http://www.swahilihub.com/image/view/-/3501664/medRes/1523655/-/nj0ywqz/-/ewafuka.jpg

 

Kazi IEBC si mchezo, aghalabu historia imeonyesha

Wanyonyi Wafula Chebukati

Wanyonyi Wafula Chebukati alipohojiwa kwa kazi ya mwenyekiti wa IEBC awali. Picha/MAKTABA 

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  11:04

Kwa Muhtasari

Sasa wengi wanafananisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na pia Afisa Mkuu Mtendaji sawa na kurushwa katikati ya tanuri la moto.

 

WENGI wanafananisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na pia Afisa Mkuu Mtendaji sawa na kurushwa katikati ya tanuri la moto.

Na visa vya hapo awali ambapo maafisa hao wakuu wanafurushwa afisini kiholela ni dhihirisho wazi la jinsi nyadhifa hizo zimegeuka kiazi moto.

Matukio ya wiki iliyopita katika tume hiyo yaashiria uwezekano wa maafisa wa sasa kukaangwa sawa na watangulizi wao.

Na hali hii imeibua shaka iwapo maafisa waliopo watadumu hadi 2022 Uchaguzi Mkuu unapopangiwa kufanyika ikizingatiwa kuwa, kisheria, makamishna hupaswa kuhudumu kwa miaka sita.

Endapo mzozo uliopo katika tume hiyo utachangia maafisa wakuu kubadilishwa, uchaguzi wa 2022 utakuwa wa tatu mfululizo kusimamiwa na kikundi kipya na Kenya itakuwa ikiendeleza mtindo wa kuondoa maafisa wa uchaguzi mamlakani kabla kipindi chao cha kuhudumu kikamilike.

Makamishna, wakiongozwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati, walimwagiza kwa mara ya pili Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Ezra Chiloba, kwenda kwa likizo ya lazima.

Mwaka 2017, hatua hiyo ilitokana na madai ya Muungano wa NASA kwamba Bw Chiloba alikuwa na ushirikiano wa karibu na Chama cha Jubilee.

Mwaka 2018 Bw Chebukati alisema uamuzi huo ulifanywa ili kuwezesha uchunguzi kuhusu uagizaji wa vifaa vilivyotumiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017.

“Ni muhimu ieleweke kuwa, kwa kuamua kufanya uchunguzi wa kina, tume inatekeleza jukumu lake la kulinda rasilimali za umma,” akasema Bw Chebukati, ishara kuwa uchunguzi huo unahusisha zabuni za mabilioni ya pesa kwa kampuni mbalimbali wakati wa uchaguzi mwaka uliopita.

Uchaguzi wa 2007 ulifungua lango la mabadiliko kwa usimamizi wa uchaguzi nchini baada ya ghasia za uchaguzi zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 na kuwaacha maelfu wengine bila makao.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), marehemu Samuel Kivuitu, alimtangaza Mwai Kibaki wa Chama cha PNU mshindi wa urais dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Bw Raila Odinga wa ODM.

Baadaye, Bw Kivuitu alikiri ilikuwa vigumu kubaini mshindi kwenye uchaguzi huo uliojaa dosari.

Tume nzima ya Bw Kivuitu ilivunjwa na wabunge kupitia Mswada wa Marekebisho ya Katiba (2008) wakaunda Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC).

Ndoto

Wakati huo, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, ambaye alikuwa Mbunge wa Ugenya, alisema: “Kwa kupitisha mswada huu, Kenya inaanza safari mpya ili iinuke kutoka kwa jivu na kuwa nchi yenye demokrasia halisi.”

Miaka kumi baadaye, azimio hilo la Bw Orengo bado ni ndoto ambayo inapiganiwa na wanachama wa upinzani.Bw Issack Hassan, ambaye alikuwa mwenyekiti wa IIEC baadaye alichaguliwa mwenyekiti wa kwanza wa IEBC baada ya katiba mpya kupitishwa 2010. Alifurushwa kutoka afisi hiyo mnamo 2016 pamoja na makamishna wake.

Kikosi cha Bw Hassan kiliandamwa na madai ya ufisadi katika utoaji wa kandarasi za uchaguzi wa 2013 almaarufu 'Chickengate’, ambapo Bw James Oswago, aliyekuwa afisa mkuu mtendaji katika kipindi hicho, alishtakiwa kwa madai ya kushiriki kwenye upunjaji huo.

Bw Oswago alikuwa amesimamishwa kazi kwa muda hadi wakati kandarasi yake na IEBC ilipokamilika, ndipo Bw Ezra Chiloba akachaguliwa Januari 2015. Bw Hassan na makamishna wenzake walisalia mamlakani hadi viongozi wa upinzani waliposhinikiza kuondolewa kwao kupitia kwa maandamano kabla uchaguzi wa 2017, ndipo wakalazimika kujiuzulu Oktoba 2016.

Bw Chebukati na makamishna sita wapya waliingia mamlakani baadaye Januari 2017, wakiwa na changamoto ya kuandaa uchaguzi mkuu katika muda mfupi.

Muungano wa Nasa ungefanikiwa kung’oa kikosi cha Bw Chebukati na Chiloba kabla uchaguzi wa marudio wa urais Oktoba 26, mwaka uliopita, Kenya ingeweka historia ya kuandaa kila uchaguzi wa urais chini ya tume mpya tangu 2007.

Kulingana na Mratibu wa Shirikisho la Mashirika ya Kijamii, Bw Suba Churchill, imani ya wananchi kwa IEBC inaweza kurejeshwa tu ikiwa Bw Chiloba atajiuzulu.

“Yamkini kuna watu wenye ushawishi mkubwa wanaoshirikiana na baadhi ya makamishna wa IEBC kulinda maafisa ambao wanafaa kuwajibikia uhalifu unaotendwa katika tume hiyo. Kuna watu wenye matamanio ya kibinafsi kuhusu uchaguzi wa 2022 ambao wameshika IEBC mateka,” akasema Churchill.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya usimamizi wa uchaguzi wameonya kubadilisha wasimamizi ghafla kila mara katika kila uchaguzi huchangia udhaifu katika usimamizi wa uchaguzi nchini.

Kwenye ripoti ya uangalizi wa uchaguzi mkuu uliopita, Muungano wa Ulaya (EU) ulipendekeza kuwa kama ni lazima maadiliko yafanywe, ni vyema yawe yakifanywa mapema ili viongozi wapya wa tume wapate muda wa kutosha kuandaa uchaguzi.