http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706648/medRes/2075140/-/ygqtby/-/mkiambua.jpg

 

Mambo si mazuri huduma za afya Kenya

Ferdinand Waititu

Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu (kulia), akielezewa na muuguzi jinsi mtambo wa CT Scan unavyofanya kazi kwa wagonjwa. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  13:47

Kwa Muhtasari

Itabidi Wakenya wabakie katika uponyaji wa kiimani badala ya kimatibabu katika hospitali za hapa nchini kufuatia ufichuzi wa uozo mkuu ulio katika huduma za sekta ya Afya.

 

ITABIDI Wakenya wabakie katika uponyaji wa kiimani badala ya kimatibabu katika hospitali za hapa nchini kufuatia ufichuzi wa uozo mkuu ulio katika huduma za sekta ya Afya.

Ikiwa sio migomo na vitisho vya kugoma kutoka kwa wauguzi ni wizi wa dawa, dawa ghushi, dawa ambazo muda wake wa matumizi umepita, hujuma kutoka kwa madaktari walio na hospitali zao za kibinafsi ambao husambaratisha huduma katika hospitali za umma, msongamano katika hospitali hizo za umma au gharama kuu za huduma za afya.

Haya ni maneno ya kusononesha ambayo yametolewa na mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu Afya, Sabina Chege akisema kuwa kuna haja kuu ya hali hii kubatilishwa, na aibu ya Wakenya kulia wamezuiliwa katika hospitali za hapa nchini kwa kukosa hela za kulipa bili zao (ikiwemo miili ya waliolemewa na magonjwa), ikome taifa.

Ingawa Waziri wa Afya, Sicily Kariuki anasema kuwa mikakati mathubuti inawekwa kulainisha hali ya sasa ya huduma duni, Bi Chege anashikilia kuwa kwa sasa kuna hatari kuu ya taifa kukosa kuafikia lengo kuu la serikali ya Rais Uhuru Kenyatta chini ya mwavuli wa ajenda nne kuu ambapo kuimarishwa kwa afya kwa wote ni mojawapo ya ajenda hizo.

“Sio siri kamwe kuwa dawa hapa nchini hazina ule uhakika kuwa ni za kutibu Wakenya. Zikiwepo, zinaibiwa katika hifadhi za serikali huku pia tukiwa na hatari ya kupokezwa dawa ghushi na zilizopitwa na wakati wa matumizi,” anasema Bi Chege.

Ripoti ya Shirika la kufuatilia biashara ya dawa ghushi duniani (GCMT) ya 2016 ilitaja Kenya kama kivukio kikuu cha biashara hiyo haramu ya madawa, ikisema kuwa ni mtandao ambao huzoa takribani Sh11 bilioni kwa mwaka.

Ilisema kuwa kuna mtandao wa watu serikalini katika sekta ya afya ambao hata huuza madawa ya kutibu wagonjwa wa Kenya katika mataifa jirani, huku wakizimba shimo hilo la uhaba wa dawa kupitia kuomba misaada kutoka kwa wahisani au kukubalia kampuni za kimataifa ‘kutupa’ dawa ambazo zimeharibikia katika mabohari yao hapa nchini.

Wengine wa maafisa hao walisemwa kuwa hushirikiana na wahisani kuandaa kliniki za umma za hadhara na bila malipo na ambapo rekodi huvurugwa ili kuzidisha gharama na kiwango, ya na cha, madawa yaliyotumika katika kliniki hizo.

Hivi majuzi, Mkurugenzi wa kimatibabu katika taifa jirani la Uganda, Dkt Diana Atwine akihojiwa na jarida la Observer alifichua kuwa Kenya ni mojawapo ya mataifa katika Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo huagiza dawa bandia na zilizopitwa na muda wa matumizi kwa wingi.

Alisema kuwa mtandao huo wa uagizaji dawa hizo hutumia vivukio vya Busia, Bugiri, Iganga na Soroti na kuangazia hali halisi kama ilivyonakiliwa na mamlaka ya National Quality Control Laboratories (NQCL) kwa pamoja na Pharmacy and Poisons Control Board (PPCB) kuwa zaidi ya asilimia 30 ya dawa hapa nchini hazina uwezo kamwe wa kutibu.

Mikakati

Katibu maalum katika Wizara ya Afya, Peter Tum anasema kuwa mikakati inaandaliwa ya kuimarisha sekta ya Afya na ambapo ni lazima kuwe na ule uwiano wa kiutendakazi kati ya serikali za Kaunti na Serikali kuu kwa kuwa asilimia 95 ya muundo mbinu wa sekta hii uko mikononi mwa ugatuzi.

Hayo yakiendelea kushuhudiwa, kwa mujibu wa utafiti wa 2017 kutoka kwa serikali na shirika la Foundation for Sustainable Development (FSD), kila mwezi, watu 9 milioni hukumbwa na matatizo ya kiafya yanayohitaji matibabu.

“Kati yao, wagonjwa 7.8 milioni husaka matibabu hospitalini na 120,000 kati yao huishia kulazwa.

Wote hutatizika katika hali moja au nyingine, ikiwa ni aidha kulemewa na gharama za kimatibabu, kupata huduma mbovu, ukosefu wa wataalamu na vifaa huku wengine wakikumbana na hali za kuwatelekeza kimakusudi,” yasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema kuwa licha ya kampeni nyingi za kuhamasisha Wakenya wajipe bima ya kimatibabu kwa Sh500 kwa mwezi, ni asilimia saba pekee ya asilimia 40 ya watu masikini ambao wamemudu gharama hiyo hadi sasa.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (Cotu), Francis Atwoli, mpango huu wa bima ni ghali mno kwa walala hoi.

