http://www.swahilihub.com/image/view/-/4883342/medRes/2190166/-/n82bifz/-/matudaa.jpg

 

Mbinu za kuitunza miche

Stevene Mwanzia

Bw Stevene Mwanzia, mmoja wa kundi la vijana wamiliki wa kampuni ya kilimo ya Sun Berry Berry Enterprise inayokuza matunda aina ya bukini Kiambu, akionesha miche inavyotunzwa. Picha/ SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  08:27

Kwa Muhtasari

Zipo njia mbalimbali za kuitunza miche.

 

KUNA vitalu vya aina mbalimbali katika upanzi wa miche, ambayo ni mimea midogo itokanayo baada ya kupanda mbegu.

Matunda, baadhi ya mboga, miti, nyanya, vitunguu, ni miongoni mwa mimea inayohitaji miche ili kuipanda.

Kitalu kinachojulikana zaidi kwa wakulima ni kile cha mchanga kuinuliwa juu kiasi, mitaro inaandaliwa kisha mbegu zinapandwa katika eneo tambarare. Aina hii inahitaji mchanga uwe mwororo kwa kuwa mche ni mmea mdogo, unaotaka matunzo ya hali ya juu. Huundiwa kibanda mithili ya mwavuli, kilichoezekwa kwa nyasi zilizokauka au magunia.

Kuna kitalu cha kutumia vitunzio vya bilauri za plastiki, hasa zinazotumiwa na wachuuzi wa kahawa.

Mbegu hupandwa kwenye glesi hicho. Mfumo mwingine ni ule wa kisasa, wa vitalu vya trei vyenye mashimo madogo madogo. Wakulima ambao wametumia mfumo huu kupata miche, wanasema ndio mbinu bora zaidi katika upanzi na utunzaji wa mimea hii michanga.

Umbo la vitalu vyake ni sawa na trei za mayai, yenye vijishimo vidogo vidogo. Aidha, trei moja husitiri idadi ya miche 150 na vijishimo vyake hutiwa mchanga mwororo uliochanganywa na mbolea kisha mbegu zinapandwa moja kwa moja.

Miche ni mimea inayohitaji matunzo ya hadhi ya juu, kwa sababu ya adui kama mifugo, nyuni, wadudu na hata miale kali ya jua inayosababisha mnyauko wa maji. Edwin Njiru ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo anasema utumizi wa vifungulio vidogo ndiyo njia bora dhidi ya adui ya mimea hii.

Vifungulio kwa Kiingereza ni Greenhouse.

Huu ni mfumo wa kisasa katika kilimo chini ya mahema maalumu. Baadhi ya wanazaraa wamekumbatia mfumo huu kukuza nyanya, pilipili mboga, giligilani, spinachi, na mimea inayokua kwa muda mfupi.

Bw Njiru hata hivyo, anasema kuna mahema maalumu yanayotumika kuzuia miche dhidi ya kushambuliwa na adui.

“Vyandarua vya kuzuia mbu ni mojawapo ya vinavyotumika kuunda vifungulio vidogo vya kutunza miche,” anadokeza mtaalamu huyu.

Mbali na kuzuia wadudu wanaopeperushwa na upepo na wanyama, Njiru anasema miche inapokuzwa chini ya vifungulio vya aina hii makali ya miale ya jua yanadhibitiwa, kwa kuwa vyandarua hivi vina mashimo madogo. Steven Mwanzia ni mmoja wa wakulima chini ya kundi la vijana wanaomiliki kampuni ya kilimo ya Sun Berry Berry Enterprise inayokuza matunda aina ya bukini Kiambu, na anasema wameweza kuepuka hasara zinazosababishwa na wadudu, wanyama, na jua kwa kutumia vifungulio vya vyandarua.

“Kazi tunayofanya ni kunyunyuzia miche maji pekee, adui wa mimea hii hudhibitiwa na vifungulio tunvayoitunzia,” anaeleza.

Sun Berry Berry Enterprise hukuza bukini katika shamba lenye ukubwa wa ekari 20 Kiambu, na idadi sawa na hiyo kaunti ya Nakuru. Kwenye mahojiano, Bw Mwanzia alisema kwa kutumia vifungulio kutunza miche zaidi ya asilimia 95 hufanikiwa kustawi.

Kauli yake inatiwa muhuri na mtaalamu Njiru, akieleza kwamba wakulima wanaotumia mfumo huu wamefanikiwa kupata miche isiyo na dosari. Mwanzia hutumia vitalu vya bilauri, anazopanda mbegu baada ya kutia mchanga mwororo uliochanganywa na mbolea ya mifugo au kuku.

Ameunda vifungulio kadha kwa vyandarua vya mbu, ambavyo hutumia kuendesha shughuli za utunzaji wa miche. Changamoto ibuka ni namna ya kupata vyandarua vya kutosha, kwa kuwa vipya madukani ni ghali mno.

Vinapocharazwa na miale ya jua sana huwa katika hatari ya kuraruka pamoja na kuoza kwa ajili ya unyevunyevu hasa wakati kuna mvua nyingi.