http://www.swahilihub.com/image/view/-/2195324/medRes/680645/-/cqfgtd/-/DNMACHAKOS1411o.jpg

 

Mpango wa Gavana Mutua kwa wakazi wa Machakos

Alfred Mutua

Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua. Picha/PHOEBE OKALL 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, May 11  2018 at  10:03

Kwa Muhtasari

Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua ameamua kuwapa wenyeji wa Kaunti hiyo hadhi ya kuhusishwa na umaridadi wa boma.

 

KATIKA jamii, ujirani huwa na njia zake za kutathimini uwezo wa kifamilia hata bila kuandaa harakati za uhasibu.

Njia moja ya ujirani ya kujua aliye katika mstari hatari wa umasikini ni kupitia kupiga msasa ulipaji wa karo kwa watoto, mavazi ya familia, uwepo wa mifugo, afya ya familia, uwezo wa kutoa michango katika umoja wa kijiji na hatimaye hadhi ya nyumba ya makazi.

Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua ameamua kuwapa wenyeji wa Kaunti hiyo hadhi ya kuhusishwa na umaridadi wa boma.

Katika hali hiyo, ametenga kitita cha Sh350 milioni cha kuwawezesha watu wote wa Machakos kama Kaunti kuafikia ubora wa maisha ya kuwa na nyumba zote zikiwa zimeezekwa kwa mabati  kwa zile zote ambazo kwa sasa zimeezekwa kwa nyasi.

“Ni miaka 500 sasa tangu Ulaya kuondolewe nyumba za kuezekwa kwa kutumia nyasi. Ni zaidi ya miaka 50 sasa tangu Kenya ijipe Uhuru wa kujitawala na kujipa mavuno ya matunda ya uhuru. Kwangu Machakos sitaki kuona nyumba ikiwa imeezekwa kwa nyasi katika kipindi cha miezi minne ijayo,” asema Dkt Mutua.

Huyu Mutua ambaye ametangaza ari yake ya kuwania urais 2022 anasema kuwa sio kwa lazima eti wakazi wa Kaunti hiyo wabadilishe paa za nyumba zao na katika kipindi hicho iwe ni makataa ya kujinunulia mabati na kubadilisha.

“Serikali yangu ndiyo itagharamia bajeti hiyo na ambayo tumeitathimin na kuiona ikiwa ya Sh50 milioni. Katika kipindi hicho cha miezi minne, serikali yangu itakuwa imewabadilishia wote walio na nyumba hizo za nyasi maisha na kuwapandisha hadhi kuwa ndani ya mabati,” asema.

Janga la moto

Dkt Mutua anasema kuwa kuna hatari kubwa kuishi katika nyumba za msonge kwa kuwa ni rahisi moto kuteketeza kila kitu ikiwa janga hilo litatokea.

Anasema kuwa katika kipindi cha miezi hiyo minne, hataki kuwa na watalii katika Kaunti ya Machakos wakiingia kufanya utafiti wa jinsi ya kujenga nyumba kwa kutumia nyasi.

Anasema kuwa juhudi hizo hazitakwamia hapo kwa kuwa ametenga kitita kingine cha Sh350 milioni cha kununua transfoma 1,000 za stima ili kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Kaunti ya Machakos anaishi katika nyumba iliyo na stima.

“Kwa hivyo, ni suala la kungoja kidogo tu upate kila mkazi wa Machakos anaafikia nyumba ya kiwango cha hadhi kijamii na pia ako katika mwangaza wa stima,” asema.