http://www.swahilihub.com/image/view/-/4883718/medRes/2190424/-/aiqn4k/-/kilkoa.jpg

 

Vijana wa kiume wanaojishughulisha na kazi zinazochukuliwa za jinsia ya kike

James Njure Wanjiru

Bw James Njure Wanjiru akionesha vinavyoshonwa vitambaa vya viti kwa nyuzi. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  12:05

Kwa Muhtasari

  • Kisingizio kisiwe ni kwamba nafasi za ajira ni finyu
  • Iwapo Mungu amekujalia kipaji, basi kitumie

 

SUALA la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana limekuwa ni wimbo nchini Kenya.

Serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto ilipochukua hatamu ya uongozi 2013, iliahidi nafasi za kazi zipatazo milioni moja kwa mwaka kwa vijana.

Hata hivyo, ahadi hii haijaafikiwa kikamilifu kwa mujibu wa maelezo ya viongozi hawa wakati wakifanya kampeni kurai wananchi kuwachagua.

Baada ya uchaguzi tata wa mwaka uliopita, 2017, Rais Kenyatta kwenye ajenda kuu nne alizozindua, mojawapo ni ujenzi wa viwanda na alisema itasaidia kubuni nafasi za kazi kwa vijana. Serikali ingali inaonekana kuteua wanasiasa wakongwe kujiunga na taasisi mbalimbali za kiserikali.

Maelfu ya vijana kila mwaka hufuzu kwa vyeti vya aina tofauti vya masamo kutoka taasisi za juu za elimu. Hii ina maana kuwa idadi ya vijana wanaosaka kazi inaendelea kuongezeka, nafasi zikiwa finyu. Baadhi yao haswa ambao wazazi wao wana uwezo kimapato, wanawekeza katika sekta ya kilimo, biashara ndogondogo na za wastani (SMEs) maarufu kama Juakali.

Wasio na uwezo wanalazimika kufanya kazi za kijungu jiko. Hayo yakijiri, kuna vijana wanaotumia talanta zao kujiajiri ili kuzimbua riziki. Awali, baadhi ya kazi zilichukuliwa kuwa za jinsia fulani. Mfano, ufumaji wa vitambaa vya viti na makochi na ususi wa nywele uliaminika kama jukumu la wanawake. Kadhalika, kazi za uhandisi zilichukuliwa ni za jinsia ya kiume pekee.

Dhana hiyo sasa imeonekana kupitwa na wakati, kwani vijana wengi wametambua kwamba hakuna kazi inayoelekezewa jinsia moja pekee. James Njure Wanjiru ni mshonaji wa vitambaa vya viti kwa nyuzi Nairobi na Molo, na anasema alipoanza kazi hii alipoteza marafiki wengi kwa sababu ya kufanya kazi iliyohusisha wanawake.

"Ufumaji wa vitambaa uliaminika ni kazi ya kike pekee, mimi niliuchukulia kama kazi yoyote ile. Vijana walionitoroka kwa sasa wananiomba niwafunze kuifanye," anaelezea kijana Njure.

Ushonaji wa vitambaa kwa nyuzi unahitaji ubunifu wa aina yake, na kulingana na Bw Njure ni kwamba anajivunia ufanisi aliopiga kimaisha na kimapato kuupitia.

Sifa

Ni kazi ambayo inahitaji mapenzi ya dhati na kijana huyu anadokeza kwamba hutoa mafunzo kwa wanaume na wanawake, wengine wakitumia maarifa waliyopokea kujiajiri. Njure alianza kazi hii kwa mtaji wa Sh500 pekee na kwa sasa inamvunia maelfu ya pesa pamoja na kwamba imemzolea sifa chekwachekwa.

Samuel Karanja, maarufu kama Sam De Salonist ni msusi wa wanawake. Barobaro alikuwa mchuuzi wa njugu jijini Nairobi, lakini anasema alikuwa na mapenzi ya kurembesha wanawake kwa kuwasuka na kuwapaka hina na wanja. Ilimgharimu mtaji wa Sh100 kuanza ususi tamba 'Mobile Salonist' mwaka 2016, na alikuwa akizuru wateja wake walipo ili kuwapa huduma za ususi.

"Wazazi walitaka nifanye umekanika, japo mapenzi yangu yalikuwa katika ususi. Watu walinipiga vita baridi vya maneno kuwa ususi ni kazi ya jinsia ya kike, langu lilikuwa kuwapa maskio tu na kusahau waliyonieleza," anasimulia Sam.

Juhudi za kijana huyu zimemuwezesha kuzindua maduka mawili ya ususi, saluni, eneo la Zimmerman, kaunti ya Nairobi.

Karanja anasihi vijana wenzake kutodhalilisha kazi za aina hii akisema zina mapato tele, akitoa mfano wa ususi wake kuwa wanawake hupiga foleni kwake wakisubiri awahudumie.

Aidha, amebuni nafasi ya kazi kwa zaidi ya vijana 20.

Serikali inahimiza vijana kujiunga na taasisi za kiufundi, ili kufanya mafunzo ya kazi za mikono kama ususi. Mbali na Bw Karanja, taifa limeshuhudia vijana wengine wakifuzu kwa taaluma za mikono, kama umekanika ambao kwa sasa unafanywa na jinsia ya kike.

Itakumbukwa kwamba kazi za mikono zinaorodheshwa katika Juakali. Sekta hii imebuni nafasi za kazi kwa zaidi ya asilimia 70 ya Wakenya.