Heko Magufuli kuunda wizara mpya kuboresha mambo

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, October 10  2017 at  09:34

Kwa Mukhtasari

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais John Magufuli alifanya uamuzi wa makusudi wa kuunda wizara mbili mpya ili kusaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi hasa katika awamu hii inayotilia mkazo uchumi wa viwanda.

 

MWISHONI mwa wiki iliyopita Rais John Magufuli alifanya uamuzi wa makusudi wa kuunda wizara mbili mpya ili kusaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi hasa katika awamu hii inayotilia mkazo uchumi wa viwanda.

Wizara mpya ni ya Madini baada ya kuigawa iliyokuwa inaitwa Wizara ya Madini na Nishati na nyingine ni ya Ufugaji na Uvuvi baada ya kuigawa iliyokuwa inaitwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Tunaungana na wadau wengine wa maendeleo kupongeza hatua hiyo hasa ikizingatiwa mchango mkubwa wa wizara hizo katika maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na nchi kwa jumla.

Hatua ya kufanya kilimo eneo linalojitegemea imefanywa kwa makusudi kutokana na mambo mawili.

Kwanza sekta hiyo ndiyo inayoajiri watu wengi nchini kuliko sekta nyngine yoyote.

Pili, tunadhani Serikali inataka kuja na mkakati wa kuhakikisha kilimo, ufugaji na uvuvi katika awamu hii vinatumia teknolojia ya kisasa kwa vitendo.

Baada ya uhuru kutokana na umaskini wa kipato cha watu, mkazo ulikuwa kutumia majembe ya kukokotwa na wanyama kama ng’ombe na punda pamoja na mbolea. Baadaye mkazo ukawa kutumia matrekta, mbolea na dawa za kuulia wadudu.

Katika awamu hii ya uhamasishaji na usimamizi wa viwanda, mbali na Serikali kuendelea kuhamasisha matumizi ya matrekta makubwa na madogo yanayotumia injini yaani power tiller tunashauri uangaliwe utaratibu wa kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia nyingine ya mashine za mkono za kulimia, kupanda, kupalilia na kuvuna.

Mashine hizi kama ambavyo watu huziona kwenye maonyesho ya biashara ndani na nje ya nchi na kwenye mitandao, zitaongeza wigo wa teknolojia hivyo kuwawezesha wakulima kulima eneo kubwa  kwa muda mfupi na pale wanapoambiwa na wataalamu kwamba mvua za kwanza ni za kupandia  wafanye hivyo kwa vitendo.

Miaka mingi iiyopita tatizo la wakulima wengi  lilikuwa ni kuachana na jembe la mkono lakini baadaye wengi wao waliliacha  lakini hata walioliacha wapo wasiotumia mbolea na dawa ya kuua wadudu.

Tena wapo baadhi ya wakulima na hata Serikali inajua kwamba wanapewa mbolea za ruzuku ili wapande lakini wanauza na wao hupanda mazao katika ardhi liyochoka na hatimaye hupata mazao kiduchu.

Wakati mwingine hali hiyo inatokana na usimamizi mdogo wakulima kuridhika na hali yao au maofisa ugani kushindwa kuwafikia wakulima kwenye maeneo yao na kuwapa elimu ya kutosha  kuhusu umuhimu wa mbolea iwe ya kisasa au samadi.

Tunatoa wito kwa maofisa hawa watimize wajibu wao ili kilimo na ufugaji viwe na tija maana kadiri kilimo kinavyokuwa cha kisasa ndivyo vijana wengi zaidi wanavyovutika  kushiriki badala ya  kubakia mijini kufanya kazi za kijungu jiko.

Wito wetu mwingine  ni masoko ya mazao. Upo ushahidi kwamba katika baadhi ya maeneo wakulima hukumbana na tatizo la uhaba wa mauzo ya mazao yao. Kwa mfano katika miaka ya hivi karibuni kulikuwa na tatizo la soko la korosho na hivi sasa sokola mbaazi.

Viwanda hivi vinavyojengwa ni vile vitakavyotumia mali ghafi inayopatikana nchini  kama vile mazao ya wakulima, bidhaa za uvuvi na ufugaji.

Tunatoa wito kwa mawaziri wa wizara hizo kwamba kazi iwe kuhamasisha kilimo, uvuvi, ufugaji wa kisasa lakini pia tuwatafutie masoko kwa mazao yao.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647