http://www.swahilihub.com/image/view/-/4611418/medRes/2008154/-/i5qlpyz/-/telsta.jpg

 

Makocha Watanzania wasikubali kubaki wasaidizi

Telstar 18

Mpira rasmi wa Telstar 18 ambao utatumika katika mchuano wa fainali ya Kombe la Dunia ya Fifa 2018 wawasilishwa katika Kasri la Kremlin Desemba 1, 2017, jijini Moscow, Urusi. Picha/AFP 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, June 25  2018 at  08:46

Kwa Muhtasari

Hakuna anayekataa ujio wa makocha wanaotoka nje ya Tanzania, lakini hofu inakuja pale makocha wa aina hiyo wanapozidi kuongezeka.

 

TANZANIA katika siku za hivi karibuni imeshuhudia wimbi kubwa la makocha kutoka nje ya nchi kuja kufundisha timu zetu za VPL na inaelekea iko siku timu zote ishirini zitakuwa na makocha wa kutoka nje.

Hii ni mbaya na kama jitihada za makocha wazawa hazitawathibitishia viongozi wa timu zetu za VPL kwamba wanaweza.

Hakuna anayekataa ujio wa makocha wanaotoka nje ya Tanzania, lakini hofu inakuja pale makocha wa aina hiyo wanapozidi kuongezeka.

Idadi ya makocha kutoka nje kwa ligi ya msimu wa 2017/2018 ni wanane na wazawa walikuwa wanane.

Kwa mwenendo unavyoelekea, kati ya timu 20 za VPL za msimu wa 2018/2019, nusu ya hizo zitakuwa na makocha kutoka nje ya Tanzania na wengi kati yao watatoka Burundi na Rwanda.

Mathalan, tayari tumeshuhudia Biashara United ya Mara nayo ikisema iko mbioni kuajiri kocha kutoka Rwanda.

Kama ambavyo nimesema hapo juu, ujio wa makocha wa kigeni ni mzuri kwa sababu unaleta ujuzi na maarifa tofauti ya kupeleka ujumbe kwa wachezaji ambayo yanaweza kuwasaidia makocha wazawa.

Ningependa kutoa ushauri kwa makocha wazawa ambao watafundisha timu za VPL na viongozi wa timu hizo. Kama ambavyo nimekuwa nikisema na nitaendenlea kusema, binafsi naamini kwa dhati kwamba makocha wazawa wana sifa na vigezo kama makocha wengi wa kutoka nje wanaokuja hapa hususan kutoka ukanda huu wa Afrika.

Wengi wanaokuja hapa wana leseni za CAF daraja la A kama walivyo wengi wa makocha wazawa.

Kwa makocha wazawa wenye leseni hizo, wengi wao wana uzoefu wa kufundisha kwa miaka mingi na kwa mafanikio.

Katika kazi ya ukocha, uzoefu (na si cheti tu) una mchango mkubwa katika kuifanya kazi hiyo vizuri.

Jambo ambalo makocha wazawa wanatakiwa kulifanya, ni kuzingatia misingi ya kazi yao kama ambavyo mafunzo yao yaliwaelekeza wafanye wanapoandaa timu. Kocha ambaye ana mpangilio mzuri wa programu yake inayozingatia muda husika, atafanikiwa ikiwa tu atasimamia programu yake.

Changamoto ambayo naiona kwa makocha wazawa ni kutokusimamia misingi ya kazi yao.

Mathalan, kocha anakubali kuingia mkataba wa kufundisha timu hata pale ambapo mahitaji ya kuifanya kazi yake kwa ufanisi hayatatimizwa, mradi apate ajira. Hapo ndipo makocha wazawa tunapoanza kushindwa kupata mafanikio na wadau kuona kocha kutoka nje ana manufaa.

Masuala yote yanayotakiwa kuwekwa sawa kama wachezaji unaowataka, kutopangiwa timu, vifaa timilifu vya mazoezi na wakati wa mashindano na wachezaji kutimiziwa stahiki zao, kusimamia nidhamu ya wachezaji nje na ndani ya uwanja nk. lazima vizingatiwe.

Unapokubali kuifanya kazi katika mazingira yasiyo rafiki kwako, hutapata mafanikio na uongozi utakuondoa.

Nawashauri makocha wazawa kuwa jeuri maskini ili waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki na hivyo wao kupata matokeo.

Aidha, mambo mengi ya kujiendeleza katika ukocha yako katika mitandao, hivyo suala kubwa ni kukumbuka kujisomea mara kwa mara ili kujiongezea maarifa.

Kwa bahati nzuri, siku hizi mechi zote kubwa duniani zinaonekana moja kwa moja hivyo inakuwa rahisi kujifunza.

Ninashauri makocha wazingalie mechi hizo wakiwa wenyewe na si sehemu yenye kelele. Viongozi wa klabu watambue kwamba makocha wazawa wana sifa sawa na makocha wengi wa ukanda huu wa Afrika na hivyo wawaamini na wahakikishe programu za makocha hao zinatekelezwa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647