Maonesho ya biasahara yawe fursa uchumi wa viwanda

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, June 28  2018 at  10:21

Kwa Mukhtasari

Maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanatarajiwa kushirikisha nchi zaidi ya 33 yakiwamo mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi na biashara duniani.

 

MAONYESHO ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanaanza leo Alhamisi hadi Julai 13.

Ni maonyesho yanayotarajiwa kushirikisha nchi zaidi ya 33 yakiwamo mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi na biashara duniani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Edwin Rutageruka maonyesho ya mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu yaanzishwe mwaka 1976 yatashirikisha nchi ya Saudi Arabia. Mataifa makubwa kama Japan, Ujerumani na Marekani ni miongoni mwa washiriki wazoefu watakaokuwapo.

Maonyesho haya pia yatashirikisha zaidi ya kampuni za ndani na nje 2,456 zikiwamo za kigeni 500 na taasisi za Serikali zipatazo 120. Kila mwaka katika maonyesho hayo huwa kuna bidhaa mpya na ubunifu mpya.

Wafanyabiashara wanapokutana mbali na kupata soko la bidhaa zao, pia hupata fursa ya kubadilishana uzoefu na kutengeneza mtandao mpana wa kitaifa na kimataifa katika uhusiano mpya wa kibiashara.

Hata hivyo, Rutageruka amesema kutakuwa na kliniki kwa ajili ya wafanyabiashara itakayohusisha kuwapa mafunzo ya mbinu mbalimbali za kibiashara, kuzijua sheria za biashara, namna ya kujenga mtandao wa kibiashara na utafutaji wa masoko ya bidhaa zao.

Kaulimbiu ya mwaka jana ilikuwa ‘ukuaji wa biashara kwa maendeleo ya viwanda’. Kwa mtazamo wa pekee ililenga kuyafanya maonyesho hayo kama jukwaa la kutangaza biashara na huduma mbalimbali kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya viwanda.

Bado azma yetu kama Taifa imelenga katika ukuaji wa sekta ya viwanda, pia Serikali imejiwekea lengo la kujenga viwanda 100 kila mkoa. Kwa mantiki hiyo maonyesho haya ni jukwaa zuri la kuhamasisha mikoa kuendeleza lengo la kujenga viwanda hivyo.

Tunafahamu kuna baadhi ya mikoa ina viwanda vinavyoendelea na uzalishaji, mfano Simiyu wana kiwanda kinachotengeneza chaki. Hivyo ni muhimu kwa viongozi wa mikoa kuyatumia maonyesho haya kuigeuza Tanzania katika uchumi wa viwanda kama Serikali ya Awamu ya Tano ilivyodhamiria.

Kupitia maonyesho haya, washiriki watatangaza huduma na bidhaa wanazozalisha ili kupata masoko endelevu ya nje na ndani ya nchi, kujenga mtandao wa kibiashara na kupata teknolojia za kisasa na kujifunza mbinu mpya za kuendeleza biashara zao.

Pamoja na kushindanisha ubora wa mabanda kwa washiriki ni muhimu wananchi nao wakapata fursa ya kujifunza mbinu mpya za kibiashara na namna ya kufanya uzalishaji wenye tija. Kubwa zaidi ni unafuu wa bei na urahisi wa upatikanaji wa teknolojia ya kisasa katika maendeleo ya kiuchumi.

Tunaamini eneo ambalo Tanzania haiko vizuri ni katika  teknolojia, hivyo maonyesho hayo ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza mbinu za namna ya kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kwenye kilimo kwa jumla.

Pia, msisitizo wetu kwa TanTrade na taasisi zingine kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) waendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waimarishe uzalishaji wa bidhaa bora zitakazopenya kwenye soko la kimataifa. Ni kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajenga uchumi mkubwa na imara.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647