http://www.swahilihub.com/image/view/-/4135966/medRes/1778304/-/404152/-/imba.jpg

 

Msanii balozi wa utamaduni wa Kiafrika ughaibuni

Jacque Njeri

Bi Jacque Njeri anayetumia ujuzi wake wa usanifu uhariri kuunganisha picha za mazingira tofauti ili kueleza hisia zake. Picha/HISANI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  09:53

Kwa Mukhtasari

Jacque Njeri anatumia picha kuonyesha tamaduni za Kenya katika ulingo wa kimataifa.

 

ANATUMIA picha kuonyesha tamaduni za nchini katika ulingo wa kimataifa.

Ni kazi ambayo Bi Jacque Njeri ameifanya kwa mwaka mmoja sasa na licha ya muda huu mfupi tayari imeanza kutambulika hata kimataifa hasa kutokana na mradi wake wa MaaSci.

Mradi huu unaoangazia utamaduni wa jamii ya Wamaasai umepata umaarufu sio tu hapa nchini bali pia kimataifa kiasi cha kuangaziwa na vyombo vya habari vya mbali.

Katika mradi huu ameunganisha picha zinazoonyesha watu wa jamii ya Maasai katika shughuli zao za kawaida huku wakiwa wamevalia mavazi yao ya kitamaduni, pamoja na zile za teknolojia ya masuala ya angani.

“Katika mradi huo nimeunda mji wa kubuni kwa jina Tatooine unaoangaziwa kwenye filamu ya “Star Wars” huku nikishirikisha utamaduni wa watu wa jamii hii,” aeleza.

Baadhi ya kazi zake zinaonyesha wanawake kama viumbe vya kubuni wakiwa na sehemu za mwili za mwili za vyuma huku wakiwa wamevalia vilulu vya Kimaasai kwenye shingo zao. Pia mojawapo ya picha zake inaonyesha wazee wa Kimaasai wakiwa wameshikilia bakora zao kwenye chombo cha safari za angani,” aeleza.

Madhumuni yake ya kufanya mradi huu ni kuonyesha utamaduni wa Kiafrika na hasa wa jamii ya Wamaasai ukiwa umechanganywa na teknolojia ya sayansi ya safari za angani. “Pia nilipata chocheo la kujumuisha utamaduni wa Kimaasaai kwani mara nyingi huwakilisha Kenya na hii ni mbinu ya kutangaza nchi hii,” aeleza.

Mbali na kuwa ujuzi wake umechochewa na taaluma yake katika usanifu uhariri, Bi Njeri anasema kuwa uchu wake katika kazi hii unatokana na nia yake ya kutaka wanawake kuhusika na kazi kama hii ambayo katika jadi imekuwa ikihusishwa na jinsia ya kiume.

“Taaluma ya upigaji picha au usanifu uhariri kwa kawaida huhusishwa na jinsia ya kiume na kazi yangu inadhamiria kubadilisha dhana hiyo. Nia yangu pia ni kuwapa mabinti kuwa pia wao wanaweza fanya vyema katika taaluma hii,” asema.

Kazi yake kwa kawaida huchochewa na mazingira halisi vile vile wanasanaa wengine kama vile Pablo Picasso kutoka Uhispania.

“Mimi hufikiria sana kila ninapotazama mambo yanayofanyika karibu nami. Wakati mwingine wazo langu huchochewa na neno. Neno MaaSci linalojumuisha Maasai na sayansi ndilo lililokuwa chocheo langu katika mradi huu kwani kwa kawaida mimi hufurahishwa na ujumi wa jamii ya wa Maasai,” asema.

Lakini kazi yake haihusishi tu mradi wa MaaSci, mapema mwaka huu alisanifu upya stampu za posta na hata kuuza icha hizo.

Ufanisi wake hata hivyo haujanasua kazi yake kutokana na vizingiti huku mara kwa mara akilazimika kustahimili ukosoaji mkali dhidi ya kazi yake.

“Nakumbuka kazi yangu ilipoangaziwa na shirika la kimataifa la habari la CNN kuna baadhi ya watu hasa kutoka mataifa ya kigeni waliohoji kuwa sanaa yangu ni sawa na ndoto kwani kiwango hicho cha teknolojia hakiko barani Afrika,” aeleza.

Lakini badala ya kufa moyo anasema maoni hayo ndio yalimpa mwamko mpya wa kuimarisha kazi yake zaidi. “Unapopata maoni ya aina hii kutoka watu wa mbali bila shaka inamaanisha kuwa kuna kitu kizuri unachofanya,” aeleza.

Kwa sasa anafanyia kazi mradi wake mpya kwa jina Mau Mau Dreams. “Kazi hii inanuiwa kuonyesha picha ya kimawazo ya Kenya endapo haingetawaliwa na wakoloni huku wahusika wakuu wakiwa majasiri waliopigania uhuru wa taifa hili,” asema.