Kigoda cha Mwalimu kiwe chachu ya maendeleo

Mwalimu Julius Nyerere

Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Picha/MAKTABA  

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, June 15   2017 at  10:37

Kwa Mukhtasari

Kongamano la tisa la Mwalimu Nyerere lililoanza juzi kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linamalizika leo na mada kuu ni “Nafasi ya wanasiasa katika kuinuka na kuanguka kwa maendeleo ya bara la Afrika,”

 

KONGAMANO la tisa la Mwalimu Nyerere lililoanza juzi kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linamalizika leo na mada kuu ni “Nafasi ya wanasiasa katika kuinuka na kuanguka kwa maendeleo ya bara la Afrika,”

Wakati akichangia mada katika siku ya kwanza ya kongamano hili, mwanakigoda wa mwaka huu Profesa Abdoulaye Bathily wa Senegal alisema bila kupepesa macho kuwa Afrika imekosa viongozi wenye mtazamo chanya kwa ajili ya maendeleo ya bara hili.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo kama Profesa Bathily alivyosema zimepata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini hadi sasa ni maskini licha ya kuwa na maliasili nyingi za madini

Katika maelezo yake, mwanasiasa huyo aliwalaumu zaidi viongozi waliopokewa vijiti kutoka kwa waasisi ambao walijitoa kwa hali na mali kupigania uhuru wa nchi zao.

Tunakubaliana na Profesa Bathily kwamba wabia kutoka nje hawawezi kuwaletea maendeleo Waafrika ndiyo maana Afrika inaendelea kuwa  bara la kuzalisha malighafi na soko la bidhaa zinazozalishwa kwingine.

Kwa Tanzania, tatizo mojawapo ni kutokamilika kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambayo ni mwongozo wa viongozi wetu katika masuala ya uchumi, kisiasa na kijamii ili yaendane na dunia ya sasa.

Wanasiasa wa Tanzania hasa wapinzani wamekuwa na malalamiko mengi kama ya Rais kupewa mamlaka makubwa na Katiba kama ilivyo kwa mawaziri katika kusaini mikataba ambayo hivi saa inapigiwa kelele.

Pia kumekuwa na malalamiko ya madaraka makubwa  ya wakuu wa mikoa na wilaya kiasi cha mambo mengi katika maeneo yao ya  kiutawala kupelekwa kisiasa zaidi.

Tunadhani mada kuu kwenye Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere inapaswa kuepusha hayo na mengine mengi yanayoisumbua nchi yetu.

Katiba Mpya

Taifa linahitaji Katiba Mpya itakayotoa mwongozo chanya kwa viongozi wetu na hata kuwabana wale wenye tamaa.

Kinachofanywa na Rais Magufuli ni juhudi binafsi lakini kama kugekuwa na Katiba imara inayodhibiti na kuwawajibisha  viongozi, nchi isingekuwa hapa ilipo na hivyo Rais Magufuli asingekuwa na kazi ngumu kama ilivyo sasa.

Tunaamini kwamba kuwa na Katiba imara, wasaidizi wa Rais wangewajibika kwa wananchi kwa kuwa wangepitia mchujo unaofanywa na Bunge kwa uwazi na hivyo mfumo kuwalazimisha kufanya kazi kwa maadili na weledi.

Hivyo kongamano kama hilo la Kigoda cha Mwalimu Nyerere  halitakiwi kuwa jukwaa la kisiasa la watu kueleza fikra zao na kuondoka bali  kuchukuliwa kwa uzito na wahusika kuyafanyia kazi.

Tunawapongeza waandaaji wa Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere kwa kufanya jitihada za kuendeleza fikra za muasisi huyo wa Taifa la Tanzania kwa kuandaa mijadala ambayo inawapa nafasi wale waliopewa dhamana ya kuongoza nchi kutathmini mwenendo wa utendaji kazi  wao na kulingaisha na falsafa hizo.