http://www.swahilihub.com/image/view/-/2539202/medRes/887146/-/la74wh/-/mizani_haki.jpg

 

Mchwa katika halmashauri washughulikiwe

Mizani ya haki

Mizani ya haki. Picha/MTANDAO 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  10:51

Kwa Muhtasari

Katika kipindi fulani miaka iliyopita ilionekana kuwa fedha za umma ni ujanja.

 

KATIKA kipindi fulani miaka iliyopita ilionekana kuwa fedha za umma ni ujanja.

Ijapokuwa walijulikana wahusika, waliishia kutajwa kuwa ni mchwa tu ambao dawa yao ilikuwa jikoni.

Kwa bahati mbaya sana jamii haikuwahi kuelezwa ingechukua muda gani kupatikana kwa dawa hiyo ya kuulia mchwa kwenye halmashauri.

Kilichoshuhudiwa ni viongozi wa Serikali walipofanya ziara mikoani na wilayani na kugundua ubadhirifu mkubwa wa mali na fedha za umma pamoja na watendaji wabadhirifu, wezi, wazembe na wasiotekeleza wajibu wao lakini waliishia kulalamika tu.

Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC zilipogundua madudu kwenye halmashauri na mashirika ya umma mchwa hao hawakushughulikiwa.

Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilipoonesha kwa uwazi uzembe, ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya fedha na mali ya umma bado hakuna ufuatiliaji wa kina uliofanyika.

Taifa likabaki la watu walalamishi. Wakati wananchi walilalamika miradi ya maendeleo kukamilika nusunusu au kutokamilika kabisa huku fedha zilizotolewa na Serikali kuu au wafadhili zikiwa zimeisha, viongozi hao nao walilalamika kukithiri kwa mchwa huku wakisema dawa yao iko jikoni.

Hivi sasa tunafurahi kuona kwamba mchwa hao wanashughulikiwa. Fursa za watu kuchota fedha za maendeleo au kuzituma tofauti na malengo yaliyokusudiwa kwa mfano badala ya kuzielekeza kwenye miradi, watendaji wakaamua kugawana posho na sasa Watanzania wanaona kutoshugulikiwa kikamilifu.

Hilo linaonekana kupitia ziara za Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika maeneo mbalimbali ambazo yamekuwa wakiacha ‘vumbi’ kwa viongozi wa umma kuwajibika.

Tangu Januari mwaka huu, baadhi ya vongozi wa umma  wamekuwa na matumbo joto kutokana na kukamatwa na polisi au kuchunguzwa na  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Wako wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na wengine kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Miongoni mwa waliofikishwa Takukuru ni Mkurugenzi Mtendji wa Mamlaka ya Maji  Musoma (Muwasa) ambaye alituhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji wilayaini Bunda.

Mkurugenzi huyo aliponzwa na kuchelewa kutekelezwa kwa mradi wa maji licha ya Serikali kutoa fedha naye akamlipa mkandarasi ziada ya Tsh7 bilioni.

Mwingine alyefikishwa Takukuru ni Meneja wa wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Mara kwa kushindwa kutekeleza ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Serikali ilitoa Tsh600 milioni tangu Aprili 2017 kwa ajili ya ujenzi huo lakini hadi wakati wa ziara ya Waziri Mkuu alikuwa hajafanya chochote.

Februari 2018, akiwa mkoani Mwanza alimsimamisha mwanasheria wa Halmamashauri ya Misungwi kwa kuidhinisha malipo ya Tsh29 milioni kwa kampuni ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Kadhalika akiwa ziarani Mtwara, aliiagiza Takukuru kumtafuta popote alipo aliyekuwa mkurugenzi wa wilaya ya Masasi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Rai yetu ni kwamba jukumu la kushughulikia wanaotumia madaraka yao vibaya lisisubiri viongozi wa juu tu.

Tunashauri wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya na mikoa wafuatilie kwa karibu kabla ya kuwasili kwa viongozi wa juu kufika kwao.

Hata hiyo, tunatoa wito kwamba pamoja kasi ya juu ya utendaji inayoshuhudiwa sasa, haki itendeke na watuhumiwa wapewe fursa ya kujieleza ili wasihukumiwe majukwaani kisiasa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647