http://www.swahilihub.com/image/view/-/4688474/medRes/2062768/-/8dd9hk/-/mbalala.jpg

 

Hili la Mawaziri Kenya litafikia wapi?

Najib Balala

Waziri wa Utalii na Wanyamapori nchini Kenya, Najib Balala. Picha/MAKTABA 

Na DOROTHY CHEBET

Imepakiwa - Wednesday, August 8  2018 at  12:56

Kwa Muhtasari

Kabla ya kumtembelea Rais mstaafu, Daniel arap Moi nyumbani kwake Kabarak, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameweka kambi katika Jimbo la Mombasa.

 

SIASA

KABLA ya kumtembelea Rais mstaafu, Daniel arap Moi nyumbani kwake Kabarak, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameweka kambi katika Jimbo la Mombasa.

Duru za kuaminika zinasema Rais Uhuru anapanga mabadiliko makubwa katika serikali yake.

Wiki mbili zilizopita, Rais huyo alifanya mabadiliko madogo lakini sasa inaonekana anapania kuleta mabadiliko yatakayowanyima nafasi ya kuhudumu baadhi ya mawaziri.

Lengo la Rais Uhuru ni kuingiza watu wanaoweza kumsaidia katika kutekeleza ajenda zake nne za maendeleo ili atakapoondoka madarakani 2022, ataacha nchi iliyopiga hatua katika uongozi wake.

Katika mabadiliko hayo, mawaziri wanne wanaweza kupoteza nyadhifa zao. Wizara zitakazoathirika na mabadiliko hayo zimekuwa zikikabiliwa na sakata mbalimbali zikiwamo za uvujaji wa pesa na uagizaji wa bidhaa duni.

Wizara ya Kilimo ambayo waziri wake ni Mwangi Kiunjuri imetuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha zilizotegwa kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa zao hilo. Badala ya kununua nafaka hiyo kutoka kwa wakulima, wizara hiyo iliwapa wafanyabiashara mabwanyenye fursa ya kuagiza mahindi na kuyauzia Halmashauri ya Taifa ya Nafaka (NCPB).

Waziri Kiunjuri alifikishwa mbele ya kamati ya Bunge kuhusu masuala ya kilimo na kuhojiwa. Waziri huyo aliahidi kuwa wakulima wangelipwa lakini hadi sasa, hawajalipwa wala mahindi yao kununuliwa.

Waziri wa Afya, Cecilly Kariuki alikuwa waziri wa Ugatuzi na maendeleo ya vijana wakati mabilioni ya fedha yalipoporwa. Takriban Sh7.5 bilioni zilipotea katika zabuni bandia. Wasimamizi wakuu katika huduma kwa vijana tayari wana kesi mahakamani.

Pia, kuna Waziri Adan Mohammed ambaye kabla ya kupelekwa katika Wizara ya Muungano wa Afrika Mashariki, alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Mohammed aliondolewa kwenye wizara hiyo kutokana na sakata la sukari yenye chembe za madini ya zebaki iliyoagizwa mwaka 2017.

 

Ulipaji kodi

Baadhi ya waigizaji hawakulipa kodi ilhali muda uliotolewa kwa kampuni hizo kuagiza bidhaa hiyo bila malipo ya kodi ulikuwa umeisha.

Waziri wa Fedha, Henry Rotich pia yuko shakani kwa kutoa kibali kwa mabwanyenye kuagiza sukari.

Pia, yeye amefikishwa mbele ya kamati ya Bunge kujibu tuhuma za kukiuka sheria.

Waziri wa Usalama, Fred Matiangí anajulikana kwa kufanya kazi yake kwa bidi lakini, hayo yote mazuri yanaweza kusahaulika. Kisa? Alipokuwa Waziri wa Elimu, Matiang’i alikuwa miongoni mwa maofisa wa juu serikalini kusaini stakabadhi zilizowezesha bwanyenye Francis Mburu kulipwa TSh3.7 bilioni.

Mburu alikuwa ameiandikia Tume ya Ardhi akitaka serikali kumlipa ardhi yake ambayo ilichukuliwa na serikali. Shule mbili za umma zilijengwa kwenye ardhi hiyo bila mmiliki huyo kulipwa lakini Waziri wa sasa wa Elimu Amina Mohammed anasema Matiang’i anafaa kulaumiwa kwa kutoa amri kwamba Mburu alipwe ilhali ardhi ambayo shule hizo zinakalia ni ya serikali wala si ya mtu binafsi.

Je, Matiang’i atabaki?

Waziri mwingine ambaye anatetemeka kwa hofu ya kupigwa teke katika mabadiliko hayo ni Waziri wa Nishati, Charles Keter. Wizara hii imekumbwa na sakata nyingi za bili za juu ambazo baada ya kuchunguzwa iligunduliwa kwamba kulikuwa na uhalifu wa kupora fedha za wateja.

