na yale ya Kamati ya Madini na Nishati ya Bunge kuhusiana na madini hayo ni miongoni mwa sababu za kuundwa kwa kamati hiyo.

Inafahamika wazi kuwa mgodi mkubwa wa almasi nchini ni ule uliopo Mwadui mkoani Shinyanga uliogunduliwa na mjiolojia raia wa Canada Dk John Williamson mwaka 1940.

Kuonyesha kuwa madini ya Tanzania yana mchango na thamani kubwa katika utawala wa kifalme wa Uingereza, almasi kubwa na safi yenye rangi ya pinki na uzito wa karati (carat) 54 walipewa binti wa Mfalme Elizabeth na Mwana wa Mfalme Philip kama zawadi kwa harusi yao mwaka 1947.

Pia utajiri wa madini hayo katika eneo la Mwadui unathibitishwa na uzalishaji wa almasi kubwa wa katarati 388 uliofanyika mwaka 1990.

Ramani ya utafiti wa madini ya Oktoba 10, 2000 nayo inathibitisha uwepo wa kiasi kikubwa cha akiba ya madini hayo katika eneo hilo.

Licha ya hadidu za rejea ambazo Ndugai ametoa kwa kamati hiyo, pia tunaamini itarejea nyuma mwaka 1971 kuangalia sababu za manufaa yaliyopatikana baada ya Rais wakati huo Mwalimu Julius Nyerere kuutaifisha mgodi huo na Serikali kumiliki hisa zote.

Pia tunaamini kamati hiyo itashughulikia bila kuacha maswali, tatizo la umiliki baada ya hisa za Serikali kushuka kutoka asilimia 50 hadi asimilia 25 ikiwamo utata wa zilikokwenda fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya hisa.

Watanzania wanatarajia kupata ukweli wa sababu iliyotolewa na watendaji  wa Serikali kwamba mgodi huo ulikabidhiwa kwa mwekezaji kwa kuwa Taifa halina uwezo wa nyenzo na teknolojia sahihi za uchimbaji wa madini hayokwa faida.

Tunapenda kuishauri kamati hiyo kuangalia kwa umakini suala la misamaha ya kodi na takwimu kuhusu uzalishaji wa madini hayo kati ya Septemba 2008 na Februairi 2009.

Kamati ya Ndugai inaleta matumaini kwamba Watanzania sasa watapata majibu sahihi baada ya Serikali mwaka 2002 kutangaza ongezeko la uzalishaji wa almasi kutoka karati 76,300 hadi  354,400 kwa mwaka , lakini mwaka 2004 ikadai kukosa gawiwo kwa sababu mwekezaji hakupata faida.

Pia Watanzania wangependa kufahamu sababu za mwekezaji kuondolewa jukumu na wajibu wa kuendeleza mji wa Mwadui na jukumu hilo kukabidhiwa Serikali.

Ni wazi kuwa kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza makontena ya makinikia zimetoa mwanga wa namna gani ya kusimamia rasilimali za Taifa.

Hivyo tunaamini kamati ya Ndugai itafuata njia hiyo kwa kuchunguza kwa umakini bila kupendelea au kumwonea mtu yeyote kwa lengo la kuhakikisha kuwa keki ya Taifa inawanufaisha Watanzania wote.