http://www.swahilihub.com/image/view/-/3963894/medRes/1666625/-/10ejq35/-/fed.jpg

 

Wajua la kufanya ili ng'ombe atoe maziwa mengi?

Stephene Mathenge

Ng'ombe wa maziwa wa Bw Stephene Mathenge mfugaji maarufu wa ng'ombe wa maziwa Kiangai Kirinyaga. Matunzo mazuri ya ng'ombe kwa kuzingatia lishe bora humzalishia maziwa mengi. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, June 9  2017 at  19:45

Kwa Mukhtasari

Siri ya kuzalisha maziwa mengi ni kulisha ng'ombe kwa chakula chenye madini tele, anasema Stephene Mathenge mfugaji wa ng'ombe wa maziwa.

 

SIRI ya kuzalisha maziwa mengi ni kulisha ng'ombe kwa chakula chenye madini tele, anasema Stephene Mathenge mfugaji wa ng'ombe wa maziwa.

Kwa takriban miezi mitano sasa taifa limekuwa likishuhudia upungufu wa uzalishaji wa maziwa miongoni mwa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa. Aidha hali hii imepelekea bei ya maziwa kuongezeka karibu mara dufu, huku wanaoishi maeneo ya mijini wakiathirika pakubwa kwa upungufu na ukosefu wa maziwa.

Lita moja ya maziwa yaliyopakiwa kwa sasa yanagharimu kati ya Sh70 - 80 kwenye maduka ya kijumla huku yale yanayotoka moja kwa moja kwa ng'ombe yakiuzwa kati ya Sh60 - 70 lita moja.

Hii ni bei ghali ikilinganishwa na uzalishaji wa maziwa unapoimarika. Maziwa yanayotoka kwa ng'ombe moja kwa moja lita moja huuzwa kwa Sh45, huku yale ya pakiti lita moja ikiuzwa kwa Sh50.

Licha ya mvua kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu,  bodi ya maziwa nchini (Kenya Dairy Board/KDB) inahoji hali ya upungufu wa uzalishaji wa maziwa nchini itarejelea kawaida kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kutoka sasa, hii ikidhihirisha wananchi wataendelea kushuhudia upungufu wa maziwa na kununua kwa bei ghali hadi mwezi Agosti.

"Kufuatia mvua iliyoanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa asilimia kidogo ya kati ya asilimia 10 - 20. Uzalishaji wa maziwa utakua pole pole kwa sababu ya kiwango kidogo cha mvua ambayo nchi inaendelea kupokea na utarejea hali ya kawaida ifikiapo Agosti," akasema Bi Margaret Kibogy maneja wa bodi ya maziwa nchini KDB akihutubu Alhamisi Juni8 katika ofisi za bodi hii Upper Hill jijini Nairobi wakati KDB ikiadhimisha miaka 90 ya kampuni ya Delamere kwenye usambazaji wa maziwa na bidhaa zinazoundwa kwa maziwa nchini.

Lakini je, unafahamu uzalishaji zaidi wa maziwa unategemea jinsi mfugaji wa ng'ombe wa maziwa anavyotunza ng'ombe?

Mfugaji maarufu wa ng'ombe wa maziwa Kiangai Kaunti ya Kirinyaga Bw Stephene Mathenge almaarufu mwalimu asema kiwango cha maziwa kwa ng'ombe kinategemea lishe kwa wanyama hawa wanaotupa bidhaa hii muhimu.

"Lishe ndio kiungo muhimu kwa uzalishaji bora wa maziwa kwa ng'ombe. Kuna wanaodhani ukilisha ng'ombe kwa chakula kingi ndipo watakupa maziwa mengi, hapo huwa wamenoa," asema Bw Mathenge.

Kulingana na mfugaji huyu madini kwa mnyama yeyote ndio jambo la maana kuzingatia iwapo mfugaji anataka kupokea matokeo mazuri.

"Kwa vyovyote vile, ng'ombe anahitaji malisho yenye uwiano wa nguvu ya wanga na mafuta (carbohydrates na fats), protini, madini (minerals), faiba (fibre) na vitamini. Hayo ndio msingi dhabiti wa kuzalisha maziwa mengi kwa ng'ombe," ashauri Bw Mathenge.

Aidha aongeza kuwa maji ndio kiungo muhimu kwa mifugo. "Maji kwa mifugo yoyote yanafaa kuwa kwa wingi, kama vile binadamu hushauriwa kunywa glasi nne za maji kila siku. Ng'ombe wanafaa kunywa maji mengi kwa siku, kwa sababu maziwa huundwa kwa kutumia maji na chakula wanachokula," asema.

Chakula wanacholishwa kinafaa kiwe cha kusagwa upesi mwilini ili virutubisho ama madini  yake yafyonzwe mwilini na hayapaswi kuwa na sumu.

Bw Mathenge ashauri chakula cha ng'ombe hususan nyasi kinafaa kuwa kimekauka.

"Makosa wanayofanya wakulima wengi ni kuwapa ng'ombe nyasi ambazo ni bichi. Chakula chochote unachowapa ng'ombe kinafaa kuwa kimekauka kwa sababu madini yake huwa yamekolea na kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa," akaeleza Swahilihub ilipomzuru kwenye mradi wake wa ng'ombe ulio na zaidi ya ng'ombe 20 wa maziwa.

Yote tisa, la kumi anayozingatia zaidi ni usafi wa zizi na mazingira ya ng'ombe.

"Makazi ya ng'ombe yanafaa kuhifadhiwa safi kila asubuhi na jioni, chakula kiwekwe mahali safi na maji pia yawe safi. Chumvi ya ng'ombe haifai kutiwa majini ila itiwe kwenye mlo wake ama wale moja kwa moja," aeleza.

Mathenge asema ana daktari wake wa mifugo anayewakagua kila mwezi ama dalili ya unyonge inapoonekana kwa ng'ombe wake.

Mfugaji huyu amehifadhi ng'ombe wa aina ya Friesian na Jersey.

Kulingana naye kila ng'ombe kwa siku humpa zaidi ya lita 30, kufuatia sheria zake za ufugaji na utunzaji bora wa ng'ombe anaozingatia.

"Mimi hupokea kitita kizuri cha pesa kupitia mauzo ya maziwa ya ng'ombe. Haswaa msimu huu ambao maziwa ni finyu ninakula kwa kijiko, japo situmii nafasi hii kukandamiza wengine. Bei yangu ni iliyoko sasa sokoni," akasema mfugaji huyu akiomba kutofichua kiasi kikubwa cha pesa anachopata mwishoni mwa mwezi.