http://www.swahilihub.com/image/view/-/4875704/medRes/369957/-/12iw1th/-/Tf1502pg11cover.jpg

 

Mapenzi kazini yanawezekana?  

Wachumba

Mapenzi motomoto. Picha/HISANI 

Na CHRISTIAN BWAYA

Imepakiwa - Friday, November 30  2018 at  13:07

Kwa Muhtasari

Kwa wafanyakazi wasiopata muda wa kukutana na watu wengine nje ya eneo la kazi, ofisi inaweza kuwa fursa ya mahusiano ya kudumu.

 

SEHEMU kubwa ya maisha yako kama mfanyakazi unaitumia kwenye eneo la kazi. Ingawa inategemea na aina ya kazi unayoifanya, ni wazi muda mrefu kwa siku unaoutumia kutekeleza majukumu yako unakuweka karibu zaidi na wafanyakazi wenzako kuliko hata familia na marafiki. Mazingira haya ya ukaribu wa kikazi, wakati mwingine, yanatengeneza uwezekano wa uhusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi.

Kwa kawaida, unapokuwa na mtu mnayefanya naye kitu kinachofanana kwa muda mwingi, ni rahisi kuanza kuvutiwa naye. Kadri mnavyoonana mara kwa mara ndivyo mnavyozidi kufahamiana kwa karibu. Hisia za mapenzi zinaweza kuzaliwa kama tahadhari hazitachukuliwa.

Msomaji mmoja ambaye hakujitambulisha jina lake aliniandikia ujumbe mfupi wa maneno, “Mazingira yanayoweza kuanzisha mapenzi kazini, Da. Nimeyasoma vizuri sana. Nahisi kama hayaepukiki hivi. Tatizo ni muda mwingi watu wanakuwa pamoja katika kufanya kazi… Issue (suala) ya mapenzi katika mazingira ya kazi haiepukiki.

Hayo ndio mambo yetu sie vijana.”

Kwa vijana wengi wanaoanza kazi, eneo la kazi linaweza kuwakutanisha na watu wanaoweza kuwa wapenzi wao.

Ni dhahiri ofisi zinakutanisha watu wenye uelewa usiotofautiana sana, wenye mtindo wa maisha usiotofautiana sana na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano ya karibu. Kukaa pamoja kwa muda mrefu pia inaweza kuwa fursa ya kumfahamu mtu anayeweza kuwa mpenzi wako bila yeye kufahamu kama Mage, 27, anavyofafanua.

“Ukisema nikwepe mapenzi kazini saa nyingine haiwezekani. Mimi karibu kila siku naondoka nyumbani saa 12 asubuhi narudi usiku saa 2. Nitaonana wapi na watu wengine?’

Kwa wafanyakazi wasiopata muda wa kukutana na watu wengine nje ya eneo la kazi kama Mage, ofisi inaweza kuwa fursa ya mahusiano ya kudumu.