Migogoro ya vyama vya siasa imalizwe kwa busara

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  11:22

Kwa Mukhtasari

Gazeti la Mwananchi Jumanne lilikuwa na habari kuhusu mkutano kati ya wabunge wa CUF kujitokeza ndani ya Bunge baada ya mbunge wa Kaliua Magharibi Magdelena Sakaya kuwasilisha majina ya viongozi wapya wa Chama hicho ndani ya chombo hicho.

 

9GAZETI la Mwananchi Jumanne lilikuwa na habari kuhusu mkutano kati ya wabunge wa CUF kujitokeza ndani ya Bunge baada ya mbunge wa Kaliua Magharibi Magdelena Sakaya kuwasilisha majina ya viongozi wapya wa Chama hicho ndani ya chombo hicho.

Kutokana na hatua hiyo, Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson alisoma taarifa ya Spika wa Bunge Job Ndugai ikionyesha safu mpya ya viongozi wa wabunge wa chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbunge wa Mtwara Mjini Maftaha Nachuma anakuwa mwenyekiti wa wabunge wa chama hicho bungeni na katibu ni Rukia Kassim (Viti Maalum) na mnadhimu wao ni Mbunge wa Kinondoni Maulid Mtulia.

Kutangazwa kwa safu hiyo ya uongozi kuliibua kutoka kwa wabunge wengine na Ally Saleh aliomba mwongozo wa Spika akihoji imekuwaje safu hiyo ikitangzwa iliali wabunge wa chama hicho wakiwa zaidi ya 40 mwalifanya uchaguzi wa viongozi wao.

Kwa mujibu wa Ally Saleh katika uchaguzi wao nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi na Riziki Ng’walu ilichukuliwa na mbunge wa Temeke Abdallah Mtolea na kuwa imekuwaje kunakuwa na safu mbili za uongozi wa chama kimoja?

Si nia yetu kuingilia mamlaka ya Bunge wala Spika lakini tunadhani kwa hali ya mgogoro wa CUF ilipofikia kunahitajika utulivu zaidi katika kufanya uamuzi ili pande zote zione kutendewa haki na kusiwe na malalamiko yoyote.

Tunasema hivyo kwa kuzingatia kuwa hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Ofisi ya Bunge kukubali barua ya upande wa mwenyekit wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwavua uanachama wabunge wanane na papo hapo kuwaapisha wengine wanane kama mbadala wao.

Taarifa ya uchaguzi

Kama alivyojibu Naibu Spika wa Bunge, amepokea taarifa ya viongozi kutoka kwa Sakaya lakini hajapokea taarifa ya uchaguzi upande wa kina Ally Saleh juu ya uchaguzi huo. Tunadhani kwa mgogoro ulivyo, uamuzi wowote ungevuta subira na kujiridhosha zaidi na hata kukaa kwa pande zote mbili kwanza kabla ya kufanya lolote.

Tunajua kwamba katika mgogoro uliopo sasa taasisi mbalimbali zimekuwa zikifanya uamuzi kwa kutumia rejea ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye anaitambua kambi ya Profesa Lipumba.

Kutokana na msimamo wa ofisi hiyo ya Msajilli ndio maana hata taasisi nyingine kama wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Tume ya Uchaguzi (NEC) na sasa Bunge vimekuwa vikitumia kigezo hicho cha Ofisi ya Msajili.

Tunajua kuwa kesi kadhaa mahakamani kuhusu mgogoro huo bado hazijamalizika, kwa hiyo tunadhani wakati mwingine ingekuwa vyema pande zote mbili zingelazimika kupatana ili kumaliza mgogoro huo.

Hakuna ubishi kuwa hatua iliyofikia chama hicho kinazidi kuvurugika na hata Sakaya anakiri kuwa katika uchaguzi huo hawakuwashirikisha wenzao wa upande wa Maalim Seif.

Tunatoa wito kwa taasisi za umma kuhakikisha kuwa zinakaa na pande hizo mbili zinazovutana na kumaliza mgogoro huo na kufanya hivyo demokrasia yetu itashamiri na kuwa mfano wa kuigwa kutoka kwa nchi nyingine za Afrika.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647