http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564314/medRes/1974556/-/ievlvj/-/maam.jpg

 

Mkasa wa bwawa la Patel, Kenya inahitaji kujipanga

Bwawa

Mwanamke aenda pahali salama baada ya bwawa la Patel, Solai kubomoka na 'kutapika' maji na matope Mei 11, 2018. Picha/JEFF ANGOTE 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  10:48

Kwa Muhtasari

Kuta za bwawa la Patel, Solai zilipasuka na kusababisha maji na matope kuvuja na kusukumwa kwa kasi iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mali na vifo vya watu 47.

 

KUTA za bwawa la Patel, Solai zilipasuka na kusababisha maji na matope kuvuja na kusukumwa kwa kasi iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mali na vifo vya watu 47.

Bwawa hilo lililoko kaunti ya Nakuru, lilivunja kingo zake mnamo Mei 9 usiku na kusababisha maafa, majeruhi na mamia kuachwa bila makao. Maafisa wa shirika la msalaba mwekundu, kitengo cha majanga nchini (DMU), maafisa wa kikosi cha wanajeshi (KDF) na wale wa shirika la NYS ndio waliendesha shughuli za kuokoa manusura.

Gavana wa Nakuru Lee Kinyajui alikuwa mmoja wa viongozi waliozuru eneo la mkasa huo na kusema bwawa hilo lilisababisha hasara kubwa ya maafa na uharibu wa mali yenye thamani ya mamilioni pesa.

Ibada ya misa kwa walioaga dunia leo, Jumatano inatarajiwa kufanyika katika kanisa la Solai AIC na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto watahudhuria. Hata hivyo, Mshirikishi wa Bonde la Ufa Wanyama Musiambo Jumanne alisema siku maalum ya mazishi ya waliofariki haijapangwa kwa kuwa waathiriwa wanaendelea kushauriana na familia zao.

"Tunaongoja waathiriwa ambao wanaendelea kushauriana na familia zao ili kuwapa heshima za mwisho wapendwa wao," akaeleza wanahabari mtaani Solai.

Alithibitisha kuwa Rais na Naibu Rais ndio wataongoza hafla ya kuwaomboleza wendazao.

Serikali ya kitaifa na ya kaunti ya Nakuru iliahidi kugharamia bili ya mochari, na ya matibabu kwa manusura. Kufikia sasa haijafahamika iwapo walioaga dunia watazikwa pamoja.

Manusura wa mkasa huo wamekuwa wakipokea misaada ya chakula, mavazi, malazi na mengine kupitia shirika la Msalaba Mwekundu na wasamaria wema.

Janga linapotokea, huo ndio wakati idara au sekta zilizotwikwa majukumu ya kukabiliana na majanga nchini hujitokeza na kupeana mwelekeo.

Kisa cha hivi punde ni cha Bwawa la Patel, Solai kaunti ya Nakuru lililovunja kingo zake na kufikia sasa limesababisha maafa ya watu wapatao 47, wengine kuachwa na majeraha na mamia kuachwa bila makao.

Jambo la kushangaza hakuna aliyetiwa nguvuni kutokana na mkasa huo, ila tulichoona ni sekta zinazohusishwa na maswala kama hayo zikinyoosheana kidole cha lawama.

Waziri wa Maji Simon Chelugui siku kadha baada ya janga hilo, alisema bwawa la Solai lilijengwa kinyuma na sheria, na kwamba halina leseni hivyo basi halikuwa halalali.

Hata hivyo, wamiliki wa bwawa hilo walijitokeza wakipuuza madai ya Waziri huyo na kushikilia kuwa ujenzi wake ulipigwa msasa na wahandisi wa serikali na likaruhusiwa kuundwa.

Kaunti ya Tana River kwa sasa ni mahame kutokana na mafuriko yanayoshuhudiwa.

Waziri wa Kawi Charles Keter mnamo Jumanne alitahadharisha kufurika kwa Mto Tana kufikia Ijumaa na kuwataka wanaoishi sehemu za chini karibu na mto huo wahame mara moja.

"Kutokana na hali ya anga kufikia Ijumaa Tana River itakuwa imefurika, wanaoishi chini yake wanatakiwa kuondoka waende maeneo salama," akaeleza waandishi wa habari jijini Nairobi. Mto Tana umekaribiana na Bwawa la Masinga ambalo pia linatarajiwa kufurika kwa muda huo.

Kando na mafuriko, kuna majanga ya njaa, kuporomoka kwa majumba, na mmomonyoko wa udongo. Kwa miaka mingi Kenya imekuwa 'ikikimbia' wakati hasara na maafa yametokea, sekta, wizara, washikadau husika, viongozi wa kisiasa wakijitokeza muda huo kutoa ahadi kukabiliana nayo siku za usoni.
Siku chache baada ya janga kutokea, hayo yote huzikwa katika kaburi la sahau hadi jingine lishuhudiwe ndipo ahadi zingine zisizotimika huahidiwe. Kitengo cha kukabiliana na majanga, Disaster Management Unit (DMU) ndicho kimetwikwa jukumu la kutathmini na kuangazia uwepo majanga nchini. Wiki iliyopita msemaji wa serikali, Eric Kiraithe aliitaka DMU kutambua maeneo yote yaliyo katika hatari ya kukumbwa na majanga.

"Wakazi wa maeneo hayo washauriwe kuondoka, wakisusia waondolewe kwa nguvu," Bw Kiraithe akaagiza DMU na washikadau husika.

Ashakum si matusi, agizo hilo ndio lilitolewa japo utasikia majanga yakitukia, na kuibua utata hasa ni nani wa kulaumiwa? Ni jambo la kuhuzunisha kuona Wakenya wakipoteza nafsi zao ilhali kuna vitengo na taasisi zilizopewa majukumu ya kuangazia uwepo wa majanga.

Shirika la Msalaba Mwekundu chini ya Katibu wake Mkuu Dkt Abbas Gullet kwa hakika linahitaji kongole za dhati, kwa kujitolea mhanga kusaidia manusura wa majanga.

Mara nyingi majanga yanapotokea nchini, Dkt Abbas na kikosi chake huwa ngangari katika maeneo hayo wakiwa radhi kuokoa Wakenya.

Shirika hilo katika mataifa mengine hufadhiliwa na serikali zilizoko mamlakani lakini kulingana na Dkt Abbas ni kuwa mara ya mwisho kufadhiliwa ilikuwa chini ya marais wastaafu Mwai Kibaki na Daniel Arap Moi. Katibu huyo anasema kwa sasa hutegemea misaada kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na wasamaria, ili kusaidia waathiriwa.