http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

Kauli ya JMP Mwanza ituongoze sote nchini

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, November 2  2017 at  10:55

Kwa Muhtasari

Rais John Pombe Magufuli alikuwa Mwanza kwa ziara ya kikazi mapema wiki hii na huko aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo baada ya kufikishana polisi.

 

RAIS John Pombe Magufuli alikuwa Mwanza kwa ziara ya kikazi mapema wiki hii na huko aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo baada ya kufikishana polisi.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo alipokuwa akijibu bango la wakazi wa Kata ya Mahina lililokuwa likimtaarifu tukio la diwani wao ambaye pia ndiye meya wa Jiji la Mwanza kuzuiwa kushiriki ziara yake kwa kukamatwa na kuwekwa mahabusu.

Wakazi hao walionyesha bango baada ya kuwapo kwa mgogoro wa muda mrefu kati ya meya huyo James Bwire na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba.

Tangu mwanzoni mwa mwaka jana Bwire na Kibamba wamekuwa katika mvutano.

Wakati  Bwire akiituhumu Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kwa ubadhirifu, Mkurugenzi naye anamtuhumu kiongozi huyo kuwa anatumia nafasi yake kuingilia utendaji kinyume na sheria na taratibu.

Tunaamini maelewano baina yao ni kwa manufaa ya wananchi kuliko kuendeleza mivutano isiyo na faida kwa Taifa.

Tunapongeza kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka viongozi wa mkoa  huo kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo. Kwa kufanya hivyo tunaamini kuwa maelewano baina yao ni kwa manufaa ya wananchi  kulio kuendeleza mivutano  isiyo na faida kwa Taifa.

Meya ni kiongozi anayetokana na wananchi baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa kidemokrasia ulioshirikisha vyama vya siasa wakati mkurugenzi ni kiongozi aliyetokana na uteuzi wa mamlaka za juu serikalini.

Hivyo viongozi hawa kuendelea kutunishiana misuli kunadhoofisha mgogoro kama huo  au unaofanana na huo kunadhoofisha  maendeleo ya wananchi na kuichafua Serikali.

Tunaamini kilichofanywa Mwanza na Rais Magufuli ni mwendelezo wa  dhamira yake ya kuwatumikia Watanzania kwa haki.

Hivyo viongozi wa maeneo mengine yenye migogoro kama huo au unafanana na huo ni vyema wakachukua  agizo la Mwanza kama mfano wa kutatua matatizo yao.

Kuna baadhi ya viongozi wa mikoa wamejiingiza Kwenye mivutano isiyokuwa na tija na viongozi wa kisiasa na Jeshi la Polisi ndilo limekuwa  fimbo ya wenye mamlaka kupambana na wanasiasa.

Tunaamini kama alivyosema Rais Magufuli kwamba njia sahihi ya kumaliza migogoro ni kwa mazungumzo.

Tunajua kwa mujibu wa mamlaka waliyo, wakurugenzi  wana haki ya kulitumia Jeshi la Polisi lakini matumizi hayo yasiwe ni ya kupambana na wengine  au kuwanyanyasa wasiokuwa  kwenye mamlaka.

Viongozi wa mikoa na wa wilaya watambue kuwa umefika wakati  wa kutumia zaidi njia ya mazungumzo  katika kutatua mikwamo sio tu kwa viongozi wa kisiasa  kutoka chama tawala, bali pia viongozi wa kisiasa wa kuchaguliwa na wananchi kutoka vyama vya upinzani.

Tumekuwa tukiona  nguvu kubwa ikitumika  kwa mameya au wabunge kutoka vyama vya upinzani  kila panapotokea kutokuelewana katika uendeshaji wa mamlaka.  Hii si sawa.

Rais ametoa ushauri huo wa jinsi ya kushughulikia matatizo katika uendeshaji wa shughull za umma  badala ya kutumia nguvu za dola kwa kukamatana na kuwekana mahabusu jambo ambalo  linajenga chuki  badala ya kujenga Taifa kwa kuwatumikia wananchi.

Tunaamini matumizi ya polisi ambayo Rais  ameona si suluhu ya haraka bali ni vyema yakaepukwa ili kujenga Taifa lenye kujadili migogoro yake kwa hoja na mwisho kurudi kuwa kitu kimoja katika kuwatumikia wananchi.

Kama tunajenga nyumba moja, tusigombanie fito.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647