Kuchoma vifaranga ni kukomoa au adhabu?

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, November 3  2017 at  10:14

Kwa Muhtasari

Mjadala mkubwa umeibuka tangu vifaranga 6,400 waliodaiwa kuingizwa Tanzania kinyume na sheria wachomwe eneo la Namanga mkoani Arusha.

 

MJADALA mkubwa umeibuka tangu vifaranga 6,400 waliodaiwa kuingizwa Tanzania kinyume na sheria wachomwe eneo la Namanga mkoani Arusha.

Vifaranga hao, mali ya Mary Matia wenye thamani ya TSh12.5 milioni walikamatwa kwenye mpaka mjini Namanga ambao ni mpaka wa Tanzania na Kenya.

Hatutetei uvunjwaji wa sheria au kitendo chochote kinachokwenda kinyume na taratibu tulizojiwekea kama nchi lakini tunaamini busara ingetumika katika kushughulikia kadhia hiyo

Tangu habari hii ianze kusambaa, baadhi ya wadau na watetezi wa haki za wanyama wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu haki stahiki ambayo ilifaa kuchukuliwa na mamlaka hasika.

Kwa walio wengi, busara ingekuwa kumuadhibu mmiliki kwa kuwarudisha vifaranga hao walikotoka. Si jambo geni.

Mathalan mara kadhaa tumeshuhudia mifugo hususan ng’ombe wanaokamatwa kuingizwa kiholela nchini amamifugo ikitaifishwa na vyombo vya dola au ikirudishwa ilikotoka.

Inasikitisha kuwa wahusika katika uchomaji wa vifaranga hao hawakulitazama suala hili kwa upande mwingine hasa ukatili dhidi ya viumbe hai.

Tukikopa maneno ya mkurugenzi mtendaji wa Shrika la Ustawi wa Wanyama Tanzania (TAWESO) busara nyingine ingekuwa kuwapima vifaranga hawa na kama ingebainika kutokuwa na magojnwa ya kuambukiza mamlaka husika ingewataifisha na hata kuwagawa kwa wajasiriamali, magereza au vituo vya watoto yatima.

Inawezekana wahusika wana hoja nzito tena za kisheria zilizowasukuma kuteketeza vifaranga hao lakini hawakuona haja kutafuta njia mbadala badala ya kuwachoma; njia ambayo ni ya kikatili.

Katika sakata hili, utu ungeweza kuchukua nafasi zaidi huku  wahusika wakitekeleza sheria na taratibu zilizopo.

Tujifunze kutoka kwa mahakimu na majaji ambao wakatif fulani hutoa uamuzi kwa kutumia busara hasa baada ya kusoma mazingira ya tukio.

Walioshiriki kuteketeza vifaranga hao wangeweza kutumia njia nyingine kama kumtia adhabu mmiliki wa vifaranga hivyo.

Kinachogusa hisia ya wengi ni kuwa mmiliki huyo alishakuwa tayari kuwarudisha alikowatoa.

Kwa maneno mengine alishakubali kupata hasara jambo ambalo lingeweza kuwa funzo kwake kuwa alipaswa kutii sheria na taratibu za nchi.

Hatudhani kuwa sheria na taratibu na hata adhabu tunazojiwekea nchini zinalenga kukomaa bali kutoa fundisho ili kosa kama hilo lisitokee tena.

Kutoa elimu

Wakati ni wajibu kwa kila raia kufuata sheria na taratibu, mamlaka nazo zinawajibika kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa umma ili kupunguza vitendo vya ukiukwaji wa sheria.

Hivi ndivyo inavyotakiwa kufanywa sio na vyombo vinavyosimamia masuala ya ufugaji lakini pia vyombo vya usalama barabarani, usimamizi wa fedha na vingine vingi nchini.

Tujitahidi kuwa Taifa linaloamini katika adhabu hasa zenye mwelekeo wa kukomoa badala ya kufundisha. Ndio maana kunatakiwa kuwepo kwa uchunguzi wa mazingira ya kosa kama ni makusudi au kwa kutokujua.

Baadhi ya makosa hufanywa si kwa nia mbaya bali kwa kutokujua au kukosea. Haya yanaweza kushughulikiwa kwa kuangalia nia mbadala ambayo ni ya kielimu zaidi kwa manufaa ya baadaye.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647