Muda mfupi baadaye, sakata nyingine iligonga mlango. Zabuni nyingi zilitolewa kwa ujanja ili kufaidi watu fulani katika wizara hiyo. Jumla ya maofisa 20 wa ngazi za juu walinaswa wiki mbili zilizopita na kufikishwa kizimbani. Je, Keter ataponea chupuchupu ama chuma chake ki motoni?

Kisa cha hivi karibuni cha faru sita weusi kufa katika hali ya kutatanisha baada ya kuhamishiwa mbuga ya Tsavo, kileta taharuki kwa wakenya wengi.

Waziri wa Utalii, Najib Balala aliwafuta kazi maofisa wakuu wa shirika la uhifadhi wa wanyama wa pori, lakini, hatua hiyo huenda haitatosha. Balala yuko hatarini kupoteza nafasi yake kwenye mabadiliko ya mawaziri yanayotarajiwa kufanyika.

Awali duru zilisema mawaziri wengine watahamishwa.

Ziliongeza kuwa mbali na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kutakuwa na mabadiliko katika usimamizi wa mashirika ya serikali.

Zilisema mabadiliko hayo yanahusiana na ajenda nne kuu za Rais Uhuru ambazo ni utengenezaji wa bidhaa, nyumba, chakula cha kutosha na afya kwa wote – na azimio lake la kupambana na ufisadi.

Kutimizwa kwa ajenda hizo nne ni muhimu kwa nchi na Rais Uhuru na kwa hivyo kiongozi huyo anataka kufanya kila awezalo kuhakikisha mipango yake inaenda vizuri.

 

Ruto na ndoto za urais

Huku Rais Uhuru akiwa ameangazia ajenda hizo, Naibu Rais William Ruto ameweka macho yake kwenye mchakato wa kumrithi.

Bila shaka ndoto za Ruto zitategemea utekelezwaji wa ajenda hizi. Waziri mmoja ambaye analengwa katika mabadiliko yanayotarajiwa alikuwa anataka kujiuzulu lakini washauri wake wakabadilisha mawazo yake.

Wengi wanahisi Rais atafanya mabadiliko wakati wowote kuanzia sasa. Hata hivyo, Jumatatu Ikulu kupitia msemaji wake Bi Kanze Dena, ilikanusha madai hayo.

“Anataka kuwatumikia Wakenya akiwa na viongozi wengine wanaotaka kumsaidia kufikia malengo yake,” anasema mwanasiasa ambaye hakutaka kutajwa jina.

Aliongeza kuwa mawaziri waliokuwa wameachwa wakati Rais Uhuru alipounda Baraza la Mawaziri baada ya kutawazwa 2017, wanaweza kupoteza nyadhifa zao katika wizara mbalimbali. Uteuzi uliendelea hadi Januari 2018.

Ingawa Rais aliwapa nafasi kuhudumu kwa mara ya pili katika baraza lake la mawaziri, mawaziri hao bado wanazembea kazini.

Uamuzi wa Rais kuandika mwenyewe kwa mwandiko wake kwenye karatasi, lengo ni kuzuia taarifa hizo kuvuja na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Rais yuko katika pilikapilika za kujenga madaraja ya ushirikiano katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Baada ya kuchaguliwa kwa mara ya pili, Rais Uhuru amebadilisha mtindo wa ufanyaji kazi. Katika muhula huu wa pili, ameacha kutafuta ushauri kutoka kwa washauri wake wa karibu anapotaka kutangaza masuala makuu.

Baraza la Mawaziri la muhula wake wa kwanza halikuwa uamuzi wake mwenyewe.

Rais amesisitiza kuwa vita vyake dhidi ya ufisadi havitazamishwa na yeyote.

Ujumbe huu wa kiongozi wa taifa ulienezewa kwa kuungwa mkono na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ambaye ameahidi kushirikiana na Rais hadi ufisadi upunguzwe kabisa.

Baada ya salamu zilizovuruga amani katika chama tawala cha Jubilee, siku hizi kuna mvumo ama mwangwi katika matamshi yao.

Viongozi hao siku hizi huzungumza kwa sauti moja. Akizungumza wiki jana katika eneo la Nyanza, Raila alisema vita dhidi ya mafisadi vitaendelea hadi wezi wote waadhibiwe.

Hata hivyo, Jumatano, Bw Odinga chama cha ODM kimetuma taarifa kwa vyombo vya habari ikivitaka kuwajibika na kuacha kupotosha Wakenya.

"Nilisoma juzi habari zisizo na msingi kwamba Rais Kenyatta na mimi tunataka kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri. Ni uvumi usio na msingi," taarifa ya ODM iliotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Philip Etale, imemnukuu Bw Odinga.

Aliongeza kwamba licha ya baadhi ya viongozi kusema vita hivyo vinalenga watu fulani, hakuna atakayeweza kuweka vikwazo katika juhudi hizo.

Wakenya wana matumaini mengi katika harakati za Rais na Raila kuleta mwamko mpya nchini.

Je, watafanikiwa ama wanachezea shere wananchi?