http://www.swahilihub.com/image/view/-/4709936/medRes/2077458/-/4pxygj/-/lugola.jpg

 

Matamko yasiyo ya kisheria hayasaidii

Kangi Lugola

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kangi Lugola. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, October 2  2018 at  08:22

Kwa Muhtasari

Kokote aendako Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amekuwa akitoa matamko ambayo huacha mawimbi katika jamii kwa siku kadhaa; hawa wakipongeza na wale wakitoa maoni tofauti.

 

KATIKA siku za hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amekuwa akitoa kauli nzuri zinazovutia masikioni mwa wasikilizaji wake.

Kokote aendako amekuwa akitoa matamko ambayo huacha mawimbi katika jamii kwa siku kadhaa; hawa wakipongeza na wale wakitoa maoni tofauti.

Baadhi ya kauli zilizoacha mawimbi na kusababisha watu kutoa maoni tofauti ni maelekezo aliyotoa akimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) afike ofisini kwake ifikapo saa 12 jioni akiwa na mbwa Hobby aliyedaiwa kupotea bandarini.

Kuna wakati aliagiza wakuu wa vyombo vya usalama chini ya wizara yake kubeba ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ili kutekeleza yale yaliyoahidiwa na chama hicho.

Kuna siku aliibua suala la ‘kupotea’ kwa mbwa wa upelelezi aitwaye Hobby, na alimtaka IGP kumpa ripoti au kwenda naye ofisini ifikapo saa 12 jioni ikiwa ni saa saa 10 tangu alipotoa agizo hilo.

Halafu siku alipozungumza na waandishi wa habari, aliagiza kuwekwa mahabusu dereva atakayebainika kusababisha ajali kwa uzembe na endapo ni ubovu wa gari basi mmiliki atahusika kulala mahabusu.

Mfano mzuri wa matamko yenye ukakasi kiutekelezaji ni alilolitoa mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa kwenye mkutano wa hadhara Kijiji cha Busanza wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma. Huko Lugola alikemea utaratibu wa watuhumiwa kunyimwa dhamana hasa siku za mapumziko kwa kisingizio kuwa si siku za kazi.

Alisema dhamana kwa mtuhumiwa inapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki ikiwamo Jumamosi na Jumapili kwa sababu vituo vya polisi nchini vinafanya kazi siku zote za wiki zikiwamo za mapumziko.

Kisha akasisitiza kwamba hatafumbia macho askari yeyote atakayeshindwa kutoa dhamana kwa kosa ambalo lina dhamana.

Kwa maneno yake waziri alishangaa akisema: “Hii tabia sijui imetoka wapi ambayo imejengeka kwa baadhi ya askari polisi, eti mtu akiingia mahabusu siku ya Ijumaa ikifika Jumamosi na Jumapili hawatoi dhamana wakisema dhamana mpaka Jumatatu, hii tabia siyo sahihi na ife haraka iwezekanavyo.”

Tunaungana naye pale anaposema dhamana ni haki ya mtu endapo kosa hilo linadhaminika, na tunakubaliana naye kwamba wananchi watakaoombwa fedha ili wapewe dhamana waripoti tukio hilo kwa maofisa wa ngazi za juu ili askari husika achukuliwe hatua za kinidhamu.

Hata hivyo, tunashindwa kumwelewa waziri katika maeneo kadhaa. Kwa nini anatoa matamko mazito kwenye mikutano ya hadhara wakati tulidhani alipaswa kukaa na maofisa wa polisi kuona warekebishe wapi na nini waboreshe katika utendaji hao?

Tujuavyo kuna mambo mengi wananchi wamekuwa wakiyalalamikia na kwa kasi aliyoingia nayo walikuwa wakidhani atakaa chini ili kufanyia marekebisho ama sheria au kanuni zake zilizotufikisha hapa.

Marekebisho yanayohitajika ni ya mfumo ambao hauwezi kubadilishwa kwa matamko katika mikutano ya hadhara au waandishi wa habari bali kukaa na watendaji. Msemo wa “kuingia polisi bure kutoka ni fedha” haukuanza leo hivyo hauwezi kukoma kwa matamko tu bila kuwakutanisha watendaji wakuu na kuona ni namna gani wanaokamatwa na kuwekwa ndani wanaweza kutoka bila kutoa fedha.

Pia, tumefuatilia na kubaini kwamba baadhi ya matamko anayotoa si ya kisheria, hivyo utekelezaji wake umekuwa mgumu au umeshindikana. Jeshi la Polisi ni letu na linapaswa kuzingatia sheria katika utekelezaji ili kulinda amani na utulivu, watu na mali zao na kujali haki za binadamu, halipaswi kusimamiwa kwa matamko.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647