http://www.swahilihub.com/image/view/-/3054850/medRes/1241423/-/69nywi/-/091341-01-02%25282%2529.jpg

 

Uchambuzi: Kila mtu aheshimu kazi ya mwenzake

Wanahabari wa kimataifa

Wanahabari wa kimataifa wakifuatilia tukio moja barani Afrika mnamo 2015. Picha/AFP 

Na EMMANUEL MTENGWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  11:24

Kwa Muhtasari

Usiwe mchonganishi, mfitini na mtu wa kusumbua wengine.

 

KAZI ni shughuli anayoifanya mtu ili kujipatia kipato. Kila mtu anapofanya kazi anatarajia kupiga hatua katika maisha.

Kila kazi ina faida na changamoto zake; majukumu ya kazi yanavyotofautiana ndivyo na masilahi yanavyotofautiana, lakini kila kazi ina umuhimu kwa mhusika.

Kuna usemi unaosema ndege mmoja mkononi ana thamani kuliko wawili walio porini. Usemi huo unamaanisha kuwa kile kidogo ulichonacho kina thamani kuliko kikubwa ambacho haukimiliki.

Kila mtu anapopata kazi iwe ajira ya kudumu au kibarua, ni dhahiri anakuwa na mategemeo baada ya kipindi fulani, akitamani kujikwamua kiuchumi.

Kimsingi, kila mtu anajivunia kwa kile anachofanya, pamoja na kwamba si wote wanaofanya kile walichotamani kwenye ndoto zao.

Pengine niwapongeze wale ambao hawachagui kazi kwani wanafanya jitihada nyingi hasa za kujikwamua kiuchumi, lakini pia nawapa pole wale ambao hawakati tamaa licha ya changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao. Ninaamini kuwa katika jamii mtu yeyote aliyepata kazi hajisikii furaha pale anapoona wengine wanadharau kazi anayoifanya.

Mathalan, kuna hawa wahudumu wa kike katika migahawa na maeneo mengine ya starehe. Ni watu wanaokutana na changamoto ya kudharauliwa katika kutimiza majukumu yao.

Ni watu ambao jamii inawachukulia katika taswira hasi, hali inayosababisha hata wale wanaopewa huduma kujijengea mazoea ya kuwadharau.

Wateja wanaohudhuria maeneo hayo ni watu wa silika mbalimbali. Wanapofika maeneo haya hukaa na kuulizwa huduma wanayotaka, kisha huagiza kile wanachohitaji kwa wahudumu.

Ninachotaka kusema ni hii tabia ya wateja wanaojifanya kuwa na mamlaka kwa wahudumu utadhani wao ndio mameneja wao.

Kwa mfano, mhudumu anapokosea kuleta kitu tofauti na kile alichoagizwa. Wapo wateja wengi hawana uvumilivu wa kumwelekeza mhudumu lakini mbaya zaidi ni kuwa kinachofuatia ni kumtukana matusi ambayo wakati mwingine hayana uhusiano na kosa alilofanya.

 

Utadhani hawafanyi kosa

Kosa dogo linaibua maneno yasiyo na tija na wakati mwingine wanatoa lugha za kuudhi dhidi ya wahudumu utadhani wao hawafanyi makosa.

Kibaya zaidi ni pale mhudumu anapokosea kidogo baadhi ya wateja wanavyomshambulia utadhani si binadamu. Hummiminia maneno ya ajabu na matusi yasiyo ya lazima. Ninaamini kuwa hakuna mtu mkamilifu, iwe katika ngazi ya familia, jumuiya au hata ofisini.

Ninajiuliza wateja wanapata wapi mamlaka ya kuwahukumu wahudumu? Pengine tabia hiyohiyo inachochewa na taswira iliyojijenga kwenye jamii dhidi ya wahudumu hao.

Ni kweli kwamba mteja ana haki ya kupata huduma bora, lakini siamini kuwa pale anayekuhudumia anapokosea suluhisho ni kumpa matusi na maneno ya kumdhihaki.

Ninachojaribu kukionyesha ni kuwakumbusha tu wale wateja wenye dharau na wanaowatukana wahudumu, mtambue kuwa wahudumu hao wako kazini kama nanyi mnavyokuwa ofisini.

Nimewagusia wahudumu wa maeneo haya kwa kuwa ndio waathirika wakubwa. Inawezekana wanakaa kimya kwa muda mrefu wakiugulia matusi na dharau wanazokumbana nazo katika majukumu.

Pengine kukaa kimya kwao kunatokana na kuwa na uelewa mdogo wa sheria zinazowalinda. Japokuwa wanao mabosi wanaowasimamia, lakini wanashindwa kuripoti kwao juu ya matusi hayo kutokana na mazoea waliyojijenga.

Katika uchambuzi huu, wahudumu hawa wamesimama tu kama wawakilishi wa kada nyingine ambazo hukumbana na kadhia ya kudharauliwa kwenye kazi kama makondakta wa daladala na watoa huduma wengine.

Naamini kuwa hakuna sababu ya kumtukana mhudumu pale anapokosea kwa kuwa matusi hayana tija.

Pamoja na kwamba mteja umekwenda na fedha zako mahala fulani kupata huduma, lakini hiyo haihalalishi kuwa una mamlaka ya kuwaadhibu wanaokuhudumia pale wanapokosea.

Kuwa na kazi nzuri hakufanyi iwe sababu ya kuwadharau wanaokuhudumia. Ninaamini kuwa kila kazi ina thamani. Ndio maana nimewiwa kukemea kudharauliana kutokana na tofauti ya vipato au kazi. Naamini kuwa utu ni muhimu kuliko kazi na vyeo ambavyo mara nyingi ndivyo vinavyowapa wengi majivuno. Ni vyema kuwa na mtazamo chanya juu ya wengine katika jamii. Hili litaepusha kudharauliana. Kila kazi ina hadhi yake. Wito wangu, tuheshimiane kwa kazi tunazofanya.

 

Emmanuel Mtengwa ni mwandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa simu namba +255753590823