http://www.swahilihub.com/image/view/-/4331510/medRes/1901884/-/y99c6/-/minista.jpg

 

Kauli tata za viongozi wetu ni hatari

Dkt Hamisi Kigwangalla

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Dkt Hamisi Kigwangalla. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, March 7  2018 at  08:38

Kwa Muhtasari

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla alifanya ziara katika Pori la Akiba la Kimisi na Burigi mkoani Kagera ambako alikakaririwa na vyombo vya habari akiwataka walinzi kuzamisha mitumbwi ya raia wa kigeni inayoingia katika pori hilo.

 

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla alifanya ziara katika Pori la Akiba la Kimisi na Burigi mkoani Kagera ambako alikakaririwa na vyombo vya habari akiwataka walinzi kuzamisha mitumbwi ya raia wa kigeni inayoingia katika pori hilo.

Waziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia rasilimali za Taifa ili ziweze kuwa endelevu hasa kwa ajili ya vizazi vijavyo, bila shaka alitoa kauli hiyo baada ya kupewa ripoti ya watu kutoka nje kuingia kwenye pori hilo bila ruhusa au vibali rasmi.

Waziri alisema kuzamishwa kwa mitumbwi hiyo ni kutuma salamu kwa wanaoingia nchini kwamba Tanzania si shamba la bibi bali ni nchi wa watu wa nchi inayotakiwa kuheshimiwa.

Kwa mtazamo wake, mitumbwi ikizamishwa, wageni hao watarejea kwao kwa kuogelea. Je, alijiuliza nini kitatokea ikiwa wakizama?

Kwanza tunatambua juhudi za waziri katika ufuatiliaji, maana katika kipidi kifupi ameweza kutembelea maeneo mengi ya hifadhi za wanyama na mapori ya akiba na kutoa matamko makali.

Pili, tunaelewa nia thabiti ya waziri kutaka kutuma ujumbe kwamba maliasili lazima zilindwe kwani ni urithi  wa Taifa na kwamba ikiwa Watanzania watazuiwa kukata miti kiholela au bila vibali kwa nini iwe hatari kwa wageni.

Pia, tunaelewa kwamba alitaka kutuma ujumbe kwamba Serikali haitaki tena mchezo wala mzaha katika kusimamia rasilimali zake. Hapa lazima kama ilivyo kwa Watanzania, majirani wa Tanzania waelewe kwamba ardhi kubwa na nzuri yenye rutuba, miti mirefu na migumu kwa mbao na wanyama waliojaa kwenye hifadhi ni rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu.

Kama ambavyo Watanzania hawaendi kuvuna  kiholela rasilimali walizopewa wao na Mwenyezi Mungu kama miti, madini na mali nyingine ndivyo na wao wanapaswa kuambiwa  na kuonywa wasithubutu kusaka utajiri kupitia rasilimali zetu kwa njia zisizofaa.

Hata hivyo, suala hili lazima lizingatie masuala ya kidiplomasia ili kuepusha uhasama na majirani hao ambao wapo na wataendelea kuwapo.

Hivyo upande wa pili tunachelea kusema kauli ya waziri imevuka mpaka na ni hatari maana madhara ni makubwa ya kuwahimiza wananchi wachukue sheria mkononi ya kuzamisha mitumbwi kwa matarajio kuwa ikizama, wenye mitumbwi hiyo hawatazama, bado watakuwa hai na hivyo wataogelea kuelekea kwao.

Je, mitumbwi ya wageni ikizamishwa sijui kwa njia ipi waziri anatarajia viongozi wa nchi anakotoka watafurahi? Tujuavyo, wageni wanaoingia nchini kwa mitumbwi ni sehemu ya wimbi kubwa la wahamiaji haramu ambao mara kwa mara vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi huwa linatutangazia kuwakamata na kwashtaki na hatimaye kuwarejesha makwao. Wajibu wa vyombo wa ulinzi na usalama ni kushughulikia vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria  kwa kuwadhibiti wahusika wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo va sheria ili wachukuliwe hatua zinaziofaa badala ya kutoa matamko ya namna hiyo ambayo yanaweza pia kuwaweka hatarini watu wetu wanaotumia usafiri  wa majini.

Tunatoa wito kwamba sheria ziheshimiwe na utaratibu wa kumkamata mhalifu awaye yote  uzingatiwe ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria  na ahukumiwe  kulingana na kosa  na wala uhai usipotezwe kwa kisingizio cha ugeni.