http://www.swahilihub.com/image/view/-/4303858/medRes/1884352/-/14updsxz/-/ss.jpg

 

Kuandika na kuchora kwa mavazi ni kazi yenye malipo maridhawa

Samuel Kariuki

Bw Samuel Kariuki, hufanya kazi ya sanaa kutia nembo na majina kwenye mavazi mtaani Maji Mazuri, Kasarani kaunti ya Nairobi Februari 12, 2018. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, February 14  2018 at  06:48

Kwa Mukhtasari

Ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ni donda ndugu katika taifa hili. Wengi wamelaza vyeti vyao vya stashahada, shahada, shahada ya uzamili na hata ile ya uzamifu 'masandukuni', kwa sababu ya ukosefu wa kazi.

 

UKOSEFU wa ajira hasa kwa vijana ni donda ndugu katika taifa hili. Wengi wamelaza vyeti vyao vya stashahada, shahada, shahada ya uzamili na hata ile ya uzamifu 'masandukuni', kwa sababu ya ukosefu wa kazi.

Wachache ndio wameweza kupata nafasi finyu za kazi serikalini na kwenye kampuni mbalimbali, na tuseme hiyo ni bahati yao, ikitiwa muhuri na kauli-bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi. Hivyo, basi wachache hao wanafaa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ndiye wa kuneemisha.

Kwa wanaofuzu vyuoni, kuna baadhi yao waliojaaliwa vipaji mbalimbali na endapo watavitumia ipasavyo, hatimaye huwa miongoni mwa mabosi wanaobuni nafasi za kazi.

Historia ya Kenya ya wabunifu wa ajira ikinakiliwa, jina la Bw Samuel Kariuki halitakosa kujumuishwa. Mwaka wa 2011, alifuzu kwa shahada ya uchoraji (Art & Graphics Design) katika chuo kikuu cha Multi-Media jijini Nairobi.

Kijana huyo hakulaza damu.

"Kupata ajira nchini imekuwa balaa, nilifahamu hayo na azma yangu tangu nijiunge na chuo kikuu ilikuwa kujiajiri na nibuni nafasi za kazi kwa vijana wenzangu," aeleza.

Mtaani Maji Mazuri, Kasarani kaunti ya Nairobi ndipo karakana yake ya kutia mavazi nembo, hasa tishati ilipo. Kariuki alianzisha kazi hiyo kwa mtaji wa Sh1, 000 mwaka wa 2012, ambayo kwa sasa inamuingizia maelfu ya pesa.

La kutia moyo ni kwamba ameajiri vijana watatu. "Kwa kuwa nilinolewa ujuzi na maarifa ya taaluma niliyosomea, kwa nini nisingeyatumia kubuni ajira?" auliza.

Mashine ya kutia nembo na maandishi kwenye mavazi ni ya kujiundia kwa mbao, ikisaidiwa na tarakalishi na printa. Kando na zana hizo za kazi, huhitaji rangi za aina mbalimbali mavazi yakiwa ni ya mteja.

Bw Kariuki anaeleza alipoonja kazi hiyo 2013, hajatamani kurudi nyuma kwa kufikiria kutafuta ajira nyingine. "Utamu wa kazi ni pesa, wengi niliofuzu nao chuoni wangali wanasaka kazi. Mimi nilishapata kazi kwa kutumia masomo niliyopokea," aeleza barobaro, ambaye ni mume na baba wa mtoto mmoja.

Anasema kuwa uchaguzi mkuu wa 2013 ulimpiga jeki, akaweza kupanua kazi yake kiasi kwamba ameweza kufungua kikundi cha vijana kinachofahamika kama 'Msingi Imara Self Help Group', chenye madhumuni ya kuimarisha vijana.

"Nilipokea oda mbalimbali za mavazi ya wanasiasa ya kufanya kampeni," afichua.

Hali kadhalika, anaeleza kuwa mwaka wa 2017 kazi iliendelea kunoga na kushika kasi kwa sababu ulikuwa mwaka wa uchaguzi mkuu Kenya.

Kwa siku Bw Kariuki hupokea oda ya kutia nembo na maandishi kwenye mavazi, isiyopungua mavazi sita. Ada ya vazi moja huwa zaidi ya Sh250, japo anaeleza bei hutegemea anavyotaka mteja.

"Bei ya chini kwa vazi moja ni Sh250," asema.

Mbali na wanasiasa, Bw Kariuki hupokea oda kutoka kwa shule na vyuo mbalimbali Nairobi na Kiambu, makanisa, kampuni na wanamuziki, miongoni mwa wateja wengine.

Vilevile, huchora vibango, michoro kwenye magari na kazi zingine za sanaa zinazohitaji uchoraji.

Kijana huyo pia amefungua kituo cha kuosha magari.