http://www.swahilihub.com/image/view/-/4646478/medRes/2033046/-/wpwh1q/-/makaroni.jpg

 

MAPISHI: Makaroni yaliyotiwa biringani na nazi

Makaroni

Makaroni yaliyotiwa biringani na nazi. Picha/HISANI 

Na MARGARET W. MAINA

Imepakiwa - Wednesday, July 4  2018 at  08:51

Kwa Muhtasari

Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kwamba makaroni ni chakula kama kamba kinachotengenezwa kwa unga wa ngano (uk. 279).

 

MAPISHI:Makaroni yaliyotiwa biringani na nazi

 

Kuandaa: Dakika 25

Mapishi: Dakika 15

Walaji : 2

ZIPO njia tofauti za kuandaa makaroni. Maelezo yafuatayo ni ya njia mojawapo ya kuandaa makaroni matamu na yenye mvuto wa kumfanya mlaji afurahie chakula. Makaroni ni laini, nyororo, rahisi na ya haraka kupika hivyo ni chakula kizuri, chenye afya na bora kuandaa kama huna muda mwingi wa kukaa jikoni.

 

Vinanyohitajika

Makaroni nusu pakiti, pima kulingana na mahitaji yako

Nyanya nne zilizoiva vizuri

Mchuzi wa nyanya/ Nyanya ya kopo (tomato paste) vijiko vitatu vikubwa

Vitunguu maji viwili

Kitunguu saumu kimoja

Pilipili mboga moja

Soy sauce kijiko kimoja kidogo

Chumvi kijiko kimoja kidogo

Giligilani kijiko kimoja kikubwa

Garam masala robo ya kijiko kidogo

Binzari kijiko kimoja kidogo

Tangawizi nusu kijiko kidogo

Nazi moja iliyokomaa

Njegere glasi moja

Biringani moja; kata vipande virefu na vyembamba

Italian seasoning kijiko kimoja kidogo

Pilipili ndefu 2 kata vipande vidogo vidogo

Udaha 'Cayenne pepper' kijiko kimoja kidogo

Maelekezo

Unaweza kuongeza viungo unavyopendelea ili kukifanya chakula kiwe kitamu zaidi. Ikiwa unakula na watoto, hakikisha unapunguza pilipili maana watoto wanaweza kushindwa kustahimili ukali wake.

Andaa viungo – menya nyanya, vitunguu maji viwili, pilipili mboga na kitunguu saumu. Kata vipande vidogo, hifadhi pembeni. Kamua tui zito la nazi, hifadhi pembeni.

Andaa njegere, zichemshe; ila zisiive sana, epua na weka pembeni.

Kwenye sufuria, weka maji na chumvi, acha yachemke. Weka makaroni, pika kwa kati ya dakika saba hadi nane (fuata muda elekezi kwenye paketi ya makaroni) kisha epua. Chuja maji, hifadhi pembeni.Ni vizuri ukipika makaroni dakika 1 au 2 chini ya muda elekezi kwenye paketi, hii itafanya makaroni yaive vizuri yakichanganywa na sauce na wakati wa kumalizia kupika.

Weka mafuta ya kupikia kwenye sufuria, bandika mekoni. Acha mafuta yapate moto vizuri kisha weka kitunguu maji. Hakikisha moto ni mkali ili mboga ziive vizuri bila kuchuja maji. Pika kwa dakika mbili huku unakoroga. Weka kitunguu saumu, bizari, tangawizi, pilipili ndefu, giligilani ya unga, italian seasoning na garam masala. Koroga vizuri kisha weka nyanya. Koroga vizuri kisha acha ziive hadi zitengane na mafuta. Weka nyanya ya kopo (tomato paste) na biringani, koroga pamoja.

Weka njegere, koroga pamoja. Weka soy sauce pamoja na chumvi kiasi. Weka makaroni kwenye sufuria. Changanya na sauce ya nyanya na njegere. Weka pilipili hoho, koroga na acha ziive kiasi, ili harufu iwe tamu na nzuri. Weka tui la nazi. Geuza mara kwa mara kisha acha chakula kichemke kidogo. Nyunyizia udaha na pilipili manga ichanganye na chakula kikishaiva epua.

Chakula kitakuwa tayari. Ili upate ladha zaidi, kula chakula hiki kikiwa bado cha moto.