http://www.swahilihub.com/image/view/-/3212850/medRes/1332116/-/3m13haz/-/michuki.jpg

 

Jinsi Michuki alinusuru Mbio za Nyika Mombasa kutibuka mwaka 2007

John Michuki

Marehemu John Michuki. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  14:16

Kwa Muhtasari

Wakenya wengi hawana habari kuwa mbio za nyika za kimataifa ambazo ziliandaliwa katika mji wa Mombasa Februari 24, 2007, nusura zitibuke lau sio ukali na msimamo thabiti wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, marehemu John Njoroge Michuki.

 

WAKENYA wengi hawana habari kuwa mbio za nyika za kimataifa ambazo ziliandaliwa katika mji wa Mombasa Februari 24, 2007, nusura zitibuke lau sio ukali na msimamo thabiti wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, marehemu John Njoroge Michuki.

Mbio hizo ambazo hatimaye ziliandaliwa katika uwanja wa gofu wa Mombasa ziliishia kufanyika licha ya upinzani mkali kutoka kwa kundi la Mombasa Republican Council (MRC) ambalo lilundwa mwaka wa 1999 likiwa na ajenda ya kutenga Mji huo kutoka Kenya.

Mashindano manne ndiyo yalikuwa yameratibiwa, yakihusisha timu za wanariadha wa kiume, wa kike, chipukizi pia wa jinsia hizo mbili.

Wanariadha 470 katika makala hayo ya 35 walijumuika katika mataifa 63.

Sasa, Michuki ndiye alipewa jukumu hilo la kushirikisha mikakati ya kufanikiwa kuandaliwa kwa hafla hiyo ya umuhimu sana kwa pato la kitaifa na kuweka Kenya katika ramani ya kimataifa kama nchi ambalo lingeweza kuhifadhi wageni hao wote.

Kundi hilo la MRC lilitoa makataa kuwa halingekubali makala hayo yaandaliwe Mombasa kwa kuwa si Kenya, na cha pili, serikali ilikuwa ikiwadhulumu watu wa Pwani kupitia misako na mauaji ya washukiwa wa ugaidi.

Walishikilia kuwa harakati hizo zilikuwa zikiendeshwa kwa njia ya kuwabagua watu wa Pwani na kuwajumuisha katika kapu moja la ugaidi na kisha washukiwa kuishia kupatikana wameuawa kinyama.

Ikawa ni MRC dhidi ya Michuki.

Michuki akiwa waziri wa kufuata mikakati ya utaratibu wa utendakazi aliwasiliana na aliyekuwa kamanda wa polisi wa Mombasa, King’ori Mwangi akimtaka awe akimpa ripoti za maandalizi ya hafla hiyo.

Kabla ya wiki moja siku ya siku ifike na wanariadha wangojewe kwa uwanja kumenyana, Mwangi hakuwa ameandaa ripoti ya uhakika kuwa hali ilikuwa shwari.

Ndipo Michuki bila arifa yoyote kwa Mwangi aliamua kuingia Mombasa na afisini mwa kamanda huyo.

Mwangi hupenda sigara sana na alikuwa tu amemaliza kuvuta moja ndani ya afisi yake wakati Michuki alitua ndani ya afisi hiyo akiandamana na wasaidizi wake wanne na walinzi sita.

Pia, anayekwandalia makala haya alikuwa katika ziara hiyo ya ghafla akiwakilisha masilahi ya kuwajulisha Wakenya.

Michuki hakuzingatia sana moshi uliokuwa ukiyeyuka ndani ya afisi hiyo na hata hakuonyesha kukerwa na hali ya afisa wa polisi kugeuza afisi yake kuwa ya uraibu huo, bora kazi ilikuwa ifanyike.

Kimya hapa na pale huku Bw Mwangi akionekana kuchanganyikiwa, Michuki akamuuliza: “Bw King’ori wa Mwangi, unajua nini kimenileta hapa?”

Jua kuwa maongezi hayo yalikuwa kwa lugha ya Gikuyu.

Bw Mwangi: “Ndio najua.”

Ni nadra sana waziri akutembelee afisini mwako ukiwa wa ngazi ya chini katika ajira ya serikali na ukiri kuwa huna habari ya ziara hiyo.

