http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759262/medRes/2109624/-/u0btydz/-/kirisasa.jpg

 

Mbinu ya kisasa katika upanzi wa miche

Samuel Kinyua

Bw Samuel Kinyua (kulia), mkulima wa nyanya na mboga Juja, kaunti ya Kiambu akieleza kuhusu mfumo mpya wa kitalu, aina ya trei, unaotumika kukuza miche. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  13:48

Kwa Muhtasari

Miche ni mimea michanga itokanayo baada ya kupanda mbegu kwenye kitalu.

 

KUNA mimea aina mbalimbali inayohitaji miche, mfano; nyanya, mboga za kienyeji kama mnavu na mchicha, spinachi, kabichi, sukuma wiki, miti, matunda, miongoni mwa zingine.

Kuna vitalu kadha wa kadha katika upanzi wa miche.

Hata hivyo, kinachojulikana zaidi kwa wanazaraa ni kile cha kuandaa shamba, sehemu inayonuiwa kuinuliwa juu kiasi, mitaro ikaandaliwa kisha mbegu zikapandwa.

Bw Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo anasema mbinu hiyo inahitaji mchanga uwe mwororo. “Miche huhitaji mchanga mwororo kwa kuwa ni mmea mdogo, unaotaka matunzo ya hali ya juu,” ashauri.

Mfumo mwingine ni wa vitalu vya trei vyenye mashimo madogo madogo. Bw Samuel Kinyua ambaye ni mkulima wa nyanya Juja, Kiambu anasema hiyo ni mbinu bora ya kisasa katika upanzi na utunzaji wa miche.

Umbo la vitalu hivyo ni sawa na trei za mayai, vyenye vijishimo vidogo vidogo. Mkulima huyo anadokeza kuwa trei moja husitiri idadi ya miche 150. “Trei hutiwa mchanga mwororo uliochanganywa na mbolea kisha mbegu zinapandwa,” asema Bw Kinyua.

Aidha, trei hizo huandaliwa sehemu maalum sawa na hema (Greenhouse), ambapo huendelea kutunzwa kwa kunyunyuziwa maji.

“Ekari moja inahitaji trei 67, na miche inapochipuka hutunzwa kwa mbolea ya kisasa kama CAN au Urea, pamoja na kupuliziwa dawa za magonjwa na wadudu,” afafanua.

Kudhibiti maadui

Mtaalamu Mwenda anasema mfumo huo huchukuliwa bora kwa kuwa, maadui wa mimea kama vile ndege huweza kudhibitiwa.

“Vitalu hivyo vinaweza kuwekwa nje ya makazi ya mkulima, na itakuwa rahisi kuvitunza na kukabiliana na adui wa miche,” aeleza.

Bw Kinyua anasema tangu mfumo wa trei kuwa kitalu uvumbuliwe, imekuwa rahisi kufanya kilimo kwa sababu miche inayoharibika ni chache mno ikilinganishwa na mbinu ya kuzipanda shambani. Anaongeza kuwa trei zimewezesha mkulima kuipa miche matunzo ya kipekee. “Wakati wa kuing'oa kuihamishia shambani inakuwa rahisi,” aeleza.

Mkulima huyo anasisitiza kwamba uhamishaji wa miche shambani ufanyike majira ya jioni, au asubuhi wakati miale ya jua haijaongeza ukali wake.

“Miale kali ya jua huifisha. Miche iwapo tayari imwagiliwe maji saa kadha kabla ya kuing'oa. Ing'olewapo iwe na mchanga kiasi wa kuendelea kuipa uhai,” anashauri.