http://www.swahilihub.com/image/view/-/3967920/medRes/1669486/-/psi9j3z/-/kil.jpg

 

Msongamano magerezani upunguzwe

Nehemiah Osoro

Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Profesa Nehemiah Osoro (aliyesimama) akifuatiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na baadaye Rais Magufuli. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, April 10  2018 at  10:30

Kwa Muhtasari

Kwa muda mrefu sana wadau mbalimbali wa masuala ya sheria wamekuwa wakitoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuona uwezekano wa kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

 

KWA muda mrefu sana wadau mbalimbali wa masuala ya sheria wamekuwa wakitoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuona uwezekano wa kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

Kuna wakati ilipendekezwa kuwa watu wanaopatikana na makosa madogomadogo wapewe vifungo vya nje, ambavyo huambatana na wafungwa hao kufanya kazi za maendeleo au usafi katika maeneo ya serikali chini ya usimamizi maalumu.

Vilevile, kuna wakati baadhi ya wabunge walijitolea kutafuta fedha ili kuwalipia wafungwa ambao kama wangelipa faini wasingekuwa ndani.

Mpango huo ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema ambaye alitaka kuhakikisha magereza yanabaki na idadi inayotosheleza majengo yaliyopo.

Hatujui mikakati hiyo imekwamia wapi maana Jumatatu bungeni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusufu Masauni alisema hadi sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na wafungwa na mahabusu zaidi ya 40,000 wakati uwezo wa magereza ni kubeba wafungwa na mahabusu 30,000. Hii ina maana kwamba magereza yamezidiwa wafungwa na mahabusu wapatao 10,000.

Tunafahamu kwamba baadhi ya watuhumiwa hulazimika kuwekwa ndani kwa usalama wao, pia tunafahamu kwamba baadhi yao huwekwa ndani kwa kuwa wakiwa nje wataharibu ushahidi. Hata hivyo, idadi yao haiwezi kuwa kubwa kiasi hicho.

Hivi kwa nini, mathalan mtu anakamatwa ananyimwa dhamana, anawekwa kituo cha polisi kwa siku mbili, tatu, nne lakini akifika kortini anapewa? Hivi kwa nini mtu ananyimwa dhamana kwa kosa ambalo dhamana iko wazi?

Ieleweke kwamba eneo lenye msongamano mkubwa wa wafungwa, hata dhana ya kuwa eneo la kurekebisha wafungwa kwa kuwapa elimu ya ufundi na kilimo inaweza kupotea, maana wanaweza kuambukizana magonjwa kama kifua kikuu, kuharisha, kuhara damu, kipindupindu na hata ebola na zika.

Wafungwa wagonjwa hugeuka kuwa mzigo na hasara kwa Serikali maana hawatumikii tena kuzalisha bali kila siku hutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuwapeleka hospitali kwaajili ya matibabu.

Ndiyo maana tunaunga mkono uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba wabunge wapeleke bungeni hoja ya kufanya marekebisho ya sheria itakayosaidia kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Hata hivyo, Serikali ama ijenge magereza mengine au iangalie uwezekano wa kuwapunguza waliopo.

Serikali inajua baadhi ya watu hukamatwa kwa makosa madogomadogo sana lakini huigharimu pakubwa katika kuwatunza kwa chakula, malazi na matibabu.

Usawa

Wafungwa ni watu sawa na sisi isipokuwa baadhi yao ama wamepotoka kimaadili, baadhi wakajikuta wameiba au kampuni zao zimeibia Serikali au watumishi wamechanganya hesabu za malipo au makosa ya uchochezi. Hao wote wakijirekebisha wengi wao hurudi na kuwa watu wema.

Tunasema wakijirekebisha hurudi kuwa watu wema maana magereza kwa lugha nyingine ni chuo cha mafunzo ambacho humpokea yeyote.

Kwa kuwa hakuna mtu aliyezaliwa ili afungwe na kwa kuwa mtindo wa maisha husababisha watu kufanya makosa, ni vyema mazingira ya magereza yakaboreshwa na kupunguza msongamano kwa kiasi kikubwa.

Tunashauri magereza yawe na shughuli za kufanya, kulima mashamba, kutengeneza samani, kushona ili wafungwa waweze kuzalisha baada ya kuwa mzigo wote wa kuwatunza utoke serikalini.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647