http://www.swahilihub.com/image/view/-/4792680/medRes/2131704/-/109x6lmz/-/mapapai.jpg

 

Kilimo: Mipapai na faida za mapapai

Mapapai

Mtaalamu wa maswala ya kilimo Bw Daniel Mwendwa akieleza mapapai yanavyokuzwa. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 5  2018 at  12:36

Kwa Muhtasari

Mapapai ni matunda ambayo ndani yake huwa na nafasi wazi na kokwa nyeusi.

 

MAPAPAI ni aina ya matunda yasiyo na asidi yakilinganishwa na machungwa, hivyo basi walio na shida ya asidi hupenda kuyala.

Maeneo yanayojulikana kukuza mipapai kwa wingi ni Nyeri, Embu, Meru na Kirinyaga.

Hata hivyo, imeibuka kuwa eneo la Thika lina mchanga na hali ya anga bora kustawisha mipapai.

Katika kijiji cha Munyu kata ya Gatuanyaga kuna mkulima mmoja ambaye amethibitisha haya kwa kufanya majaribio.

Eneo hilo ni tambarare linalokuzwa nafaka aina ya mahindi na maharagwe kwa wingi.

Pia lina maeneo ambayo ni machimbo ya mawe ya ujenzi, na kuna waliowekeza kwenye nyumba za kukodisha.

Bw Harrison Kinyanjui Mbachia anafanya kitu tofauti kabisa na mkondo uliochukuliwa na wakazi wengi.

Shamba lake lenye ukubwa wa ekari tano, ekari moja ameligeuza kuwa ugani wa zaraa ya mapapai.

Thika iko katika kaunti ya Kiambu na ni wakulima wachache mno wanaofanya kilimo cha matunda haya.

Kinyanjui ambaye ni mfanyabiashara, anasema awali shamba lake lilishamiri vichaka lakini kupitia mtaalamu wa kilimo alivalia njuga ukuzaji wa mapapai ambao hajutii.

“Nilianza kilimo cha mapapai 2017, na kwa hakika nimeona matunda yake,” anasema Bw Kinyanjui.

Ingawa kufanya uamuzi huo ilikuwa vigumu kushawishi nafsi yake, anasema kufikia sasa hata kwa dawa akielezwa akuze mimea mingine hataitikia.

Mkulima huyu anafichua ilimgharimu mtaji wa Sh180,000 kuanzisha zaraa hiyo.

Mtaalamu na mshauri wa maswala ya kilimo Bw Daniel Mwendwa alimfaa pakubwa kwa kumuelekeza aina ya mipapai bora kukuza. Mwendwa anasema mapapai hukua katika mchanga mwekundu na vilevile kwenye udongo.

“Mipapai aina ya Solo-Sunrise Hybrid ndiyo bora kwa anayenuwia kupanda matunda hayo,” anaeleza Mwendwa.

La kutia moyo kwa kilimo chake ni kwamba hakina gharama ya kuitunza pindi inapopandwa. Mtaalamu huyu anasema miche ya mapapai huchukua muda wa miezi miwili na nusu kwenye kitalu.

Mbegu za kiume na kike ni jambo la kuzingatia kulingana na Mwendwa, na kwamba asilimia 95-98 inafaa kuwa kike huku iliyosalia iwe ya kiume.

Anasema mbegu au kokwa za mipapai huuzwa kulingana na jinsia.

Utaratibu wa upanzi

Miche ikikaribia kuwa tayari, mkulima anashauriwa aanze maandalizi ya shamba.

“Shimo moja hadi jingine iwe na nafasi ya mita 2.5, na kutoka laini moja ya shimo hadi nyingine iwe na kipimo sawa na hicho,” anafafanua.

Hata hivyo, urefu wa shimo kuenda chini unategemea aina ya mchanga. Mwendwa anasema mchanga mwekundu unahitaji shimo lenye urefu wa futi moja kwenda chini, na upana wa futi 1.5

Mashimo ya mchanga wa udongo anapendekeza yawe na urefu wa nusu futi kuenda chini na upana wa kipimo sawa na hicho.

Kulingana na mkulima Kinyanjui ni kwamba upanzi wa mipapai hauhitaji mbolea ya kisasa.

“Mchanga uchanganywe na mbolea hai; mifugo au ndege, kisha mashimo yatiwe maji na kupanda miche ya mipapai moja kwa moja,” aelekeza.

Mwendwa anasema miche inayofaa kupandwa ni yenye kimo cha urefu wa futi moja.

Kifuatacho ni kuitunza kwa kunyunyuzia maji, na Kinyanjui hutumia maji ya bwawa. Wakati mipapai inaendelea kukua, Mwendwa anasema nafasi iliyoko kati ya miti ya matunda hayo inaweza kupandwa mimea yenye madini ya Nitrojini.

“Maharagwe yanapopandwa kwenye shamba la mipapai huipa Nitrojini,” anasema.

Mwendwa anasema ni nadra mapapai kuathiriwa na magonjwa wala wadudu. Hata hivyo, magonjwa kama Pawpaw ring virus na Bacterial wilt hushuhudiwa iwapo mkulima hakabiliani na makwekwe shambani. Mdudu aina ya Tiripsi aghalabu ndio huonekana kwa mapaipai.

Mtaalamu huyu anasema Solo-Sunrise Hybrid huwa tayari kuvunwa baada ya miezi sita. Bw Kinyanjui amepanda mipapai 900 kwenye shamba lake, na kwamba mpapai mmoja humpa hadi kilo 40 kwa mwaka. Kilo moja huuzwa wastani wa Sh40.