Kasoro zirekebishwe wastaafu wapate mafao kwa wakati

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, June 26  2018 at  08:36

Kwa Muhtasari

Tunawashauri watendaji walioko serikalini watumie muda huu kufanyia marekebisho kasoro zilizopo ili wastaafu wa sasa wapate mafao yao bila usumbufu na wao wakistaafu wasisumbuke.

 

MOJA ya masuala ambayo huwa yanaibua mijadala mikubwa bungeni karibu kila mwaka ni kuhusu kilio cha malipo ya wastaafu.

Kila mwaka wabunge huwa wanahoji sababu za kucheleweshwa kwa mafao ya watumishi waliostaafu, na kila mwaka watendaji hutoa majibu yaleyale ya ama wahusika hawakujaza vizuri fomu za taarifa za utumishi wao au mfumo wa malipo umebadilishwa, au tuko kwenye mchakato wa kulipa ama unafanyika uhakiki kujua uhalali wa madai.

Watendaji wanaotoa majibu hayo leo wakiwa ofisini, ndio wastaafu watarajiwa na kwa kuwa mamlaka zimeshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala la malipo haya wastaafu watarajiwa ndio pia wanatarajiwa kuwa walalamikaji watarajiwa.

Mfano mzuri ni malalamiko ya wastaafu 164 wa Jeshi la Polisi ambao kwa mwaka mmoja wanahangaikia kudai mafao ya kiinua mgongo. Tangu Julai 2017, wastaafu hao wako kiguu na njia kufuatilia mafao yao.

Msemaji wa jeshi hilo amedai suala hilo linashughulikiwa na hundi za malipo zinaendelea kutolewa kwa kadri zinavyokamilika. Anayejibu kwa urahisi hivyo yuko kazini anapata mshahara kila mwezi wakati wanaohitaji mafao walikoma kufanya kazi mwaka mmoja uliopita na hivyo hawana mshahara wa kila mwezi.

Msemaji wa polisi anasema ucheleweshaji unaweza kuwa umechangiwa na mambo mengi ikiwamo kutokamilika kwa nyaraka muhimu za malipo zinazowahusu mwajiri na mwajiriwa.

Tujiulize, hivi hadi mtumishi anafikia kustaafu bado anakuwa hajui utaratibu wa kujaza fomu za mafao hadi akae nyumbani mwaka mzima? Je, ni kweli mwajiri anaweza kupokea taarifa za mtumishi fulani kustaafu asijue kasoro zilizopo kwenye fomu hadi mwaka mmoja ndipo agundue na kurekebisha?

Wastaafu hawa 164 wa Jeshi la Polisi ni sehemu tu ya watumishi wengi nchini wanaopewa lugha tamu ya kushughulikiwa haraka malipo yao, lakini hali huwa tofauti wakiondoka katika utumishi.

Tuonavyo unakosekana utashi wa kumaliza tatizo hili. Miaka nenda miaka rudi watumishi hukatwa fedha za michango, lakini hazipelekwi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ama kwa wakati au kutopelekwa kabisa. Miaka nenda miaka rudi madai ya kasoro ndio huwa kinga huku wastaafu wakizidi kuumia.

Tunasema unakosekana utashi wa kisiasa kwa sababu wabunge wakimaliza muhula wao wa miaka mitano hupewa haki yao mara moja, tena kwa mkupuo bila kuwepo kuambiwa subiri au njoo kesho.

Anayetafuta fedha za mishahara na mafao ni Serikali. Sasa kwa nini mfumo wa malipo ya stahiki za wabunge ufanye kazi, lakini iwe vigumu kwa watumishi wanaostaafu? Kwa nini iwe rahisi kuhakiki na kulipa mafao ya wabunge, lakini uhakiki wa mafao ya watumishi wanaostaafu uchukue mwaka?

Maana hata kama suala ni kuhusu madai kwamba fedha kidogo ndizo zinapatikana kwa ajili ya mafao ya wastaafu waliolitumikia Taifa kwa miaka mingi, kwa nini wabunge waliokaa miaka mitano tu wanapelekewa fedha zao zote?

Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018 hadi kufikia Aprili 2018 ni Tsh716.19 bilioni sawa na asilimia 71 pekee zilitumika kulipa michango ya mwajiri kwa watumishi wa umma. Kwa nini asilimia 29 haikupelekwa?

Tunapenda kuwakumbusha watendaji walioko serikalini kwamba miaka hupita kwa kasi na kabla hawajajijenga vizuri watajikuta wanastaafu. Hivyo tunawashauri watumie muda huu kufanyia marekebisho kasoro zilizopo ili wastaafu wa sasa wapate mafao yao bila usumbufu na wao wakistaafu wasisumbuke.