Mijadala Bunge la bajeti ilenge kumsaidia mwananchi

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, April 4  2017 at  13:10

Kwa Mukhtasari

Mkutano wa Bunge la 11 la Bajeti unaoanza leo mjini Dodoma ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu.

 

MKUTANO wa Bunge la 11 la Bajeti unaoanza leo mjini Dodoma ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu.

Watanzania takriban milioni 50 macho na masikio yao yataanza kufuatilia vikao vya Bunge hivyo kujua mustakabali wao kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kutokana na umuhimu wake, Bunge hilo hudumu kwa miezi miwili hadi miwili na nusu.

Matarajio ya Watanzania ni wabange kutumia muda wao vizuri kuishauri Serikali kutumia fedha za walipa kodi kwa maendeleo endelevu na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa hali ya chini.

Tunafahamu wabunge wameshirikishwa tangu vikao vya kamati na pia wamesafiri maeneo mbalimbali ya nchi kuona maendeleo ya miradi ya Serikali iliyoombewa fedha katika Bunge la Bajeti lililopita.

Hivyo hatutarajii kusikia wabunge wakiingiza siasa pale hoja inapohusu miradi ya kiuchumi.

Wote tunafahamu uelewa wa wabunge kuhusu masuala ya bajeti ni mkubwa sana, hivyo tunatarajia pamoja na kuchangia kwao kwenye mijadala watatumia pia lugha nyepesi inayoeleweka kwa urahisi ili kuwawezesha wananachi kufuatilia kwa ukaribu na kuielewa bajeti.

Tunasema hivi kwa maana moja tu.

Bajeti ni mkataba baina ya Serikali na wananchi.

Kwa maana nyingine Serikali inapeleka bungeni maelezo ya namna watakavyotumia kodi ya wananchi katika kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo.

Hivyo wabunge ni wawakilishi wa wananchi katika kuhoji kwa nia njema ya kinaachowasilishwa na Serikali bungeni.

Kama wabunge hawataweka mkazo kuisimamia Serikali katika matumizi ya fedha, maumivu ya kiuchumi yatarudi kwa wananchi na hata kudhoofisha mapato ya Serikali.

Siyo kazi yetu kuwapangia wabunge hoja za kuzungumza bungeni lakini wafahamu wananchi waliowapa kura za ubunge, walifanya hivyo kwa matarajio ya kuwa na uwakilishi wenye weledi ndani ya combo hicho cha kutunga sheria.

Tunaamini na ndivyo ilivyo kwani hata wabunge wanaotokana na chama tawala hawakuchaguliwa na wananchi ili wawe wasemaji na watetezi wa Serikali. Pia tunatarajia hoja za wapinzani ziwe za kuboresha na kujenga badala ya kukosoa pekee.

Nia yetu ni kuwashauri wabunge wote kutekeleza jukumu lao la msingi la kuisimamia Serikali kutekeleza ahadi zake walizotoa wakati wa kuomba kura kwa wananchi, kuzifanyia kazi kero zao na kuwawezesha Watanzania waishi kwa uhuru, amani na utulivu.

Tunachokiona ni kama siasa zitatawala ndani ya Bunge hili, kuna hatari Serikali ikakosa ushauri wenye kujenga kuhusiana na matumizi ya fedha zinazotokana na kodi ya wananchi.

Tunawasihi wabunge kutumia nia njema ya Serikali kwa kutoa ushauri wa wenye kulijenga Taifa.

Ni imani yetu kwamba mkutano wa Bunge utakuwa na hoja zenye kujenga zaidi na wabunge watakuwa na ushirikiano katika kuwatetea wananchi ambao ndio walipa kodi.

Wabunge wanaolipwa posho na mishahara hutokana na kodi za wananchi.

Watanzania wanatarajia mambo kama vijembe, siasa za matusi na kupotezeana muda kwa kuomba mwongozo wa spika wenye lengo la kuleta malumbano ya kisiasa au kukomoana, havitakuwapo kwenye Bunge hili.

Sote tunatarajia litakuwa Bunge la kujenga Tanzania ya viwanda.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.