http://www.swahilihub.com/image/view/-/4244080/medRes/1846142/-/tk4fi4z/-/shisha.jpg

 

Marufuku dhidi ya shisha yatekelezwe

Shisha

Mwanadada afurahia Shisha katika kilabu maalumu cha starehe hiyo jijini Nairobi mnamo Aprili 11, 2013. Picha/MAKTABA 

Na TAHARIRI YA TAIFA LEO

Imepakiwa - Friday, December 29  2017 at  06:30

Kwa Muhtasari

Hatua ya serikali kupiga marufuku uuzaji na uvutaji wa shisha inafaa ifuatwe na utekelezaji wake ufanyike kikamilifu.

 

HATUA ya serikali kupiga marufuku uuzaji na uvutaji wa shisha inafaa ifuatwe na utekelezaji wake ufanyike kikamilifu.

Ingawa hatua hiyo imetpkea kuchelewa, ikitekelezwa kikamilifu itasaidia kuokoa maisha ya vijana wengi ambao wamekuwa wakipuuza maonyo kutoka kwa wataalamu wa afya kuhusu madhara ya shisha kwa afya ya binadamu.

Tafiti zimethibitisha kwamba kiwango cha tumbaku kinachovutwa kutokana na shisha huwa ni kingi zaidi kuliko kile kinachovutwa kwenye sigara hata ingawa inafahamika wazi kwamba madhara ya sigara kwa afya pia ni mabaya mno.

Tangu shisha ilipoanza kupata umaarufu nchini hasa mijini, uvutaji wake umevutia idadi kubwa ya vijana, hasa wasichana wasiojua tumbaku huwa na madhara mabaya zaidi kwao.

Wengi wao wamekuwa wakipuuza maonyo yanayotolewa kwa sababu wanahadaiwa na ladha tamu ya shisha pamoja na ueneaji wa sifa zake kama bidhaa ya kisasa ya kujiburudisha ambayo asiyevuta ni mtu 'aliyebaki nyuma’ kimaisha.

Marufuku iliyotangazwa jana kupitia kwa Waziri wa Afya, Dkt Cleopa Mailu, isiwe kama sheria nyingine nzuri zinazopitishwa bila kutekelezwa.

Nchini humu kuna sheria tele na maagizo mengi yanayolenga kusaidia wananchi ambayo yamewahi kupitishwa lakini yakasalia kuwa maandishi tu kwenye karatasi yasiyo na maana yoyote.

Zaidi ya hayo, maagizo kama haya yanapotolewa na serikali huwa kuna maafisa laghai serikalini waliotwikwa jukumu la kuyatekeleza ambao hudondokwa mate kwani wanaona ni nafasi ya kujitajirisha kupitia kwa ulaji rushwa.

Itakuwa masikitiko makubwa kama maafisa husika hawatawajibika kutekeleza agizo hili la marufuku ya shisha na kuruhusu biashara hiyo kuendelea kisiri kwa njia za kilaghai.

Mbali na haya, tayari kuna manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao hawajapendezwa na hatua hii ya wizara ya afya.

Baadhi wanadai Dkt Mailu hana mamlaka ya kutoa marufuku aina hiyo, hivyo basi hii ni ishara kuwa huenda amri yake ikapingwa mahakamani katika siku zijazo.

Itakuwa vyema kama waziri kuhakikisha sheria zote zinafuatwa kikamilifu katika kutoa agizo hilo kwani si siri kwamba ingawa ni agizo lenye nia njema kwa maslahi ya umma, kuna wale watakaoathirika kibiashara na huenda wakatafuta kila sababu ya kufanya agizo hilo libatilishwe.