http://www.swahilihub.com/image/view/-/4612468/medRes/2009113/-/csj4ya/-/andalau.jpg

 

Muda mwingi wa kupumzika baada ya masomo chuoni aliutumia kwa kilimo

Derrick Mutugi

Bw Derrick Mutugi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) akivuna nyanya Juni 11, 2018, Ngoliba, Kiambu. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  17:30

Kwa Muhtasari

Si mwanafunzi mmoja, wawili au watatu ambao wameripotiwa kupotelea kwenye lindi la anasa kama unywaji wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na mihadarati. Visa vya wanafunzi kugura masomo na hata wengine kusajiliwa katika vituo vya kubadilisha mienendo si vigeni.

 

aVIJANA wengi wanapojiunga na chuo kikuu, taasisi ya juu ya elimu, husau shabaha iliyowapeleka humo ya kujiongeza ujuzi na maarifa.

Si mwanafunzi mmoja, wawili au watatu ambao wameripotiwa kupotelea kwenye lindi la anasa kama unywaji wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na mihadarati. Visa vya wanafunzi kugura masomo na hata wengine kusajiliwa katika vituo vya kubadilisha mienendo si vigeni.

Kijana Derrick Mutugi, mwanafunzi anayesomea Shahada ya Maswala ya Hesabu (Economics & Finance) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) anasema muda wake wa ziada huutumia kufanya zaraa. Akiwa na umri wa miaka 20, historia ya Wakenya wanaofanya kilimo nchini ikiandikwa jina lake halitakosa.

Anasimulia kuwa alipojiunga na KU miaka miwili iliyopita, ndoto yake ilikuwa kuimarisha maisha yake yawe bora.

“Ninaamini bidii huondoa kudura, ufanisi unategemea maono ya mtu binafsi,” anasema Bw Mutugi.

Wengine wakitumia mkopo wa Helb kwa starehe zisizofaa, Bw Mutugi aliutumia kwa njia ya kipekee.

“Kwa nini ninywe pombe, nitumie dawa za kulevya ama kuenda katika maeneo ya burudani kwa pesa zinazoweza kubadilisha maisha yangu?” auliza.

Mwaka 2017, kijana huyo alikuwa ameweka akiba ya Sh40,000.

Anasema alifanya utafiti kwenye mitandao ya kijamii, wakulima na kuhudhuria mafunzo ya kilimo jijini Nairobi yaliyomfungua mawazo. Mutugi anasema kwamba baada ya kujihami na maarifa ya kutosha, alikodi nusu ekari Ngoliba, Kiambu akaanzisha kilimo cha tikiti maji.

“Ekari nusu hiyo nilikodishwa Sh10,000 kwa mwaka na pesa zilizosalia kwa jumla ya Sh40,000, zikatumika kulima, kununua mbegu, mbolea, dawa na kulipa wafanyakazi,” afichua.

Miezi minne baadaye, alivuna tikitimaji zilizompa karibu mara dufu ya mtaji aliotumia. Kijana huyo anasema mapato ya mazao hayo yalimpa motisha, na kukodi ekari mbili zaidi.

“Februari 2018 nilipanda nyanya ambazo nilianza kuvuna mwezi Mei,” akaeleza Swahili Hub ilipomtembelea mtaani Ngoliba, kilomita moja hivi kutoka barabara kuu ya Thika-Garissa.

Wakati wa ziara yetu tulimpata akivuna nyanya na alisema wateja wake wengi hutoka Thika.

“Wateja hujia mavuno hapa hapa shambani,” akasema.

Mbali na nyanya, mwanafunzi huyo pia amepanda vitunguu vilivyobakisha mwezi mmoja pekee kuvunwa. Hali kadhalika, ana miche ya tikitimaji iliyoko kwenye kitalu.

Hata hivyo, wengi wanajisaili anamudu vipi kuendesha masomo na kilimo kwa wakati ule mmoja?

Anajibu, “Si wakati wote wanafunzi huwa darasani, kuna ule muda wa ziada ambao wengine huutumia isivyofaa na huo ndio ninautumia vyema”.

Changamoto

Hakuna kazi isiyo na pandashuka zake, alipoanza kilimo kupata wafanyakazi na soko ilikuwa balaa japo alitumia mitandao ya kijamii kutatua changamoto hiyo. Ana mfanyakazi mmoja aliyemuajiri ili kumsaidia akiwa shuleni na wakati kazi imekuwa nyingi kama msimu wa mavuno, na kupalilia huajiri vijakazi.

Mutugi anasema kilimo ndicho ofisi yake inayomlipia karo, na hata kusaidia wazazi wake kwa mahitaji mengine.

“Nikihitimu chuoni sitaacha ukulima hata nikipata ajira ya taaluma ninayosomea,” anasema.

Kwa hakika ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ndio changamoto kuu Kenya, na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto imekuwa ikitilia mkazo umuhimu wa kilimo ili kutatua swala hilo.

Wanafunzi wengi wanapofuzu huanza kusaka ajira, na iwapo Bw Mutugi atatilia maanani kilimo huenda akakosa kujipata kwenye mtumbwi wa wanaotaabika kutafuta kazi. Kuna baadhi ya vijana ambao wamegura kazi za ofisi ili kufanya zaraa na ufugaji, na kwa hakika baadhi yao wamekiri kuwa shughuli hiyo ina natija.