http://www.swahilihub.com/image/view/-/4330112/medRes/1900963/-/87s3wez/-/bala.jpg

 

Madereva wawe makini wawapo barabarani

Aboud

Ajali ya basi la Kampuni ya Aboud iliyotokea mapema mwaka 2018 nchini Tanzania. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, March 6  2018 at  08:53

Kwa Muhtasari

Tumeanza mwezi Machi kwa neema ya mvua katika mikoa mingi ya Tanzania.

 

TUMEANZA mwezi Machi kwa neema ya mvua katika mikoa mingi ya Tanzania.

Neema iliyokuja baada ya wiki kadhaa za joto kali lililotishia uhai wa mimea na hata afya za watu na viumbe hai wengine.

Hata hivyo, kwa upande mwingine mwezi huu umeanza kwa majonzi makubwa.

Ndani ya siku nne kumeripotiwa ajali tatu ambazo zimesababisha vifo vya watu 12 na wengine kwa makumi kujeruhiwa.

Juzi watu watano walifariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya New Force lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Tunduma mkoani Songwe na basi dogo aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea Mlali wilayani Mvomero kwenda mjini Morogoro katika eneo la Rugemba Barabara ya Morogoro–Iringa.

Taarifa za awali kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Hiace aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na kukutana uso kwa uso na basi hilo lililokuwa katika njia yake. Juzi hiyo hiyo watu wengine sita walifariki dunia papo hapo na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya basi la abiria kugongana na lori huko Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gillece Muroto alisema ajali hiyo ilitokea mchana na kwamba katika ajali hiyo, majeruhi wako katika hali mbaya.

Ajali hizo zilitanguliwa na ile ya basi jingine la New Force lililotokea mkoani Songwe ambapo dereva wa basi dogo aina ya Toyota Altezza alifarikia dunia baada ya gari hlo kuacha njia yake n kugonga basi hilo linalofanya safari zake kati ya Tunduma na Dar es Salaam. Haya si matukio ya kuachwa yapite hivihivi tu.  La hasha! Athari zake ni kubwa mno  katika ngazi ya familia kwa kupata pigo la kupotewa na wapendwa wao hivyo kuziacha katika hali ngumu za kiuchumi.

Taifa pia limepoteza nguvukazi kubwa ambayo ilikuwa ikitegemewa katika kulikwamua kutoka hali ya umaskini iliyopo na kulifikisha katika uchumi wa kati.  Ni pigo kila upande.

Ipo kauli ya wahenga isemayo kwamba ajali haina kinga lakini tunadhani kuwa ajali inaweza kuzuilika

Tunaamini kuwa ajali inaweza kuzuilika kama tukichukua tahadhari za kiusalama hasa kwa madereva wawapo barabani muda wote.

Mathalan katika ajali hizo inaonyesha kwamba madereva wangechukua tahadhari pengine haya yote yasingetokea Hivyo madereva wanabeba abiria wanatakiwa wawe makini na waangaifu kila wakati wawapo barabarani.

Ni kweli kwamba kumekuwa na matukio machache ya ajali ikilinganishwa na miaka ya nyuma na hii ni kutokana na askari wa usalama barabarani kuimarisha usimamizi  lakini si rahisi kwa askari hao kuwa kila mahali.

Wakati tukitoa pole kwa ndugu waliopoteza wapendwa wao na kuwaombea wapate nafuu wale waliojeruhiwa, tunawakumbusha madereva kujisaili kabla ya kuchukua hatua yoyote wanapokuwa barabarani kwa maslahi yao, ya abiria waliowabeba, familia zao na Taifa kwa jumla.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647