http://www.swahilihub.com/image/view/-/3808150/medRes/1559931/-/fwj3nmz/-/makonda.jpg

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar aheshimu sheria zilizopo

Paul Makonda

Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. Februari 10, 2017 alitangaza majina ya watuhumiwa wa dawa za kulevya (65) wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini. Picha/SWAHILIHUB 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  09:47

Kwa Mukhtasari

Tumeshtushwa na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kusitisha mabaraza yote ya ardhi ya kata katika Mkoa wa Dar es Salaam na kesi zote hadi utaratibu wa kupitia upya taaluma za wanasheria waliopo kwenye mabaraza hayo utakapofanyika.

 

TUMESHTUSHWA na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kusitisha mabaraza yote ya ardhi ya kata katika Mkoa wa Dar es Salaam na kesi zote hadi utaratibu wa kupitia upya taaluma za wanasheria waliopo kwenye mabaraza hayo utakapofanyika.

Mbali na kusitisha mabaraza hayo na kesi, aliwaagiza makatibu tawala wote kutembelea mabaraza hayo na wakurugenzi wa halmashauri wampatie wasifu wa Wakuu wa Idara na kazi wanazofanya.

Vilevile aliagiza madalali wa mahamaka kufika ofisini kwake leo Jumanne asubuhi wakiwa na nyaraka za usajili ili wafahamike akisema wako baadhi ambao wanapindisha sheria na taratibu.

Tunafahamu kuwa lengo la Mkuu wa Mkoa ni zuri lakini ieleweke yeye kama mkuu wa mkoa kisheria hana jukumu katika mfumo wa utoaji haki na kwamba mahakama zinatakiwa kuwa huru bila kungiliwa na mamlaka nyingine ya nje.

Tunaposoma nyaraka mbalimbali kuhusu muundo wa mabaraza ya ardhi ya kata tunachelea kusema amekiuka sheria kwani sheria zinaonyesha wazi mabaraza haya yalianzishwa kwa Sheria ya Mabaraza ya Kata ya Mwaka 1985 chini ya sheria namba 7 ili kusaidiia kutatua migogoro ya kijamii inayotokea katika kata husika.

Sheria hiyo iliongezewa nguvu kwa Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 na baadaye Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi ya mwaka 2002 ili pia yaweze kusikiliza mashauri ya ardhi.

Mamlaka ya Baraza la Kata kwa mujibu wa Sheria ya Utatuzi wa Mogogoro ya Ardhi  ya mwaka 2002 ni kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi.

Mamlaka ya Baraza la Ardhi kwa mujibu wa sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi ya mwaka 2002 ni kusikiliza na kutatua  migogoro ya ardhi iliyotokea katika kata husika.

Mabaraza ya Kata ambayo husimamiwa na Wizara ya Nyumba na Ardhi husikiliza mamshauri ya ardhi yenye thamani ya ardhi isiyozidi Sh3 milioni.

Mabaraza haya pamoja na kazi nyingine yanasuluhisha migogoro ya ardhi kwa kufuata mila na desturi za mahali, kanuni za haki  asilia au taratibu ambazo wajumbe wamefundishwa katika mafunzo yao.

Tunafahamu kwamba kuna matatizo katika usuluhishi au utatuzi wa migogoro hiyo ndiyo maana  kuna malalamiko mengi na kesi nyingi mahakamani.

Tunatambua zinahitajika juhudi za ziada za usimamizi, uaminifu na uharaka katika utatuzi wa migogoro hiyo.

Hata hivyo, ufumbuzi wake hauwezi kuwa ni kusimamisha shughuli za mabaraza ya kata ambayo yaliundwa kwa sheria.

Kama kuna tatizo katika muundo wake ni vyema mkuu wa mkoa ambaye yumo katika Serikali ifanye juhudi za kutatua kero mbalimbali tena kwa haraka, akafanya ushawishi uandaliwe mswada wa marekebisho ya sheria ya ardhi kwa kurekebisha mabaraza hayo badala ya kutoa tamko lisilo la kisheria.

Hivi mkuu wa mkoa hana habari kwamba mahakamani kuna kesi nyingi na watu wengi wamekaa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa?

Kama zipo mbona shughuli za mahakama hazisimamishwi hadi wasifu wa mahakimu na majaji upitiwe?

Tunamshauri mkuu wa mkoa na wengineo wawatumie wanasheria waliomo kwenye ofisi zao kupata ushauri ili wasijikute wanaingilia wizara au mihimili mingne au kuzua migongano ya kisheria.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647