http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885232/medRes/2191282/-/jl6iru/-/onchuru.jpg

 

Matikitimaji: Kilimo chake na faida zake kiafya

Zachariah Onchuru

Bw Zachariah Onchuru, akionesha na kueleza jinsi ambavyo matikitimaji yanavyokuzwa. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  10:21

Kwa Muhtasari

Zachariah Onchuru ni mmoja wa wakulima wa matikitimaji Pwani ambaye amepata ufanisi mkubwa wa kuhakikisha anapata mavuno mazuri na kuwauzia wateja matunda yenye afya.

 

MATIKITIMAJI yapo katika jamii ya matunda yanayotambaa ardhini.

Yanaorodheshwa katika kundi moja na matango au maboga. Aidha, matunda haya ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na yanayokuzwa kwa muda mfupi.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanahoji ekari moja ya matikitimaji iliyohudumiwa vizuri ina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 15-36 kwa msimu. Yanastawi katika maeneo ya joto la wastani, nyuzi kati ya 21-30 sentigredi. Hii ina maana kuwa hastawi maeneo yenye joto kali, baridi jingi, mvua ya masika na udongo unaotuamisha maji.

Zachariah Onchuru ni mkulima wa matunda haya kaunti ya Kilifi, na anasema yanahitaji kiasi cha mvua cha milimita 400-600 kwa msimu. Anatahadharisha kuwa mvua ya gharika husababisha ugonjwa wa fangisi na bakteria, pamoja na mimea na mazao kusombwa na maji.

"Mchanga au udongo yanapokuziwa matikitimaji uwe na virutubisho vya kutosha, na usiwe na alikali nyingi. Uwe na asidi ya pH kati 5.0-7.0," aeleza Onchuru. Mkulima huyu hutumia mfumo wa kisasa aina ya 'masterpiece' katika upanzi. "Masterpiece ni uaandaji wa mashimo kisha mbegu zikichipuka, matandazo yanawekwa ili kuzuia mnyauko wa maji hasa msimu wa kiangazi," afafanua.

Mbali na kuzuia mnyauko wa maji, matandazo hupunguza uotaji wa magugu au makwekwe, huongeza rutuba mchangani pamoja na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Nyasi ama mimea iliyokauka ndiyo bora kutumika kama matandazo. 

Kijana huyu anasema kwamba kipenyo cha mashimo kinalingana na weledi wa mkulima, urefu kuenda chini ukipendekezwa kuwa sentimita 45. Umbali wa shimbo moja hadi lingine uwe mita 2 kwa kuwa matikitimaji hutambaa. "Maeneo yasiyo na rutuba ya kutosha, mkulima anaweza kutumia mbolea ya mifugo au ya kisasa aina ya DAP. Mfumo ninaotumia hupanda mbegu tatu pekee katika kila shimo," aelezea.

Barobaro huyu mwenye umri wa miaka 25, alianza kilimo cha matunda haya 2013 katika robo ekari ya kukodi, shughuli iliyomgharimu Sh20,000 pekee. Kwa sasa amenunua zaidi ya ekari 10 kijiji cha Chakama, eneobunge la Magarini, Malindi, anazokuzia matikitimaji.

Anasema kinachorambisha sakafu wakulima wengi wa matunda haya ni kutojua mbegu na dawa maalumu. Kuna aina mbalimbali ya matikitimaji kama Asali, Kito, Sukari F1, Maridadi na Ndovu. Onchuru hukuza aina ya Sukari F1 kutoka kwa kampuni ya East Africa Seeds.

"Wakulima wafanye utafiti wa kutosha kujua mbegu bora kukuza pamoja na dawa maalumu za wadudu na magonjwa," ashauri, akiongeza kuwa maji yawe ya kutosha kwa mujibu wa vigezo vya kulima matunda haya.

Matunzo kwa mitikitimaji ni kuinyunyizia maji, kutia mbolea kama CAN, Urea au NPK (Top dressing), na kudhibiti magonjwa na wadudu dalili zinapoonekana kwa kutumia dawa zifaazo kwa mujibu wa maelekezo ya mshauri wa kilimo.

Aidha, huwa tayari kwa mavuno kati ya miezi mitatu hadi mitano baada ya upanzi, na kulingana na aina ya mbegu.

Wakati wa mahojiano Bw Onchuru alisema ekari moja inasitiri mitikitimaji isiyopungua 1,600. Aidha, kila mmea huzalisha matunda mawili, hivyo basi ekari moja ina jumla ya 3,200.

“Kila tunda huwa na wastani wa kilo nane, bei yake ikiwa Sh20 kwa kilo,” alieleza. Wateja wa mkulima huyu ni wa kijumla.

Kilifi inafahamika kuwa mojawapo ya kaunti kame nchini, lakini mkulima huyu anatumia maji ya Mto River kubadilisha taswira ya Pwani ambayo ni tajika kwa kilimo cha nazi na korosho. Sifa zake zimetanda katika nchi za Afrika Mashariki ambapo hutoa mafunzo maalumu ya upanzi wa matunda haya.

Tunda la tikitimaji limesheheni Vitamini C na linaaminika kupunguza magonjwa ya moyo. Aidha, wataalamu wa masuala ya afya wanasema lina kirutubisho ambacho huondoa sumu zinazosababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Vilevile, husaidia katika kuimarisha mifupa na kupunguza magonjwa yake, haswa kwa waliokula chumvi. Aidha, hupunguza na kuzuia mafuta kujikusanya mwilini pamoja na kuongeza maji kutokana na uwepo wa maji yake.

Yanaimarisha kinga ya mwili kwa sababu ya Vitamin C, ambayo ni muhimu katika kupambana na magonjwa ibuka. Faida zake ni nyingi kuzitaja, na ndio maana wataalamu wa masuala ya afya wanashauri tikitimaji lisikose katika orodha ya mlo wa binadamu aghalabu kila siku.