“Wafanyakazi wengi hapa nchini ni vibarua ambao mahangaiko yao ni mishahara duni na ambayo hairidhiani na gharama za maisha. Ni hali ya kusikitisha kumtaka mfanyakazi huyo agharamie Sh500 kila mwezi za kimatibabu. Ni mpango mzuri ndio, lakini ambao hauzingatii hali halisi ya kiuchumi hapa nchini,” anasema.

Anasema kuwa hatari nyingine kuu katika sekta ya afya ni hali ambapo hospitali nyingi za umma zimeanza kususia kutibu wasio na kadi ya bima hiyo, hivyo basi kuzua hatari kuu ya wasio nayo kubakia manyumbani mwao wakingojea aidha imani iwaponyye, au wasalimu amri ya mkuki wa mauti.

Ripoti hiyo ya FSD inaonya kuwa kuna asilimia 38 ya wagonjwa ambao hukaa na magonjwa manyumbani mwao kwa sababu ya umasikini usiowaruhusu kusaka matibabu, wengine wao wakingojea hadi wahisani wajitokeze kuwagharamia matibabu.

Bi Chege anasema kuwa hali hii inawafanya wengine kugeukia matibabu kutoka kwa madaktari bandia mitaani ambao hujifahamisha kama waganga wa kienyeji.

Muungano wa Madaktari na wahudumu wa madawa nchini (KMPPDU) unasema kuwa hali kwa sasa katika sekta ya afya ni duni kutokana na serikali kukosa kujituma kutekeleza marekebisho na pia kuinyima ufadhili.

Katibu Mkuu wa muungano huo, Dkt Ouma Oluga anasema kuwa mataifa ya umoja wa Afrika (AU) yaliafikiana kufadhili sekta za afya katika mataifa wanachama kwa asilimia isiyopungua 15 ya pato lote la taifa katika kauli mbiu ya Abuja ya mwaka wa 2001.

Alisema kuwa Kenya haijakuwa ikijituma kutimiza kauli hiyo ya Abuja 2001 kwa miaka hiyo yote saba hadi sasa na pia kwa kiwango kikuu kumekuwa na ubutu wa sera za kusimamia sekta ya afya.

Aliongeza kuwa hata kile kitita kidogo ambacho hutolewa katika bajeti, huwa hakitumiki kwa njia ya maadili.

Aliongeza kuwa hatua ya serikali ya kuwaleta madaktari kutoka taifa la Cuba ni mojawapo ya ushahidi kuwa taifa limefeli katika kuweka sera zake katika mkondo wa ulainifu.

“Tunaleta madaktari huku tukiwa na wetu ambao hawana kazi. Hii ni mojawapo ya sababu ambazo zimefanya Kenya iorodheshwe kama mojawapo ya mataifa 57 yaliyo na changamoto kuu katika wahudumu kwa sekta ya afya,” akasema.

Thika Level Five

Hayo ya hali mbovu kando. Hospitali kuu ya Thika Level Five imepata dawa za kutosha huku wagonjwa wakihimizwa kutafuta hapo huduma.

Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu amekanusha 'dhana potovu' akisema ni mahasimu wake walioeneza uvumi kuwa hakuna dawa za kutosha katika hospitali hiyo.

"Mimi ningetaka kuwajulisha watu wote kuwa mgonjwa yeyote akija hospitalini hapa atapata dawa bila shida. Kwa hivyo nawahimiza wagonjwa wote wasikubali kupotoshwa na uvumi," alisema Bw Waititu.

Alisema kwa muda wa siku kadha kumekuwa na uvumi kuwa hospitali ya Thika ina upungufu wa dawa; jambo alilosema ni nia mbaya kwa Kaunti ya Kiambu.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi jioni alipozuru hospitali hiyo ili kujionea hali ya maendeleo na kuthibitisha kuwa lina dawa za kutosha.

Alilazimika kuzuru kitengo cha kuhifadhi dawa ambapo alijionea dawa za sampuli tofauti zilizosambaza hivi majuzi na kitengo cha kutoa dawa KEMSA.

Kuhusu wagonjwa kulala wawili kwenye kitanda kimoja alisema hiyo inatokana na wagonjwa wengi kufurika hapo kutoka kaunti jirani kama Murang'a, Machakos, na hata Nairobi.

"Tumepata changamoto nyingi za wagonjwa kufurika katika hospitali zetu za Kiambu hasa ya Thika Level 5 na Kiambu Level 4. Kwa hivyo kila mgonjwa huhudumiwa bila kubaguliwa na kwa hivyo kunasababisha msongamano," alisema Bw Waititu.

Alisema kwa wakati huu hospitali ya Thika ina vitanda 250 na kwamba haviwezi kutosheleza mahitaji ya wagonjwa wengi wanaofurika hapo.

Hata hivyo alisema mwezi Septemba hospitali ya Thika itafungua kitengo kingine kipya cha wadi chenye vitanda 300 kuwafaa wagonjwa wengi.

Alisema kwa siku za hivi karibuni hospitali ya Thika Level 5 imepiga hatua kwa kutoa huduma za kuridhisha wagonjwa na hata wageni kutoka maeneo mengine.

Katika ziara hiyo Bw Waititu aliandamana na maafisa wakuu wa afya wa kaunti ya Kiambu, na washika dau wa mji wa Thika.