Karibu Jaji Mkuu uziboreshe mahakama

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, September 12  2017 at  15:58

Kwa Mukhtasari

Rais John Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania baada ya ukaimu nafasi hiyo kwa muda wa miezi minane kabla ya Jumatatu alipomwapisha katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

RAIS John Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania baada ya ukaimu nafasi hiyo kwa muda wa miezi minane kabla ya Jumatatu alipomwapisha katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tunapongeza hatua ya Rais kukukabidhi jukumu hilo baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu mwezi Januari ina maana amekutathmini na kuona unastahili kusimamia mhimili huo.

Katika kipindi cha miezi minane ambacho umekuwa ukikaimu utakuwa umeshuhudia kwa macho yako changamoto mbalimbali za, ukosefu wa nidhamu, uhaba wa fedha na majengo ya mahakama, ucheleweshaji wa kesi na mgongano wa mihimili.

Tunadhani utakuwa umejiwekea mpango mkakati wa kushughulikia changamoto hizo ili kuzifanya mahakama zitumike kuwa chombo pekee za kimbilio kwa kila mtu na haki itolewe kwa wakati.

Inafahamika kuwa dola ni moja lakini ina mihimili mitatu ambayo imegawana majukumu.

Serikali Kuu, Bunge na Mahakama.

Serikali huandaa miswada, Bunge hutunga sheria ambazo hutafsiriwa na Mahakama.

Hata hivyo katika mikakati ya hivi karibuni Mhimili wa Serikali umekuwa ukigubika Mahakama.

Tunafahamu kuwa Serikali ni mdau mkubwa katika shughuli za Mahakama kwa kuwa Mwanasheria Mkuu ana kesi nyingi mahakamani.

Mbali na Mwanasheria Mkuu kuwa na kesi nyingi kiuhalisia Serikali ndiyo inatafuta fedha za kuendesha shughuli za mahakama na ndiyo kiini cha mhimili huo kusema una mizizi mirefu unayofika hadi kwenye mihimili mingine.

Hata hivyo katika suala la utoaji haki tunaomba mahakama isimame kwa miguu yake isishurutishwe na isiingiliwe.

Majaji wazingatie sheria nwakati wa kutoa hukumu.

Haiingii akilini kama mahakama inatoa amri fulani lakini watendaji walioko chini ya Serikali wakapuuza na wakaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna amri yoyote.

Mfano halisi ni ubomoaji wa nyumba unaoendelea katika baadhi ya maeneo nchini hasa katika Jiji la Dar es Salaam ambazo nadaiwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara.

Katika eneo moja nyumba za wananchi ambazo mahakama ilitoa ubomoaji usitishwe, maofisa waliokuwa wakisimamia kazi hiyo waliendelea kubomoa na mahakama ikakaa kimya.

Umalizaji kesi

Jambo jingine ambalo tunadhani Jaji Mkuu atalisimamia vyema ni umalizaji wa kesi.

Baadhi ya kesi zimekaa muda mrefu mahakamani kwa madai mbalimbali.

Kuna kesi zinazoahirishwa mara kwa mara kwa madai kwamba upelelezi haujakamilika na nyingine kwa maelezo kuwa hakimu amesafiri au ana udhuru na sababu nyingine nyingi.

Tunaomba masuala yote mawili na hasa ucheleweshaji wa kesi kwa visingizio vya upelelezi haujakamilika au faili la kesi haijaonekana yakomeshwe ili haki isicheleweshwe.

Vilevile tunaomba juhudi zifanyike ili kuboresha mahakama ili kuwafikia zaidi Watanzania kwa kuwasogezea kwa karibu huduma za kisheria au mahakama wasitembee kitambo kirefu kufuata haki.

Kwa mfano katika miaka ya hivi karibuni kulikuwa na mpango wa kusogeza huduma za afya na elimu, kuwa na zahanati katika kila kijiji na kuwa na kituo cha afya katika kila kata.

Mkakati huu unaweza kutumiwa hata na idara za mahakama ili kuwa na Mahakama za Mwanzo walau katika kila kata.

Mafanikio wa ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na polisi yalitokana na Serikali kuwahamasisha na kuwashirikisha wananchi, tunadhani mbinu hizo zinaweza kutumiwa na hata ujenzi wa mahakama ili kupunguza gharama za kutafuta haki.

Vilevile mahakama zitumie Tehama na kuona uwezekano wa kesi kubwa kuamriwa kwa uwazi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.