http://www.swahilihub.com/image/view/-/4956478/medRes/2236772/-/1348c1v/-/usarama.jpg

 

Kilimo: Matufaha yanaweza kufanya vyema nchini Kenya

Matufaha

Bw James Macharia, afisa na mtaalamu wa kilimo ambaye pia ni mkulima wa matunda, katika kiunga chake Murang'a akionesha matufaha anayopanda. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  12:01

Kwa Muhtasari

  • Matufaha yana faida chungu nzima
  • Tufaha ni tunda lenye mbegu chache na nyama nyingi nyeupe na zenye utamu

 

KWA mwaka Kenya hununua zaidi ya tani 10,000 za matufaha kutoka kwa mataifa ya kigeni.

Matunda haya yanapendwa kutokana na tija zake tele kiafya na kimapato hasa kwa wafanyabiashara.

China ndiyo inaongoza katika orodha ya mataifa yanayoyazalisha kwa wingi duniani, kwa mwaka ikikuza karibu tani milioni 37.

Inafuatwa na Marekani inayozalisha tani milioni 4.11 na Uturuki tani milioni 2.88.

Nchi zingine bora katika kilimo cha matufaha ni; Poland tani milioni 2.87, India (2.20), Italia (1.99) na Brazil (1.81). Barani Afrika mataifa yanayokuza matufaha kwa wingi ni; Misri, Morocco, Afrika Kusini, Tunisia na Nigeria.

Licha ya Kenya pia kuyapanda-kwa uchache, asilimia 98 ya raia wanaamini nchi hii haina uwezo wa kuyazalisha. Wataalamu wa masuala ya kilimo hata hivyo, wanasema taifa hili lina mchanga na hali bora ya anga kupanda matufaha.

Bara Uropa hukuza na kuvuna msimu mmoja kwa mwaka kwa sababu ya kipindi kirefu cha baridi.

James Macharia, afisa wa kilimo nchini anasema kwa kutumia mfano wa Uropa, ina maana kuwa uzalishaji wa matufaha Kenya unaweza ukawa wa misimu miwili. Msimu wa baridi kali nchini hushuhudiwa kati ya mwezi Julai hadi Agosti.

Matofaha yanakua vyema katika maeneo ya baridi, inayohitajika ili majani yapukutike kuruhusu uchanaji maua yanayozaa matunda yenyewe.

Wataalamu wa kilimo husema "baridi huyapa matufaha mzongo wa mawazo, majani yapukutike ili yaanze kuchana maua kwa sababu ndiyo hatua gumu".

Aidha, yanahitaji baridi kati ya nyuzi 7-10 sentigredi, kiwango hiki kikiwa maeneo yanayozalisha majani chai na kahawa. Nyamira, Nyeri, Bomet, Kiambu, Kericho, Nandi, Muranga, Kisii, Meru, Kirinyaga, Embu , Kakamega, Nakuru na Trans Nzoia, ni baadhi ya kaunti zinazozalisha majani chai kwa wingi nchini. Maeneo ya Kati mwa Kenya kama Nyeri, Murang'a, Meru, Kiambu, Kirinyaga na Embu ndiyo yanajulikana katika kilimo cha kahawa.

"Kinachoshurutisha Bara Uropa kuvuna msimu mmoja pekee kwa mwaka ni kipindi kirefu cha baridi. Kenya, baridi hushuhudiwa mwezi Julai-Agosti, na kiasi Aprili hadi Mei," anaeleza Bw Macharia. Kwa kuwa matufaha yanahitaji baridi majani yapukutike ili uchanaji wa maua uanze, mtaalamu huyu anasema shughuli hii inaweza ikafanywa wakati wa misimu hii miwili ya baridi nchini Kenya kwa njia ya mkono (artificial).

"Yakipukutuliwa majani na mchipuko wowote ule wa matawi kwa mikono yapewe muda kati ya wiki 2-3, kisha yanyunyiziwe maji kwa wingi yataanza kuchana maua mara moja. Hii ina maana kuwa baada ya mwezi Mei na Agosti, Kenya itakuwa ikivuna matufaha," Macharia afafanua. Mkulima anahimizwa maua yanapoanza kuchana 'yalishwe' maji kwa wingi.

Upanzi wa matawi

Mbegu za kupanda matufaha ni matawi yake (cuttings), yanayopandwa katika mashimo. Taratibu za upanzi na utunzaji wake ni sawa na za matunda mengine. Bw Macharia anashauri haja ya kutumia mfumo wa kisasa katika kuyapanda, ujulikanao kama 'kupandikiza' kwa Kiingereza 'grafting'.

Mtindo huu unahitaji miti ya matunda mengine kama; maembe, machungwa, loquat... Yanayokatwa tawi, lililosalia linachongwa na kupandikiza lile la tofaha.

"Mbinu hii inazuia miti kunenepa na kuiwezesha kuzaa kwa wingi," anasema mtaalamu Macharia ambaye pia ni mkulima wa matunda haya Murang'a. Ana kiunga cha matunda, miche ya matunda na mimea ya dawa asilia, chenye ukubwa wa ekari moja na nusu.

Mitunda ya matofaha ipandwapo, huchukua muda wa miaka miwili ili kuanza mavuno. Ni muhimu kukumbusha kuwa inahitaji matunzo kwa njia ya maji, mbolea na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu.

Mchanga tifutifu (loamy) na mchanga halisi (sandy) ndio bora katika kilimo cha matufaha. Unapaswa kuwa usiotuamisha maji na kuruhusu hewa kuingia, ili kupata mazao bora na mengi. Tufaha moja nchini huuzwa zaidi ya Sh20.