Msomi, mtaalamu wa Fasihi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi

Evans Mbuthia

Dkt Evans Mbuthia ni msomi, mtaalamu wa Fasihi na mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Nairobi. Picha/CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, December 29  2016 at  10:27

Kwa Mukhtasari

Dkt Evans Mbuthia – msomi, mtaalamu wa fasihi na mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

UPO mahali ulipo kwa sababu kuna mtu aliyetambua ukubwa wa uwezo wako na hivyo akakuchochea kufikia kilele cha ndoto zako maishani.

Ujasiri wa kukabili changamoto mpya na imani kuwa hakuna lisilowezekana ni siri kubwa ya kufanikiwa katika taaluma yoyote ile iwayo.

Maamuzi yoyote unayoyafanya yakizidi uwezo na nguvu ulizonazo, basi huangukia kwenye udhaifu ulionao na matokeo yake ni kwamba utakosa mambo mengi muhimu kati ya yale uliyoyatarajia.

Uwajibikaji, ari ya kufanya kazi bila kufadhaika wala kutamauka pamoja na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika jambo lolote analolifanya mtu ni sifa muhimu na za lazima kwa yeyote kuwa nazo ili afanikiwe katika maazimio yake.

Huu ni ushauri wa Dkt Evans Mbuthia – msomi, mtaalamu wa fasihi na mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Maisha ya Awali

Baada ya kupata elimu ya awali katika shule ya msingi ya Starehe Boys’ Centre jijini Nairobi, Mbuthia aliendeleza masomo yake ya sekondari katika shule iyo hiyo hadi mwishoni mwa mwaka wa 1980.

Anakiri kwamba mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili zilipandwa ndani yake tangu utotoni kutokana na ulazima wa kuitumia lugha hiyo kwa lengo la kudumisha mawasiliano na watu wa jamii mbalimbali walioishi nao Nairobi ambako Mbuthia alizaliwa na kulelewa.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1981 kusomea masuala ya Siasa, Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza.

Ingawa hivyo, baadaye alizamia zaidi Kiswahili na masuala ya Siasa.

Japo marehemu Yusuf King’ala, Bi Kang’ethe na Bw Ernest Ahere (marehemu) tayari walikuwa wamemtia Mbuthia ilhamu ya kukichangamkia Kiswahili akiwa mwanafunzi wa shule ya upili, jambo ambalo hakulijua kabisa ni kwamba angefundishwa na wataalamu watajika katika ulimwengu wa Kiswahili kama vile Kazungu Kadenge na Maprofesa Mohamed Bakari na Jay Kitsao (marehemu) katika kiwango cha Chuo Kikuu.

Anahisi kwamba ufanisi wake katika Kiswahili ulichangiwa pakubwa na yeye kufundishwa na watu ambao zaidi ya kubobea katika taaluma, waliipenda na kutawaliwa na msukumo wa ndani wa kuipigia chapuo lugha hiyo.

Isitoshe, darasa lilikuwa na idadi ndogo ya wanafunzi ambao walikuwa na hamasa ya kujisomea vitabu mbalimbali vya Kiswahili tofauti kabisa na jinsi hali ilivyo siku hizi.

Mchango Kitaaluma

Baada ya kuhitimu kwa kupata shahada ya kwanza mnamo 1985, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Mbuthia kufundisha Kiswahili katika shule ya upili ya Kahuhia Girls, Murang’a alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili.

Miaka miwili baadaye, alihamia Moi Forces Academy, Nairobi alikohudumu hadi mwishoni mwa 1989.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma na kukabiliana na changamoto mpya katika mazingira mapya ya kufanyia kazi ilimchochea Mbuthia kurejea katika Chuo Kikuu kusomea shahada ya Uzamili mnamo 1989.

Alifuzu mwishoni mwa 1991 baada ya kuandaa na kuwasilisha tasnifu Uchunguzi wa Kazi za Mshairi Boukheit Amana chini ya usimamizi na uelekezi wa mwanaisimu Mung’ania na marehemu Profesa Jay Kitsao.

Baadaye alifundisha Kiswahili kwa muda mfupi katika Chuo cha Ufundi cha Kinyanjui (KTTI), Riruta.

Anakiri kwamba hatua ya kutotahiniwa kwa Kiswahili kama masomo mengine katika kiwango hicho cha elimu ilichangia pakubwa mapuuza ya wanafunzi wengi ambao walikosa kuionea fahari lugha hiyo.

Ingawa hivyo, Mbuthia alibadilisha pakubwa mbinu za usomaji na ufundishaji wa Kiswahili chuoni Kinyanjui kiasi kwamba wanafunzi walianza kuichapukia lugha hiyo kwa ufasaha kwa lengo la kuimarisha ujuzi wao wa kimawasiliano.

Mbali na kuwapenda, kuwaheshimu, kuwajali na kuwathamini wanafunzi wake wote, Mbuthia aliwahimiza pakubwa kuhusu umuhimu wa Kiswahili na upekee wa mchango wa lugha hiyo katika kufanikiwa kwao baadaye kitaaluma.

Mnamo 1992, aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Nairobi anakofundisha Kiswahili hadi sasa.

Mbali na kufundisha, Mbuthia kwa sasa ndiye Mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi (CHAKINA) ambacho kiliasisiwa mnamo 1979.

Mnamo 2005, alihitimu kwa kupata shahada ya Uzamifu (phD) baada ya kuwasilisha tasnifu A Thematic & Stylistic Analysis of Kiswahili Short Stories chini ya usimamizi wa Dkt Marete na Maprofesa Monica Mweseli na Kyallo Wadi Wamitila.

Ili kufanikisha utafiti wake kwa minajili ya kutimiza mahitaji ya mada hiyo, ilimjuzu Mbuthia kusoma na kuzichanganua hadithi fupi zote zilizokuwa zimechapishwa humu nchini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2005.

Katika kipindi hicho, Mbuthia alikuwa mshiriki katika kipindi Lugha Yetu kilichokuwa kikiendeshwa na Profesa Timothy Arege katika kituo cha KBC Idhaa ya Taifa.

Uandishi

Mbuthia anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu alipoandaa tasnifu katika jitihada za kutimiza baadhi ya mahitaji ya kuhitimu shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Baadaye alishirikiana na Prof Wamitila kuandika Mwongozo wa Kitumbua Kimeingia Mchanga ambao ulichapishwa na kampuni ya Longhorn.

Mwongozo wa Mstahiki Meya ni kitabu chake cha pili ambacho kilichapishwa na kampuni ya Spotlight.

Mbuthia anajivunia hadithi fupi Aliyemtapeli Mzalendo katika mkusanyiko wa Kunani Marekani; kitabu ambacho kilihaririwa na Profesa Iribemwangi kisha kikachapishwa na East African Educational Publishers (EAEP).

Isitoshe, ana hadithi fupi Anga Kavu katika mkusanyiko wa Mwavyaji wa Roho na Hadithi Nyingine ambao uliohaririwa na Dkt Leonard Sanja ambaye pia ni mwandishi mahiri na mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mbali na riwaya pamoja na kazi nyingi za watoto, Mbuthia ambaye anaazimia kukwea ngazi za kiusomi hata zaidi, ametunga pia idadi kubwa ya hadithi fupi ambazo baadhi zitachapishwa na kampuni mbalimbali kuanzia mwaka wa 2017.

Mbuthia ambaye kwa pamoja na mkewe amejaliwa watoto wawili anajivunia pia kuwalea kitaaluma wasomi wengi wakiwa ni pamoja na Prof Iribemwangi na Madaktari Sanja, Miriam Musonye na Alex Wanjala ambao kwa sasa ni wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.