Mjukuu wa mtunzi wa Malaika naye pia ni mwanamuziki

Brian Kamau Baha

Brian Kamau Baha anayefahamika pia kwa jina la kisanii miongoni mwa mashabiki wake kama Yoda ni msanii chipukizi anayeimba nyimbo aina ya Hip Hop. Picha/MARY WANGARI 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, June 13  2017 at  16:19

Kwa Mukhtasari

Brian Kamau Baha anayefahamika pia kwa jina la kisanii miongoni mwa mashabiki wake kama Yoda ni msanii chipukizi anayeimba nyimbo aina ya Hip Hop.

 

BRIAN Kamau Baha anayefahamika pia kwa jina la kisanii miongoni mwa mashabiki wake kama Yoda ni msanii chipukizi anayeimba nyimbo aina ya Hip Hop.

Msanii huyu mwenye umri wa miaka 29 na mzaliwa wa nne katika familia ya watoto watano amesomea shahada ya Somo la Hesabu katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Aidha, muziki umo katika damu yake maadamu anajivunia kuwa mjukuu wake Charo Baha, mwanamziki mwenye kipaji cha pekee aliyetunga kibao kilichovuma cha ‘Malaika, Nakupenda Malaika’.

Alitutembelea katika ukumbi wetu ambapo alitufahamisha yafuatayo kumhusu;

SWALI: Tufahamishe kwa mukhtasari kukuhusu

JIBU:  Kwa jina ni Brian Baha ambapo nafahamika kwa jina la kisanii kama YODA miongoni mwa mashabiki wangu. YODA kwa maana ya Yielding Optimisti Dreams Only. Nina umri wa miaka 29 na mimi ni mtoto wanne kati ya watoto watano wa mamangu.

SWALI: Uligundua lini una kipaji cha mziki

JIBU: Naweza kusema kuwa nilianza mambo ya mziki tangu nilipoanza kujifahamu vyema. Niligundua kipaji changu nilipokuwa katika shule ya msingi ya Mariakani ambapo nilikuwa nikicheza ngoma katika mashindano ya nyimbo za kiasili.

Vilevile niliendelea vivyo hivyo katika shule ya upili ya Kanunga ambapo niliwaongoza wanafunzi wenzangu hadi kiwango cha kitaifa katika mashindano ya uchezaji ngom,a za kiasili.

Aidha, nilipojiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, niliendelea ana mziki ambapo hata nilianzisha bendi kwa jina Wazo Band.

SWALI: Tueleze historia yako kimasomo.

JIBU: Nilisomea shule ya msingi ya Mariakani na kisha nikajiunga na shule ya Upili ya Wavulana ya Kanunga  ambapo baadaye nilijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton niliposomea shahada ya Hisabati.

SWALI: Ni hatua gani kuu uliyochukua kimziki

JIBU: Ni baada ya kukamilisha elimu ya Chuo Kikuu ambapo niliamua kwenda kivyangu kimziki na kuanzisha YODA Music.

SWALI: Umetoa albamu yoyote?

JIBU: Naam, nimetoa albamu mbili. Ya kwanza inayofahamika kama ‘It’s My Time’ huku albamu ya pili iliyo jikoni na ninayotazamia kuipakua mwanzoni mwa Juni kwa jina ‘Revolution Addict.’

SWALI: Maudhui ya nyimbo zako yanatokana na nini hasa?

JIBU: Mimi huimba kuhusu matukio ya maisha ya kila siku, pamopja na mambo ninayopitia katika maiosha yangu binafsi. Falsafa yangu nikuwa kioo cha jamii.

SWALI: Kando na uimbaji, ni mambo yapi tofauti unayofanya kuhusiana na mziki?

JIBU: Kando na uimbaji mimi hucheza ala za mziki kama vile gita na ngoma.

Vilevile mimi hutunga na kuimba nyimbo zangu.

SWALI: Umewahi kufanya kolabo yoyote iwapo ndio na kina nani?

JIBU: Nimefanya kolabo na wanamziki wa humu nchini kama vile Al faizal, Afrika Giza.

SWALI: Ni wasanii gani wa humu nchini au kimataifa ungependa kufanya kolabo nao?

Ningependa kufanya kolabo na wasanii kama vile Flow Flani, Nafsi Huru na Moh Jay.

SWALI: Ni changamoto gani unazokumbana nazo kama msanii chipukizi?

JIBU: Miongoni mwa chanagmoto kuu ninazokumbana nazo ni kama vile changamoto za kifedha na wakati. Mziki una gharama kubwa kifedha na kiwakati. Aidha kuna ushindani mkuu katika tasnia ya mziki. Kukosa kuchezwa hewani kwenye televisheni na redio ni tatizo lingine kuu maadamu vyombo vya habari ni kana kwamba hupuuza wanamziki chupukizi.

Inakuwa vigumu sana kabla ya kuwa maarufu.

SWALI: Unakabiliaan vipi na changamoto hizi?

JIBU: Mbinu kuu ninayotumia ni kujipigia debe hususan kupitia nembo ya T Shirts, vilevile napigia debe mziki wangu kupitia mitandao ya kijamii mathalan Facebook na Youtube na pia katika tamasha mbalimbali ninazohudhuria.

SWALI: Una shughuli yoyote ya kujikimu kimaisha kando na mziki?

JIBU: Kando na mziki, mimi ni mfanyabiashara vilevile. Ninamiliki maduka mawili moja ya kuuzia nguo (boutique) na nyingine ya kuuzia filamu.

SWALI: Ni nani kielelezo chako maishani na kwasababu gani?

JIBU: Namwenzi mno mwigizaji wa filamu wa Hollywood Denzel Washington kutokana na ubunifu na kipaji chake kinachojitokeza tu kirahisi. Ametoshea vyema katika taaluma yake.

Aidha nawaenzi wasanii wote wa mziki wanaotunga nyimbo zinazofaidi jamii kwa jumla.

SWALI: Unajiona wapi katika muda wa miaka 5 ijayo.

JIBU: Ndoto yangu nikuwa nembo imara katika tasnia ya mziki. Niwe na nembo yangu rasmi ya kurekodi mziki. Vilevile niwe namiliki studio na kituo change binafsi cha kurekodi video.