Hata ikiwa huna habari na kwa uhakika hujui, sema unajua na ukiulizwa uelezee sababu hiyo, wewe jibu kuwa “kama afisa wa serikali wa ngazi ya juu na mmoja wa viungo vya kiserikali una kila haki ya kuzuru hapa kwa lolote na kwa wakati wowote.”

Kwa wakati huu, Bw Mwangi alikuwa amefanikiwa kutuma arafa kwa maafisa wengine ambao walizingira makao makuu hayo ya polisi kuonyesha kulikuwa na mgeni mheshimiwa wa kulindwa rasmi.

Michuki: Ningetaka kujua umefika wapi na maandalizi kuhusu hizi mbio za nyika ambazo ni lazima zifanyike kwa kuwa msimamo wa serikali ni kuwa ni lazima zifanyike.

Mwangi: Kwa uhakika nimekuwa nikijadiliana na wazee wa vijiji ili… (Michuki akamkatiza kwa ukali wa kipekee).

Michuki: Unataka kuniambia kuwa wewe umegeuka kuwa ombaomba wa ruhusa kutoka kwa mabaraza ya wazee ili uwe na uwezo wa kutekeleza sera ya serikali?

Mwangi: Hapana.

Michuki: Mimi nimekuja hapa uniambie kuhusu changamoto zako ni gani za kulemewa kushirikisha hafla hiyo kufanyika hapa Mombasa kama ilivyoratibiwa. Serikali haiwezi kuwa ya kuomba ruhusa kutoka kwa makundi yasiyotambulika kisheria.

Mwangi: Yes Sir.

Michuki: Narudi Nairobi. Kabla nifike huko, uwe umetuma ripoti ya ukadiriaji wako wa hali, unahitaji kuungwa mkono kivipi, idadi ya maafisa unataka na vifaa vya kuhakikisha hafla hiyo imefanyika. Na katika ripoti hiyo nisipate mahali unapoomba ruhusa ya wazee wa kijiji. Wewe ndiye kuwaambia wazee hao hafla hiyo itafanyika wapi, saa ngapi kwa niaba ya serikali.

Mwangi: Yes Sir!

Michuki: Wewe King’ori Mwangi ni Mkikuyu?

Mwangi: Yes Sir.

Michuki: Unajua kuhusu msemo wa Agikuyu unaosema Ibilisi ataingiwa na kiburi cha maringo akifanyiwa nini?

Mwangi: Akichinjiwa.

Michuki: Hiyo ripoti yako niipate Nairobi.

Usafiri wa ndege kutoka Mombasa hadi Nairobi utakuchukuwa dakika 45 zikizidi sana.

Saa 12 jioni Michuki alikuwa katika afisi yake na Mwangi alikuwa ametuma hiyo ripoti.

Ilikuwa imeomba maafisa wa kupambana na ghasia, magari ya kuwasafirisha, vitoa machozi, mipini na vifaa vingine vya kutwanga watu.

Asubuhi iliyofuatia, alipata usaidizi huo na kazi ikaanza Mombasa.

Kuona cha mtema kuni

Wale wazee ambao walikuwa na mazoea ya kutoa makataa na kutisha kuwa wangevuruga hafla hiyo, pamoja na vijana wa MRC walikipata.

Vita katika kila pembe ya ngome za MRC, wakiandamana wanatimuliwa, wakijaribju kuwasiliana na Mwangi wanaambiwa siku za kuombwa washirikiane zilikuwa zimeisha.

Seli za Polisi Mombasa zikawa na mamia ya washukiwa wa pingamizi hizo, kilio katika kila ngome ya ukaidi.

Siku iliyofuatia, wazee hao wa kijiji waliandaa kikao na waandishi wa habari wakisema kuwa walikuwa wakiunga mkono kikamilifu hafla hiyo kuandaliwa Mombasa na wakaahidi kuiunga mkono kwa dhati na bila masharti kwa msingi kuwa ilikuwa ya manufaa halisi kwa Mji wao, maisha yao na taifa lao.

Michuki akiwa Nairobi alitabasamu na akamwambia aliyekuwa msaidizi wake, George Natembeya ambaye leo hii ni Kamishna wa Kaunti ya Narok: “Ukichinjia Ibilisi, atakuduwaza na maringo na kiburi.”

Hafla ikaandaliwa na Kenya ikawika, yote kwa kuwa Michuki alinusuru hali kupitia mtindo wake wa utendakazi wa “masihara kando, kazi kwanza”.