http://www.swahilihub.com/image/view/-/4215098/medRes/1827949/-/7fg7ag/-/madia.jpg

 

Kilimo cha dania ni rahisi, mapato yake yana faida tele

Dania

Sehemu ya shamba la Bi Leah Wanjiru Ndung'u, Lari Uplands kaunti ya Kiambu lenye dania zilizomaliza muda takriban mwezi mmoja tangu zipandwe. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, December 5  2017 at  10:45

Kwa Mukhtasari

Je; unafahamu kwamba dania ni miongoni mwa mimea rahisi na isiyohitaji ujitutumue zaidi kwa kazi ya sulubu kukuza?

 

DANIA ni aina ya mmea unaotumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, kando na kuwa na harufu ya kuvutia. Je; unafahamu kwamba dania ni miongoni mwa mimea rahisi na isiyohitaji ujitutumue zaidi kwa kazi ya sulubu kukuza?

La muhimu kwa dania ni maandalizi murwa ya shamba linalokuziwa, utunzaji bora, maji kwa wingi endapo si msimu wa mvua.

Kinachofuata baada ya kuzingatia hayo ni kupokea mazao yake, huku soko lake likiwa la kupigiwa chapuo kwa kuwa dania haikosi wateja. Mmea huo hauna wakulima wengi wanaoufanya, hivyo basi soko lake linasalia imara kila wakati.

Wakulima ambao wamekumbatia zaraa ya dania, wakati wa mavuno hutabasamu kwa sababu ya donge nono wanazopokea.

Matayarisho na upanzi

Shamba ambalo mkulima anapania kukuza dania, linafaa liwe limechimbwa vyema. Aidha urefu kuenda chini unafaa uwe kati ya sentimita 8-10. Mchanga uandaliwe uwe mwororo kwa kuwa dania haina mizizi mirefu. Bi Leah Wanjiru Ndung'u ni mkulima wa dania kata ya Lari Uplands kaunti ya Kiambu, na anaeleza taratibu za kukuza mmea huo.

Kulingana na mkulima huyo ni kwamba mchanga unafaa uinuliwe kiasi kwamba utakuwa juu kuliko mazingira ya kipande kinachopandwa.

Mbolea imwagwe kwa wingi, na kuandaa mitaro yenye urefu wa sentimita tano hivi kuenda chini na sentimita kumi na tano kutoka mtaro mmoja hadi mwingine.

"Mimi hutumia mbolea ya mbuzi ama kondoo, kwa kuwa ni mwororo. Mbegu humwagwa kwenye mitaro hiyo kwa kipimo, mchanga chache tu utumiwe kuzifunika," ashauri Bi Wanjiru, akiongeza kuwa maji yanyunyiziwe kwa wingi.

Magonjwa na wadudu

Katika kila kilimo chochote kile hakikosi changamoto zake, magonjwa na wadudu pia huathiri dania. Siku tisa baada ya upanzi, mkulima anashauriwa kupulizia dawa ya kuua makwekwe. Bi Wanjiru hutumia dawa aina ya 'Linagan'.

Dania huchipuka ardhini kati ya siku 10-14, na kwamba baada ya siku 20 inafaa kupuliziwa dawa ya kukabiliana na ugonjwa wa baridi unaofahamika kama 'Ukungu'. Ugonjwa huo huwa na dalili sawia na za 'Blight', ambapo baridi huwa kali majira ya asubuhi na jioni.

"Uplands ni sehemu yenye baridi sana, mimea mingi huku huathiriwa na ugonjwa wa baridi. Mimi hutumia dawa aina ya 'Score', ambapo huipulizia mara tatu, yaani baada ya kila siku 14 mtawalia," aeleza.

Mbolea ya folia ya maji hufanya dania kukua upesi, kando na kunawiri na kustawi vyema, Bi Wanjiru huinyunyizia mbolea hiyo kati ya siku 30-40.

Hata hivyo, anasema changamoto za wadudu kwa dania ni finyu mno. Viwavi (Cutworms) ndio wadudu wanaoshuhudiwa.

"Viwavi huwaangamiza kwa dawa kadha wa kadha kama vile; Alpha, Tata ama Karate. Ingawa mkulima anafaa kuomba ushauri kutoka kwa mtaalamu wa kilimo anapoona dalili za mimea yake kuathirika," aeleza mkulima huyo.

Dania huwa tayari kuvunwa baada ya siku 45 hadi 50. Bi Wanjiru hufanya kilimo cha dania kwenye ekari moja. Aidha ameigawanya kwa vipande kadha vya thumni ekari (1/8).

Ameviandaa kiasi kwamba kila baada ya siku 14 huvuna dania na kupata mapato tele. Kulingana naye ni kwamba kipande kimoja humpa zaidi ya Sh25,000, hii ikidhihirisha kwa mwezi Bi Wanjiru hutia kibindoni kima cha Sh50,000.

Dania pia hutumiwa kama kiungo kwenye kachumbari.

Mmea huo una madini aina ya Vitamini C yenye nguvu za kupambana na magonjwa.