JAMVI: Ushindani huu baina ya NASA na Jubilee huenda ukasukuma kura hadi 2018

Waziri Mkuu Raila Odinga

Mwaniaji urais wa NASA Raila Odinga. Picha/MAKTABA 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, July 16  2017 at  15:18

Kwa Mukhtasari

MWONGOZO wa kikatiba kuhusu idadi ya kura ambazo mgombeaji urais anapasa kujizolea kabla ya kutangazwa mshindi pamoja na ushindani mkubwa uliopo kati ya mirengo miwili mikuu ya kisiasa nchini, Jubilee na NASA, huenda zikachangia uchaguzi wa Agosti 8 kuendelea hadi Januari mwaka ujao, wataalamu wa kikatiba wanaeleza.

 

Kuna taratibu mbalimbali za kisheria ambazo lazima zizingatiwe, ili kuhakikisha mshindi amepatikana katika uchaguzi huo.

Rais Uhuru Kenyatta (Jubilee) na mgombea urais wa NASA, Raila Odinga ndiyo washindani wakuu katika kinyang’anyiro hicho.

Wakili wa kikatiba Wahome Gikonyo asema hilo litatokea ikiwa mshindi hatapatikana moja kwa moja baada ya Wakenya kupiga kura Agosti 8.

“Kikatiba, lazima mwaniaji atakayetangazwa mshindi wa urais apate asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kura moja zaidi ya kura halali (zilizopigwa). Ikiwa hilo halitaafikiwa, basi inamaanisha kwamba, nchi itajiandaa kwa duru ya pili ya uchaguzi wa urais,” asema Bw Gikonyo.

Anasema, mbali na hayo, ikiwa matokeo ya urais yatakayotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yanatapingwa na upande mmoja, basi hilo pia litaathiri mchakato mzima wa kumtafuta kiongozi mpya.

Asema: “Kulingana na Kipengele 140 (1) cha katiba, mtu yeyote anayetaka kuwasilisha kesi kuhusiana na matangazo ya urais amepewa muda wa siku saba. Hilo linamaanisha kwamba, ana hadi Agosti 22 kuwalisha kesi hiyo kwa Mahakama ya Juu. Hii ni kwa sababu, IEBC imepewa hadi muda wa siku saba kutangaza matokeo ya urais, yaani hadi Agosti 15 kuyatangaza.”

Septemba 5

Na ikizingatiwa kwamba mahakama hiyo imepewa muda wa siku 14 kutoa maamuzi ya uchaguzi huo, hilo linamaanisha kwamba, Wakenya watalazimika kungoja hadi Septemba 5, wakati mahakama itaamua ikiwa uchaguzi huo ulikuwa halali au la au ikiwa mshindi aliyetangazwa alishinda kihalali au la.

Bw Wahome asema, rais mpya anaweza kuapishwa tu mnano Septemba 12, ila hilo pia linaweza kukosa kufanyika.

Kulingana na wakili Bobby Mkangi, ikiwa mahakama itapata uchaguzi huo kutokuwa halali, au hitilafu katika matokeo, basi itabidi IEBC kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi.

Kulingana na kipengele 140 (3) cha katiba, duru ya pili ya uchaguzi inapaswa kuandaliwa katika muda wa siku 60.

Kwa hayo, mtaalamu huyo asema kwamba, kwa mantiki ya ufasiri wa kikatiba, uchaguzi huo unaweza kuandaliwa mnamo Oktoba 5.  Kimantiki basi, matokeo ya urais yatatangazwa kufikia 0ktoba 12.

“Lakini hali inaweza kuwa kama duru ya kwanza. Mshindi atatangazwa, ila katiba ingali imetoa mwanya wa kila mmoja kueleza hisia zake. Hili linamaanisha kwamba kutakuwa na uwezekano wa kesi kuwasilishwa tena. Kikatiba, mlalamishi ana hadi Oktoba 19 kuwasilisha kesi hiyo,” asema Bw Mkangi.

Novemba 2

Aidha, anaongeza kuwa kwa kuzingatia kwamba kesi hiyo inapaswa kuamuliwa kwa muda wa siku 14, hilo linamaanisha kwamba Mahakama ya Juu itakuwa na hadi Novemba 2 kutoa uamuzi kuhusu matokeo hayo. Lakini kikatiba, mahakama inaweza kuyakubali ama kuyafutilia mbali, na kuamua uchaguzi mkuu mpya kuandaliwa.

Na kuzingatia mpangilio wa kikatiba, hilo linaweza kufanyika hadi Januari 2, 2018 kwa kuwa tume imepewa siku 60 kuandaa uchaguzi mpya.

Kwa kauli hiyo, mchanganuzi wa kisiasa Kipkorir Mutai asema kwamba, kwa hali hizo, Wakenya na wawaniaji wadhifa wa urais lazima “wajitayarishe kisaikolojia” kwa uhalisia huo wa kikatiba.

Asema kuwa ukaribu wa umaarufu wa Mabw Kenyatta na Odinga huenda ukachangia nchi kuingia kwenye duru ya pili ya uchaguzi, ikiwa hali haitabadilika.

“Wawili hao (Kenyatta na Odinga) wanafahamu hayo, na ndiposa wameweka mikakati mahsusi kuhakikisha wameibuka washindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi,” asema Bw Mutai.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2013, Bw Kenyatta (TNA) alitangazwa kuwa mshindi kwa kuzoa asilimia 50.7 ya kura, huku Bw Odinga (ODM) akishinda asilimia 43.7 ya kura.

Hali kutobadilika

Hali hiyo inaonekana kutobadilika kwa kuwa, kwenye utafiti wa kura ya maoni uliotolewa juzi na shirika la Infotrak, Rais Kenyatta alipata asilimia 48, akifuatwa kwa karibu na Bw Odinga, aliyeorodheshwa kupata asilimia 43.

Wachanganuzi wanataja ukaribu huo kama ishara ya uwezekano wa mmoja kati ya hao kuibuka mshindi.

“Hii ni ishara ya ushindani mkali utakaokuwepo kati ya mirengo hiyo miwili,” asema Bw Mutai.

Mchanganuzi wa kisiasa Prof Macharia Munene asema kupata mshindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza, itakuwa manufaa kwa nchi ili kuepuka uwepo wa taharuki ya kisiasa.

“Tutaepuka hali ya taharuki ya kisiasa kama ilivyokuwa mnamo 2013, wakati kila mmoja alingoja uamuzi wa mahakama. Mbali na hayo, wawili hao (Kenyatta na Odinga) wangetaka sana kuepuka uchovu unaotokana na michakato mirefu ya maamuzi ya mahakama,” asema Prof Munene.