http://www.swahilihub.com/image/view/-/2892314/medRes/1134237/-/uonwkv/-/SNTEACHERSSTRIKE0509w.jpg

 

Mageuzi shuleni yasilete mgogoro

Lydia Nzomo na Nancy Macharia

Mwenyekiti wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Dkt Lydia Nzomo (kulia) akiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Bi Nancy Macharia baada ya kuhutubia wanahabari jijini Nairobi awali. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na TAHARIRI YA TAIFA LEO

Imepakiwa - Wednesday, December 27  2017 at  06:34

Kwa Muhtasari

Hatua ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ya kuhamisha walimu wakuu 557 haifai kuzua mgogoro katika sekta ya elimu kwa sababu ni hatua ya kawaida na inayolenga kuboresha viwango vya elimu nchini.

 

HATUA ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ya kuhamisha walimu wakuu 557 haifai kuzua mgogoro katika sekta ya elimu kwa sababu ni hatua ya kawaida na inayolenga kuboresha viwango vya elimu nchini.

Ni unafiki mkubwa kwa Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya (Knut) kutishia kugoma shule zikifunguliwa ili kupinga hatua hiyo.

Iwapo kuna mwalimu yeyote mkuu aliye na malalamishi kuhusu mpango huo anafaa kutumia utaratibu unaofaa badala ya Knut kutoa vitisho vya mgomo.

Uhamisho wa walimu wakuu si suala linalohitaji majadiliano kati ya TSC na Knut kwa sababu ni jukumu la serikali kufanya mabadiliko yoyote yale kwa lengo la kuboresha utendakazi wa wafanyakazi wake.

Kuna shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri au vibaya kwa sababu ya usimamizi wa mwalimu mkuu na inafaa wakuu wa shule wahamishwe ili kusambaza ujuzi wa uongozi katika shule nyingine.

Kwa sasa, Knut inafaa kujihusisha na mjadala unaoangazia kuajiriwa kwa walimu zaidi ili kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi.

Tayari TSC imetangaza kuwa itakuwa ikiajiri walimu 12,696 kila mwaka kwa miaka minne ijayo, ahadi ambayo Knut inafaa kuhakikisha imetimizwa.

Kauli ya Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia, kuwa walimu hao wataajiriwa, inawapa matumaini maelfu ya vijana waliosomea ualimu lakini wakaishia kufanya vibarua baada ya kukosa kazi.

Mwanzoni mwa mwaka 2017, Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i, alisema kuna uhaba wa walimu 80,000 nchini ingawa maafisa wa vyama vya walimu wamekuwa wakisisitiza walimu wanaohitajika ni zaidi.

Mpango wa kuajiri walimu utawapa kazi vijana waliosomea ualimu na pia kuambatana na idadi kubwa ya wanafunzi.

Wakati huu katika shule za msingi za umma, mwalimu mmoja hushughulikia wanafunzi zaidi ya 100 darasani.

Huu ndio mjadala ambao Knut na wadau wengine wa elimu wanafaa kushughulikia badala ya kuharibu wakati kwa kuingiza siasa katika mpango wa kuhamisha walimu.
Kile wanafunzi na wazazi wanahitaji kwa sasa ni mazingira bora ya kusomea.