Maziwa yanayopotea Rungwe yatuzindue

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, August 9   2017 at  09:37

Kwa Mukhtasari

Moja ya habari tulizokuwa nazo katika gazeti letu la Mwananchi toleo la Jumanne, Agosti 8, 2017 ni ile iliyokuwa ikielezea ukosefu wa soko la maziwa katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kusabibisha lita 53 milioni kati ya 62 milioni zinazozalishwa kwa mwaka kupotea.

 

MOJA ya habari tulizokuwa nazo katika gazeti letu la Mwananchi toleo la Jumanne, Agosti 8, 2017 ni ile iliyokuwa ikielezea ukosefu wa soko la maziwa katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kusabibisha lita 53 milioni kati ya 62 milioni zinazozalishwa kwa mwaka kupotea.

Akizungumza katika kikao cha Maofisa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi na pia wadau wengine  wa maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chalya Nyangindu alisema kwa takwimu  hizo, lita 206,000 zinapotea kwa siku kati ya lita 236,000 zinazozalishwa.

Mei 29, 2017 Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya uhamasishaji wa unywaji wa maziwa  yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Kyakailabwa, mkoani Kagera aliwataka Watanzania kunywa maziwa kwa wingi ili kuboresha afya zao na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema lengo la wiki hiyo ni kuongeza kiasi cha unywaji maziwa nchini kutoka lita 47 kwa mtu kwa mwaka hadi 200 kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Matukio haya ni kielelezo tosha kwamba Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB)  ina mlima mrefu  wa kukwea na ili kufikia malengo ya kuundwa kwake. Imeundwa na Sheria ya Tasnia ya Maziwa, Sura 262 na kukabidhiwa wajibu wa kusimamia, kuratibu, na kuendeleza tasnia ya maziwa. Pia ina jukumu la kuhamasisha na kuwawezeshha wadau katika shughuli za uzalishaji, ukusanyaji  maziwa usindikaji, kuboresha masoko na unywaji wa maziwa na bidhaa zake.

Inaelezwa kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili katika bara la Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe ambayo ni zaidi ya milioni 21.3. Nchi ya kwanza kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe ni Sudan.

Pamoja na ukweli huo Tanzania haijapata mafanikio makubwa ya kiuchumi kutokana  na kutowekeza kikamilifu katika biashara ya maziwa licha ya kwamba kwenye maziwa kunapatikana bidhaa nyingi kama vile maziwa fresh, mtindi, samli, siagi na jibini za aina mbalimbali.

Kwa sababu hizo tunadhani kwamba wakati umefika kwa wadau wa bidhaa hii kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Ili kuleta mageuzi ya kweli tunashauri mambo matatu yazingatiwe na kufanyiwa kazi  kwa umakini mkubwa wa kimkakati.

Jambo la kwanza ni uhifadhi wa maziwa.

Tunaamini kwamba  kama wafugaji watahamasishwa kununua  au hata kukopeshwa vifaa bora vya kuhifadhia maziwa kwa muda mrefu, kilio cha kupoteza kiasi cha maziwa kama kilivyoripotiwa huko Rungwe kitamalizika hivyo kuokoa mamilioni hayo ya fedha.

Jambo la pili ni kutafuta masoko.

Baada ya kuhifadhi, wafugaji wanahitaji kupata masoko ya uhakika ili waendelee kuzalisha zaidi  hasa kwa kuwa watakuwa na uhakika wa kipato.

Hiyo ndiyo njia ya mkato ya kukuza uchumi na kuongeza tija.

Wakiona maziwa yanalipa nchini  ambavyo tumesikia baadhi wakilalamikia uhaba wa bidhaa hiyo watapambana kwa hali na mali kuhakikisha mifugo yao inakuwa katika hali nzuri, inatoa maziwa mengi na yaliyo bora.

Viko viwanda vya kuchakata maziwa nchini ambavyo tumesikia  baadhi vikilalamikia uhaba wa bidhaa hiyo, jambo  linalotupa picha kwamba kuna tatizo la mawasiliano ambalo linatupeleka  kwenye jambo la tatu linalotakiwa kufanyiwa kazi kimkakati.

Jambo hili linawahusu wafugaji na watumiaji wote  wanahitaji elimu.

Wakati wafugaji wanahitaji maarifa ya uzalishaji bora  na mbinu za masoko  ikiwamo kujitangaza, watumiaji wanatakiwa kuelimishwa juu ya umuhimu wa maziwa  katika mwili wa binadamu na jinsi bidhaa  hiyo inavyoweza kutumika  katika mambo mbalimbali yenye manufaa kijamii na kiuchumi. Hii ni fursa tuichangamkie.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.