http://www.swahilihub.com/image/view/-/4181066/medRes/1805787/-/124bvvc/-/alaziki.jpg

 

Aila yenye kipaji cha muziki kutoka juu hadi chini

Samson Ng'ang'a Munyambo

Mwanamuziki Samson Ng'ang'a Munyambo akiwa na aila yake; mkewe na watoto wanajua kucheza ala za muziki. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, November 10  2017 at  11:06

Kwa Muhtasari

Talanta inafaa kutiliwa maanani kwa vile inaweza kukuajiri na kukupa riziki yako ya kila siku.

 

TALANTA inafaa kutiliwa maanani kwa vile inaweza kukuajiri na kukupa riziki yako ya kila siku.

Bw Samson Ng'ang'a Munyambo ameacha wanakijiji cha Gakui, Gatundu Kaskazini, wakiwa wenye furaha baada ya kujumuisha familia yake katika bendi yake ya kueneza injili.

"Mimi  kama mzazi naeneza injili kupitia  uimbaji  na nimeweza  kukuza  injili hiyo kwa kujumuisha  familia yangu. Bendi hiyo  inajumuisha mke wangu, vijana  wawili wa kiume na msichana mmoja," alisema Bw Munyambo.

Wakati mwingi Bw Munyambo hutumbuza wakazi wa kijiji chake katika soko lao na wakazi hao hufurahia ajabu.

Anasema jambo la kushangaza ni kwamba familia hiyo yote inaweza kupiga gitaa, kucheza kinanda pamoja na ala zingine muhimu za kutumbuiza waumini kanisani.

"Ama kwa hakika Mungu alinifunulia ndoto yangu kwani mke wangu na watoto walifurahishwa na ujuzi wangu wa kupiga gitaa na ndipo wakatamani kujifunza ili wawe kama mimi," anasema Bw Munyambo.

Anasema ratiba yake huwa ina utitiri wa shughuli kwa mwezi mzima kwa vile yeye huitwa kwenye harusi, mazishi, katika sherehe na pia kanisani ili aburudishe  waumini na wananchi.

Alisema hiyo talanta yake imemwezesha kupata fedha za kuikimu familia yake bila kuwa na shida na kwa hivyo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo.

"Nimewafunza watoto wangu kutokana na fedha ninazopokea kupitia uimbaji. Nawahimiza wazazi wawape nafasi wana wao kukuza talanta zao popote walipo," asema Bw Munyambo.

Anaeleza kwamba Mungu alimfungulia njia mwaka wa 1999 ambapo alianza kujifunza kuimba na kucheza gitaa. Hatua hiyo pia ilimsaidia kujumuisha familia yake mnamo 2002.

Yeye ni mshiriki wa Seventh Day Adventist.

Anasema licha ya shinikizo, ameamua kuendelea kuwa mfuasi wa dini yake na wala sio zile za wanaomshawishi.

Anasisitiza kuwa juhudi zake ni kuona kwamba watoto wake wanajiendeleza kwa kukuza talanta hiyo ya muziki wa dini na kucheza ala.

Anashajiisha kila mzazi achukulie kwa uzito talanta yoyote ambayo anaweza kuwa nayo na kumweka Mungu mbele kwa kila jambo.