http://www.swahilihub.com/image/view/-/3178632/medRes/1313190/-/kb5gw8z/-/PLEASECALLME.jpg

 

Madereva wa Serikali wawe mfano wa uendeshaji magari

Jaguar

Jaguar. Picha/HISANI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, August 6  2018 at  08:05

Kwa Muhtasari

Tasnia ya habari ilimpoteza mwanahabari, Shadrack Sagati katika ajali iliyotokea mkoani Geita ambayo pia iliwaacha watu wanne wakiwa majeruhi wa ajali hiyo.

 

MWANZONI mwa wiki jana, tasnia ya habari ilimpoteza mwanahabari, Shadrack Sagati katika ajali iliyotokea mkoani Geita ambayo pia iliwaacha watu wanne wakiwa majeruhi wa ajali hiyo.

Katika ajali hiyo ilielezwa kwamba, Sagati na wenzake walikuwa wakisafiri kutoka mkoani Kagera kwenda Mwanza, wakiwa katika safari ya kikazi kutembelea miradi mbalimbali ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji ambako pia mwanahabari huyo alikuwa ni ofisa habari.

Taarifa ya kamanda wa polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo ilieleza kuwa gari alilokuwamo mwanahabari huyo ambalo pia lilimbeba naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Ludovick Nduhiye lilipinduka wakati likimkwepa mtembea kwa miguu katika eneo la Katoro mkoani humo.

Kamanda alisema licha ya kumkwepa mtu huyo kuwa chanzo cha ajali hiyo, pia gari hilo lilikuwa katika mwendokasi mkali ambapo dereva ambaye pia alijeruhiwa, alishindwa kumudu kulituliza vizuri barabarani.

Wakati jamii ikiwa bado inatafakari juu ya tukio hilo, jana gari la Serikali analotumia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla lilipata ajali asubuhi katika eneo la Magugu mkoani Manyara na kusababisha kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba.

Taarifa zilieleza pia kuwapo kwa majeruhi na hali ya waziri ilikuwa mbaya. Kama ilivyokuwa kwa tukio la Geita, pia chanzo katika tukio hili kilielezwa kuwa ni mwendokasi wa gari hilo.

Wakati tukitoa pole kwa wafiwa na majeruhi wa ajali hizo, tunapenda kuikumbusha Serikali ambayo iko katika mapambano ya kudhibiti na kuhakikisha kuwa ajali zinapungua nchini, ianzie kwa madereva wake.

Tunajua kwamba mawaziri na maofisa wengine wa Serikali wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata muda na ratiba wanazokuwa nazo, lakini hilo halihalalishi kwamba magari wanayotumia yawe yanaendeshwa kwa mwendo unaohatarisha maisha ya walio ndani.

Tunasema hivyo kwa sababu hatuioni sababu ya msingi ya ajali hizi kugharimu maisha ya ndugu zetu, ilhali unaweza kuwekwa utaratibu mzuri wa ratiba na muda wa kutekeleza majukumu ya wahusika.

Haiingii akilini kwamba kwa sababu kesho asubuhi ofisa wa Serikali ana ratiba ya kukutana na wananchi mkoani Dodoma, na leo kutwa nzima ameshinda akikutana na wananchi Iringa, basi aondoke asubuhi akiamiani kwamba gari analotumia litakimbia kwa kasi na kumfikisha salama huko Dodoma. Hili halipaswi kuwa vichwani mwa wahusika.

Ni vyema ratiba za viongozi na watendaji wa Serikali zikaacha muda mrefu wa wao kusafiri kwa mwendo wa kawaida ili waweze kufika salama waendako.

Isitoshe tunapenda kuwasihi maofisa wa usalama barabarani kuwa wakali kwa madereva wote wakiwamo wa Serikali, pale wasiporidhishwa na mwendokasi wa magari wanayoendesha. Uzoefu uliopo unaonyesha kuwa madereva hususan wa vigogo hawakamatiki na hasa wanapokuwa na mabosi wao.

Ni vyema trafiki wafike mahali kila gari liwapo barabarani walichukulie kuwa sawa na magari mengine ili kudhibiti ajali zinazotokana na mwendokasi wa madereva. Ni kwa kufanya hivyo, usawa utakuwapo baina ya madereva binafsi na wale wa Serikali na vilevile watasaidia kupunguza ajali zinazouilika.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647